Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 34,171
- 79,630
USITAFUTE PESA, IFANYE PESA IKUTAFUTE YENYEWE
Na, Robert Heriel
Ndoto ya watu wengi ni kupata pesa zitakazowafanya waishi maisha mazuri. Ndio maana watu wanahangaika usiku na mchana kutafuta pesa, watu wanahangaika mijini na vijijini kutafuta pesa, majini na nchi kavu, mashimoni na angani, kote watu huhangaika. Kutafuta pesa.
Kitu pekee watu wengi wasichokijua ni kuwa, jinsi unavyohangaika kutafuta pesa ndivyo unavyoikimbiza na kamwe hutoweza kuipata. Kwa nini hutaweza kuipata? Ni kwa sababu huwezi tafuta kitu ambacho kipo na unakiona. Vitu vitafutwavyo ni vitu visivyoonekana, vitu ambavyo havijulikani vipo wapi. Lakini hakuna asiyejua mahali pesa ilipo, nani asiyejua kuwa pesa ipo mikononi mwa watu, hilo kila mtu analijua. Ikiwa unafahamu pesa iko mikononi mwa watu iweje useme unatafuta pesa, ona hata wewe unavyoshangaa.
Pesa ni kama Bahari, ni kama ziwa. Siku zote zipo na zitaendelea kuwepo. Ukiamua kwenda kuzichota utazipata kulingana na chombo ulichoenda nacho, lakini unachopaswa kujua ni kuwa haijalishi utachukua chombo kikubwa kiasi gani ukaenda kwenye bahari ya pesa na ukakijaza, pesa hizo lazima zitaisha tuu. Na wengi ndivyo tunavyofanya, kila siku tunaamka asubuhi na kurudi jioni tukiwa tumeenda kujaza vyombo vyetu mapesa, ajabu ni kuwa kesho tena tutaenda kuchota, huko pengine tutakuta foleni kubwa.
Ni wachache wenye akili ya kuchimba mto au mfereji unaounganisha bahari ya pesa na mifuko yetu ili pesa zitufuate bila ya sisi kwenda kuzichota.
Siri ya pesa ipo katika kuifanya pesa ikufuate yenyewe na wala usiihangiikie kukufuata, na hapa ndipo kazi ilipo. Kutafuta pesa ni jambo rahisi sana kwani unatafuta kitu ambacho unajua kipo na unajua kipo wapi. Lakini kuzifanya zile pesa zikufuate yaani zitoke zilipo zije zenye huo ndio mtihani ambao wengi tunashindwa.
Kuzitafuta pesa ni kuzitumikia, kuhangaika kila siku ili uzipate. Nina uhakika watu wengi ni watafutaji wazuri wa pesa lakini kamwe hawatakuja kuzishika pesa kwa sababu wanatafuta kitu kilichopo, na kwa kawaida huwezi kutafuta kitu kilichopo unachojua kipo wapi.
Kila mtu anauwezo wa kuzifanya pesa zimtafute, kuzifanya pesa zimtumikie yeye badala ya yeye kuwa mtumwa wa kuzitafuta. Kila mtu anakitu ambacho pesa inakihitaji. kitu hicho ndicho kitaifanya pesa iwe mtumwa wako. Sio wewe uone kitu cha muhimu kwenye pesa, bali pesa ione umuhimu wako kwake.
Watu wote wanaoona pesa ni muhimu wengi huishia kuwa masikini, huishi kwenye mateso na kuhangaika. Lakini watu wote wenye pesa wanajua wao ni muhimu kuliko pesa, na wamezifanya pesa zijione kuwa hazina umuhimu zaidi yao.
Mtu hutafuta kile kilicho cha muhimu, halikadhalika kwa pesa. Pesa hutafuta mtu muhimu kuliko yenyewe ilivyo. Huwezi kumiliki pesa ikiwa yenyewe inaona wewe sio muhimu kwake. Haikutegemee kwa lolote, ndio maana mtu akitaka aipate pesa huifanya pesa imtegemee. Yaani pesa inakuwa tegemezi kwako. Yaani bila wewe pesa haina maana, na sio bila pesa wewe huna maana. Sijui kama naeleweka.
Ili pesa ikufuate lazima ufanye jambo fulani kwa kiwango kikubwa ambacho wengine hawawezi kukifanya, jambo hilo lazima litatue shida za watu wengi, au watu wachache wenye uwezo.
Lazima ufanye jambo fulani kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu. Pesa haina kawaida ya kumfuata mtu mzembe, asiyejiamini, asiyejiona kuwa yeye ni wathamani.
Zingatia; Unaweza ukawa unaweza jambo fulani kwa kiwango cha juu, na ukalifanya kwa ufanisi na weledi lakini ukawa hujiamini, yaani unaona pesa ni kubwa kuliko kazi yako, na hapo ndipo unakuwa mtumwa wa pesa. Utashangaa mtu anakuambia nikupe elfu 20 unifanyie kazi yangu, wakati kazi hiyo ni elfu 50, kwa vile hujiamini, au unaitumikia pesa, itakubidi ukubali, kwa kisingizio cha njaa, au unauhitaji wa pesa, yaani usipochukua pesa hiyo hautapata pesa nyingine, kumbe hujiamini, nani alikuambia kukataa pesa ndogo ambayo hailingani na kazi yako utakosa pesa, huko ni kutojiamini.
Biblia inasema; Usikubali mtu adharau ujana wako.
Nami Taikon nasema; Usikubali mtu adharau kazi yako ikiwa unaiamini, na unajua unaifanya kwa kiwango cha juu kabisa.
Kuidharau kazi yako wewe mwenyewe unaifanya pesa nayo ikudharau. Mtu yeyote anakuamulia akupe kiasi chochote atakacho bila kuangalia kazi uliyoifanya.
Ni bora uwe na wateja wachache wanaoheshimu kazi uifanyao kuliko kuwa na wateja lundo wanaokupa pesa za fedheha wakati wewe unapiga kazi za kimataifa.
Nakuhakikishia Ukijiamini, ukipiga kazi kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu pesa inakufuata yenyewe na wala wewe huna muda wa kuhangaika nayo.
Pesa inahitaji uijengee Mkondo wake, Yaani uaminifu, kwamba kazi zako hazibadiliki, unazifanya kwa kiwango kile kile na kwa namna ile ile mlivyokubaliana. Kama mtu anataka kazi yake ifanyike hivi, mfanyie vile vile atakavyo kama unachakumshauri mshauri ili ionekane vizuri.
Pesa hufuata Mkondo, yaani njia ile ile uliyoitengenezea. Kama hujatengeneza mkondo wa pesa,kamwe pesa haitoweza kukufuata. Wewe ndio utaenda kwenye mikondo ya watu kuchota pesa kwao, siku wakikunyima utaanza kuhangaika.
Usiifuate pesa, usiikimbilie kwani hunauwezo wa kuishika, hata ungeikimbilia kwa kasi kubwa vipi bado usingeikamata.
Vijana mliomaliza chuo, vijana mliomtaani, tengenezeni mifumo pesa ziwafuate. Msihangaike kuzifuata pesa, mtapoteza muda wenu bure.
Namna ya kuifanya pesa ikufate:
1. KUWA MBOBEVU KATIKA FANI YAKO
Hakikisha unapata elimu na ujuzi kuhusu fani uitakayo, iwe ni shule au popote pale lakini hakikisha unabobea.
Jitahidi kujidhatiti na kuwa mweledi na mfanisi katika fani yako. Kama ni Daktari au mwalimu, au fundi, hakikisha eneo ulilopo kuwa bila ya wewe kazi haziendi, hakikisha watu waone kwako kuwa wewe ndio umeshikilia eneo hilo yaani kama utaondoka basi kampuni, au biashara au jambo lolote litakwama
Kwa kufanya hivyo pes aitakufuata mwenyewe. Hakuna mtu aliyebobea katika jambo lolote asiwe na pesa. Haijawahi kutokea.
2. KUWA NA ANUANI
Hakikisha unakuza jina lako, kuwa na sehemu ya kazi zako, yaani ofisi, na mawasiliano. Pesa haijawahi kumfuata mtu asiye na anuani. Watu wasio na anuani ndio huhangaika kuitafuta pesa. Kamwe pesa haiwezi kukufuata ikiwa haijui ni wapi unaishi, haijui jina lako na haina mawasiliano yako.
Jenga ofisi, kuza jina lako, kisha acha mawasiliano, utashangaa pesa inakufuata tuu yenyewe hata ukiwa umelala. Utashangaa mtu anatoka nchi za mbali anakufuata nyumbani kwako, hii ni kwasababu unaanuani.
Ukishafungua ofisi hakikisha unafanya kazi kwa kiwango cha kutisha, kiwango cha kimataifa, kwa uaminifu na kwa muda mliokubaliana. Watu watakuja wenyewe.
3. MILIKI WATU
Pengine utashangaa lakini hii ni siri nyingine nakupa, bila kumiliki watu kamwe huwezi pata pesa, utaitafuta mpaka ukome. Pesa haiwataki watu wasiomiliki watu kwani pesa ni watu na watu ndio hiyo hiyo pesa. Kumiliki watu ni kumiliki pesa.
Kumiliki watu kutakufanya utumie muda wao, kumbuka masaa kwa siku hayajawahi kuzidi labda kupungua. Hivyo uzalishaji wa pesa hutegemea zaidi watu. Kadiri unavyomiliki watu ndivyo unavyomiliki pesa.
Nitawezaje kumiliki watu? Nitakupa mbinu kadhaa hyapo chini
> Anzisha mradi, kisha ajiri watu, watu hao watakuzalishia wewe. Usisahau kuwapa haki zao kulingana na makubaliano
> Jenga hofu
Kama huna mradi wa kuajiri watu basi waweza jenga hofu kwa watu kisha itumie hofu yao kupata pesa. Ukishajenga hofu jifanye unaowezo wa kuondoa hofu yao. Hapo utayaona maelfu maelfu ya watu wakija kukuletea pesa ili uondoe hofu yao. Hii hutumiwa zaidi na watu wa dini na waganga wa kienyeji. Kwa kadiri unavyotishwa na kuongezewa hofu ndivyo mtu huyo anavyokuweka karibu katika milki yake. Anakutawala kisha unakuwa mtumwa wake.
> Unda tatizo kisha litatue
Ikiwa hapo juu umeshindwa kumili watu basi chukua mbinu hii. Unda tatizo ndani ya jamii kwa mfano ugonjwa ambao watu watahangaika bila ya madawa kisha wape dawa ziwatibu lakini baada ya muda hakikisha ugonjwa unajirudia ili wakuletee pesa. Mbinu hii hutumiwa na wataalamu wa madawa, watu wa madawa ya uraibu. Hii hufanya watu wawe watumwa wa jambo fulani, hivyo humilikiwa.
Niishie hapo kwa habari za mbinu za kumiliki watu.
4. MILIKI RASILIMALI
Pesa hufuata watu wenye Rasilimali kama vile ardhi, majengo, magari, mashamba, miongoni mwa mambo mengine. Kamwe pesa haijawahi kumfuata mtu asiye na vitu hivyo. Vijana wengi huwemkeza kwenye pombe, kwenye mavazi, kwa wanawake wakasahau kuwa pesa haijawahi kuwafuata watu wa dizaini hiyo. Ni vyema hata kama unapata pesa ndogo ndogo hata kama ni elfu 50 uiweke na kuiongeza mpaka ifike laki tatu ukanunue shamba. Kuliko utumie elfu 50 kununulia simu au nguo. Utakuwa mtumwa wa pesa kisha utalaumu kwa nini hupati pesa wakati muda huo pesa yenyewe inajaribu kukukimbia.
Kumiliki Rasilimali kunakupa kuaminiwa na watu, ukimuambia mtu niazime milioni tano anatumia shamba lako kukupa imani kuwa utaweza kumrejeshea, anaamini kuwa ikiwa unakiwanja basi utamrejeshea kwani hautakubali kiwanja chako kiuzwe kwa bei ya kutupa kisa milioni tano.(Huu ni mfano)
Kufikia hapa ili nisiwachoshe, nafikiri kwa sehemu nimeweza kukuleza ni namna gani tunaweza kuifanya pesa itufuate yenyewe na sio sisi kuitafuta.