Utata kuhusu usalama maji ya chupa

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WATANZANIA wapo njia panda kutokana na kuzuka kwa hoja mbili za kitaalamu zinazokinzana kuhusu ubora wa maji ya kunywa ya chupa yanayotengenezwa na kuuzwa nchini.

Wataalamu hao wenye ushawishi kutokana na nafasi walizonazo katika jamii ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Profesa Tolly Mbwete na Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekelege.

Katika maelezo hayo, Profesa Mbwete alisema aina nyingi za maji ya kunywa si salama, wakati mkuu wa TBS, taasisi inayoshughulika na uthibitishaji wa ubora wa bidhaa, akipinga na kusisitiza kuwa maji hayo ni salama.

Kauli ya Profesa Mbwete aliitoa akizingatia utafiti wa kitaalamu ulifanywa na chuo chake kwa maiaka mitano na kubaini kwamba "..aina nyingi za maji ya chupa si salama na yanatengenezwa kienyeji katika viwanda feki vilivyoko katika mazingira machafu".
Alitoa taarifa hizo katika mhadhara wa kiprofesa uliofanyika katika hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam mapema Desemba mwaka jana.

Alifafanua kwamba watumiaji wengi wa maji ya chupa wana imani kubwa kwamba yana ubora, lakini ukweli ni kwamba hayana viwango vya ubora.

Kauli hiyo ilimfanya Ekelege kuibuka ili kukanusha hasa ikizingatia kwamba aina nyingi za maji zina nembo ya TBS ya kuthibitisha yana ubora wa viwango vya kimataifa na ni salama kwa afya ya mtumiaji.
Ekelege alisema utafiti wa Profesa Mbwete hauna msingi na kuwa watu waendelee kunywa maji ya chupa yenye nembo yao ya TBS.
“Wananchi puuzieni taarifa potofu na zisizo na msingi zilizotolewa kuhusiana na ubora wa maji, endeleeni kunywa maji ya chupa yaliyothibitishwa na TBS," alisema Ekelege.

Ekelege alisema maofisa wa shirika hilo, wamekuwa wakifanya ukaguzi wa kushtukiza mara kwa mara katika viwanda na sokoni ili kuhakikisha wazalishaji wa maji ya chupa ya kunywa wanazingatia ubora.
Baada ya hoja hizo mbili kuibuka, ni dhahiri Watanzania wamebaki njia panda kwani hawaelewi wafuate kauli gani baina ya kauli hizo mbili.

Baadhi ya waliozunguma za Mwananchi walieleza kushangazwa na kauli ya mkurugenzi wa TBS, aliyepewa dhamana ya kulinda afya za Watanzania akipinga vikali utafiti wa kisayansi wa chuo hicho kinachotegemewa na nchi kutoa wataalamu watakaolisaidia Taifa katika nyanja mbalimbali.

Akizunguma na Mananchi, Profesa Mbwete ameutaka umma wa Watanzania kutambua kwamba utafiti wake ni wa kisomi ambao haukuwa na lengo la kumnufaisha mtu binafsi.

“Mimi ni msomi na nilifanya utafiti huu wa kina na kisayansi, si kwa ajili ya kupata pesa, bali kuwapa wananchi taarifa ambazo zitawasaidia. Kama kweli hao TBS wapo makini, watoe takwimu zinazoonyesha kuwa wanapima maji hayo,”
Profesa Mbwete alisema: "Watu waende Kariakoo wakaone jinsi maji yanavyotengenezwa kiholela katika vibanda tena vingine vipo pembeni ya vyoo".

Alisema kuna viwanda vya kienyeji vinavyotengeneza maji ya chupa kwa kuokoteza chupa zilizotumika, kununua nembo kwa njia za panya toka viwandani na kisha kuweka vifuniko kwa mashine maalumu.

Mbwete anasema kuwa nchi hii inatawaliwa na rushwa na ndiyo maana maisha ya Watanzania yanapotea bila sababu.
Alikwenda mbali zaidi na kutoa mfano wa jinsi Watanzania wanavyodhulumiwa akizinyooshea kidole hospitali na mahakama ambako alisema watu wanakosa haki zao na kupoteza maisha na kwamba hivyo ndivyo ilivyo hata kwa maji ya kunywa ya chupa.
“Inawezekana shirika la viwango linatumiwa na mafisadi, nilipotoa ule mhadhara nilikuwa nawaeleza Watanzania ukweli, sina tamaa ya pesa mimi, nia ilikuwa ni kuokoa maisha yao na si vinginevyo,” alisema Profesa Mbwete.

Profesa Mbwete alifanya utafiti huo kwa muda usiopungua miaka mitano katika miji mikuu Tanzania na kugundua kuwa maji ya chupa hayapimwi mara kwa mara na TBS, hivyo kuruhusu kuingizwa sokoni bidhaa zilizotengenezwa kiholela.

Aliongeza kuwa maji ya chupa si salama kwa asilimia mia moja na kwamba miongoni mwa athari za maji hayo ni kusababisha ugonjwa wa akili kwa watumiaji kama hatua za udhibiti wa ukaguzi wa mara kwa mara hazitafanyika.

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliitaka TBS nayo itoe ushahidi wa kitaalamu na kiuchunguzi kuhusu maji ya kunywa ili kuusaidia umma kufanya uamuzi sahihi.

Walisema kuna baadhi ya maji yamekuwa yakionekana yamefungwa vizuri mitaani, lakini ndani yake kuna vielea vinavyoonekana kwa macho, hali inayothibitisha baadhi ya maji kutokuwa salama.
 
Back
Top Bottom