Sina hakika endapo ni sahihi kwamba Dr. Ulimboka ni Mtumishi wa Serikali. Nadhani nimepata kusoma katika vyombo vya habari wakati wa ule mgomo wa kwanza wa Madaktari kuwa Dr. Ulimboka hakuwa Mtumishi wa Umma, isipokuwa Madaktari walikuwa na imani naye kuwa atawawakilisha ipasavyo kwenye madai yao dhidi ya Serikali. Kuhusu kujiunga na Vyama vya Upinzani na kupata kura za Kishujaa, nadhani pia hauko sahihi. Apate kura za kishujaa kwa kuhamasisha mgomo uliopelekea Watanzania takribani 400 kupoteza maisha kwa vifo ambavyo pengine vingeweza kuzuilika endapo Madaktari wangekuwepo kazini? Au unamuona Dr. Ulimboka ni shujaa wako kwa kuwa wewe hukufiwa na mkeo, mwanao, mjomba, shangazi, baba, mama au ndugu wakati wa mgomo ule? Kwa mtazamo wangu, nadhani ilifaa sana sasa Wananchi kwa kupitia Wabunge wa Upinzani au Chama Tawala, wakati wa Bunge hili la Bajeti WAIBANE SERIKALI ILI SASA ITOE TAKWIMU HALISI ZA IDADI KAMILI YA WATU WALIOPOTEZA MAISHA WAKATI WA MGOMO WA MADAKTARI ili tuweze kuupima huo ushujaa unaousema alioupata Dr. Ulimboka kwa vifo vya Watanzania wote hao wasio na hatia! Inawezekana vipi hakuna mtu hata mmoja kati ya Wanasiasa, Viongozi wa Dini, Wanaharakati, Wanahabari ambaye anapenda kuihoji Serikali juu ya nini tathmini ya mgomo wa madaktari kwa upande wa vifo vilivyotokea? Kwa maoni yangu nadhani kutoulizwa kwa swali hili ndipo kunakopelekea wengi wetu kuamini kuwa Suala la Dr. Ulimboka ni agenda na mtaji wa kisiasa kwa watu fulani! Hivi ni sahihi kudhani kuwa haki za binadamu zimevunjwa kwa Dr. Ulimboka kuteswa na kupigwa pekee? Vipi haki za binadamu wale wengine waliopoteza maisha kwa kukosa Daktari wa kuwawekea 'Oxygen' kule hospitali? Au kwa kukosa Daktari wa kuwafanyia upasuaji? JF ni jukwaa makini la majadiliano, na ni vyema kujadili hoja katika uwanja mpana zaidi kuliko kulitumia jukwaa hili kukwepesha hoja na kuuliza maswali yanayokidhi mahitaji mbalimbali ya kisiasa ya Wachangiaji. Ni wakati muafaka sasa tupate takwimu za ndugu zetu waliopoteza maisha ili tulipime sakata hili kwa mizani inayoeleweka. Naomba kuwasilisha..!