Utaratibu wa likizo Mbalimbali kwa mujibu wa Sheria ya kazi

Sildenafil Citrate

JF-Expert Member
Jan 29, 2021
573
2,553
Wafanyakazi wafuatao wanastahili likizo ya malipo, Waliofanya kazi kwa zaidi ya miezi sita mfululizo, Wafanyakazi wa msimu, Wafanyakazi waliofanya kazi kwa kipindi tofauti kwa mwajiri mmoja katika mwaka iwapo vipindi husika vikijumlishwa vitazidi miezi sita.

Walioajiriwa katika utumishi wa majeshi hawatahusika katika utaratibu wa likizo hizi ikiwemo:-
(a) Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(b) Polisi
(c) Magereza
(d) Jeshi la Kujenga Taifa

Mfanyakazi ana haki ya kupata likizo zifuatazo:
  • Likizo ya mwaka.
  • Likizo ya uzazi kwa akina mama.
  • Likizo ya ugonjwa
  • Likizo ya Uzazi kwa akina baba
  • Likizo ya huruma au majukumu ya kifamilia.
  • Likizo ya mwaka mzunguko wake ni miezi 12 na likizo nyingine zilizobaki mzunguko wake ni miezi 36.
Likizo ya mwaka
  • Mfanyakazi anastahili kupewa likizo ya siku 28 mfululizo katika mzunguko wa miezi 12.
  • Siku za likizo zinaweza kukatwa na mwajiri iwapo mfanyakazi alipewa ruhusa mbalimbali.
  • Mwajiri anaweza kuamua siku ya kuanza likizo mfanyakazi ndani ya miezi sita kuanzia siku ambayo mfanyakazi alistahili kuanza likizo.
  • Muda wa kuanza likizo baada ya miezi 6 unaweza kuongezwa kwa makubaliano iwapo yapo mahitaji ya uendeshaji na nyongeza ya muda wa kuanza likizo isizidi miezi 12.
  • Mfanyakazi hapaswi kufanya kazi wakati wa likizo.
  • Hairuhisiwi kumlipa mfanyakazi pesa badala ya likizo (kununua likizo) isipokuwa tu wakati wa kusitisha ajira.
  • Likizo ya mwaka haitakiwi kuchukuliwa wakati wa likizo nyingine au wakati wa kipindi cha notisi ya kusitisha ajira.
  • Mwajiri ni lazima amlipe mfanyakazi mshahara wake wakati wa likizo.
  • Mwajiri ni lazima amlipe mfanyakazi malipo mengine yanayoambatana na likizo kwa mujibu wa Tamko au Amri ya kima cha chini cha mshahara na masharti ya ajira.
Likizo ya Uzazi kina mama
  • Mfanyakazi anastahili likizo ya uzazi ya malipo ya siku themanini na nne (84) au siku mia moja (100) iwapo atajifungua mtoto zaidi ya mmoja katika mzunguko wa miezi 36.
  • Mfanyakazi analo jukumu la kutoa notisi ya ujauzito kwa mwajiri miezi mitatu kabla ya tarehe anayotarajia kujifungua. NOTISI hiyo inapaswa iambatane na uthibitisho kutoka kwa Daktari.
  • Mfanyakazi anaweza kuanza likizo ya uzazi wiki nne kabla ya tarehe anayotarajia kujifungua au kabla ya hapo kwa uthibitisho wa Daktari.
  • Mfanyakazi anaweza kuanza kazi wiki sita baada ya kujifungua. Isipokuwa kama daktari atathibitisha kuwa anaweza kuanza kazi kabla ya muda huo kumalizika.
  • Mwajiri anakatazwa kumtaka au kumruhusu mfanyakazi mjamzito au anayenyonyesha kufanya kazi zenye madhara kwa afya ya mfanyakazi huyo au afya ya mtoto wake.
  • Endapo kazi za kawaida za mfanyakazi zina madhara kwa afya yake au ya mtoto wake, mwajiri ni lazima amtafutie kazi nyingine kwa masharti yale yale ya ajira yake.
  • Mfanyakazi anastahili kupewa saa mbili (2) kila siku kwa ajili ya kunyonyesha.
  • Mwajiri anawajibika kutoa likizo ya malipo ya uzazi kwa vipindi vinne tu.
  • Endapo mtoto aliyezaliwa atafariki ndani ya mwaka mmoja tangu kuzaliwa, na mfanyakazi akapata mtoto mwingine ndani ya mzunguko huohuo wa likizo, mfanyakazi atastahili kupata likizo nyingine ya malipo ya siku themanini na nne (84).
  • Ni kinyume cha Sheria kumwachisha kazi mfanyakazi kwa sababu ya ujauzito au majukumu ya kifamilia.
  • Mfanyakazi aliyemaliza likizo ya uzazi ataendelea na ajira yake kwa masharti yaleyale ya ajira yake.
Likizo ya Uzazi ya kina baba
  • Mfanyakazi anastahili angalau siku tatu (3) za likizo ya uzazi ya baba katika mzunguko wa miezi thelathini na sita (36) bila kujali idadi ya matukio.
  • Mfanyakazi atapoteza haki za likizo endapo atashindwa kuchukua likizo hiyo ndani ya siku saba (7) baada ya mtoto kuzaliwa.
  • Mfanyakazi analo jukumu la kuthibitisha mtoto aliyezaliwa ni wake.
Likizo ya Ugonjwa
  • Mfanyakazi anastahili likizo ya ugonjwa ya angalau siku 126 katika mzunguko wa miezi 36.
  • Katika siku 63 za kwanza mfanyakazi anastahili kulipwa mshahara kamili na katika siku 63 zinazofuata anastahili kulipwa nusu mshahara.
  • Kabla ya kuchukua likizo ya ugonjwa mfanyakazi anapaswa kuwasilisha kwa Mwajiri uthibitisho wa Daktari.
  • Endapo mfanyakazi anastahili kulipwa wakati wa likizo ya ugonjwa kwa mujibu wa Sheria, mfuko wowote au makubaliano ya pamoja, Mwajiri atakuwa hana jukumu la kumlipa mfanyakazi huyo wakati wa likizo.
Likizo ya Huruma au Majukumu ya Kifamilia
Mfanyakazi anastahili angalau siku nne (4) za likizo ya malipo katika mzunguko
wa miezi 36 bila kujali idadi ya matukio kwa sababu zifuatazo:
  • Kuugua au kifo cha mtoto.
  • Kifo cha mke/mume, mzazi, babu, bibi, mjukuu au ndugu wa kuzaliwa.
Mfanyakazi anaweza kupewa siku zaidi ya nne (4) na mwajiri kwa tukio moja au matukio mengine katika mzunguko wa likizo, siku ambazo zinaweza kupunguzwa katika likizo ya mwaka au kutolipwa mshahara wa siku hizo.

Angalizo:
Siku za likizo zinaweza kuongezwa kupitia makubaliano ya pamoja au kanuni za mwajiri.
 
Back
Top Bottom