USHAIRI: Nakonda sababu wewe

USHAIRI: Nakonda sababu wewe

ramadhani kimweri

Senior Member
Joined
Apr 22, 2016
Posts
183
Reaction score
181
NAKONDA SABABU WEWE.

Kwanini nijiadhibu, kama kweli sikupendi
Nikavumilia tabu, kwako imenasa gundi
Kukuacha najaribu, moyo wangu siushindi
Huku kukonda nakonda, Ila sababu ni wewe.

Kila unacho tamani, mie ninakupatia
Umetaka kitu gani, kwacho sijakufanyia
Nambie wataka nini, utakacho furahia
Huku kukonda nakonda, ila sababu ni wewe.

Ninaomba ufahamu, kwako sina la kutenda
Basi usinidhulumu, kwasababu nakupenda
Huba lanipa wazimu, dawa ipo kwako nyonda
Huku kukonda nakonda, ila sababu ni wewe

Kuzuia ningeweza, ningeukataza moyo
Ni ngumu waniumiza, hayo ufanyayo siyo
Ni wewe tu nakuwaza, mbona wanendesha mbiyo
Huku kukonda nakonda, ila sababu ni wewe.

Nakondeshwa na mapenzi, nakonda kwa huba lako
Na kukuacha siwezi, unanipa babaiko
Nimekuwa kama chizi, nimeshakuwa kicheko
Huku kukonda nakonda, ila sababu ni wewe..

Mwenye mapenzi ya kweli, ndio hupata machungu
Humkuta udhalili, na adha za ulimwengu
Mie kwako sina hali, sijiwezi peke yangu
Huku kukonda nakonda, ila sababu ni wewe

Najiona hayawani, niliechanganyikiwa
Zaidi ya majununi, pendo limekataliwa
Sina amani miyoni, huwezi kunielewa
Huku kukonda nakonda, ila sababu ni wewe.

[emoji2398]Ibn kimweri.
 
Back
Top Bottom