Usaliti wa Butiama ni ukombozi - jee ndiko nchi inakoelekea?

Bikirembwe

JF-Expert Member
Feb 13, 2008
250
7
Hii ni sehemu ya makala iloandikwa katika gazeti la Tanzania Daima la Julai 2,2008. La kujiuliza ni jee mawazo ya mwandishi yanaweza kuwa kweli ukitilia maanani maamuzi ya CCM Butiama?

........Baada ya kuona usaliti dhidi ya dhamira ya Kikwete na kamati ya muafaka ya CCM na CUF ni mambo yasiyo na nguvu, chama hicho kikaenda mbele zaidi na kwa ujeuri kikaamua kumsaliti Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi aliyekuwa akitamani kuona serikali ya umoja wa kitaifa inaundwa Zanzibar, miaka 13 iliyopita, tena kikikutana hatua chache tu kutoka mahali alipopumzishwa. Hii ndiyo jeuri ya CCM.
Maamuzi haya ya CCM kimsingi yamesababisha nikumbuke moja ya makala za mwanzo kuchapwa katika safu hii wakati fulani mwaka jana, ambayo ilikuwa ikijaribu kuwakumbusha Wazanzibari na Watanzania namna Zanzibar ilivyo na kiu, haja na njaa ya mapinduzi mengine baada ya yale ya mwaka 1964 kushindwa. Makala hiyo iliandika yafuatayo:
‘‘Kikwete na wana CCM wenzake wanapaswa kutambua kwamba, Zanzibar inadai Mapinduzi mengine, na kimsingi mapinduzi hayo yanakuja. Yatakuja kwa CCM kupenda au kutopenda.
‘‘Watanzania, Wazanzibari na dunia ya wapenda mageuzi wanatakiwa kulifahamu, kulikubali na kujiandaa kwa tukio hilo linaloweza kuja wakati wowote na kuondoa usultani wa CCM Zanzibar kukubali kubeba dhamana ya makosa yake.
‘‘Mapinduzi mengine Zanzibar yanakuja. Yatakuja zama hizi wakati kina Kikwete, Karume, Maalim Seif na wenzake wa CCM na CUF wakiwa hai au hata watakapokuwa wamekufa.
‘‘Zanzibar inahitaji mapinduzi yatakayoiondolea CCM ukiritimba na dhana ya mapinduzi Daima. Zanzibar inadai mapinduzi yatakayoondoa udikteta wa CUF Pemba. Zanzibar inadai mapinduzi yatakayoondoa ubaguzi wa Wazanzibari dhidi ya Watanganyika, Wapemba dhidi ya Waunguja.
‘‘Zanzibar inadai mapinduzi ya fikra yatakayoondoa ubaguzi wa rangi, wa sisi weusi, wale Waarabu, sisi Wangazija, wale Wanyamwezi na kadhalika. Zanzibar inadai mapinduzi yatakayomaliza urithi wa hovyo kabisa wa kibaguzi wa sisi ndio CCM - ASP wale ni wabuguzi wa Ki-Hizbu.
‘‘Zanzibar inadai mapinduzi yatakayoondoa uhalali wa Waunguja kuendelea kuwatawala Wapemba. Mapinduzi ya kuondoa uhalali usio halali wa CCM kujipa dhamana ya kuvitawala visiwa hivyo kimabavu.
‘‘Iwapo CCM Zanzibar inadhani kwamba, tatizo la Zanzibar ni Maalim Seif, itakuwa ikifanya makosa ya Marekani inayofanya katika dunia ya sasa.
‘‘Wakati fulani, taifa hilo kubwa duniani lilidhani kuwa kifo cha kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini, Kim Il Sun, alipofariki dunia na ikadhaniwa kwamba huo ndio ungekuwa mwisho wa sera za kikomunisti za Juche. Ilikosea, alikuwapo Kim Jong Ill.
‘‘Ni kosa hilo hilo ambalo taifa hilo kubwa limekuwa likilifanya Iraq leo, inakodhani kuuawa kwa watoto wa Saddam na baadaye baba yao na jamaa wengine wa kiongozi huyo wa zamani wa Iraq kungemaliza mambo. Maafa yanayotokea Iraq leo yanatisha.
‘‘Si huko tu, hivi sasa taifa hilo kubwa linafuatilia kwa karibu hali ya afya ya Rais Fidel Castro wa Cuba, ambaye ni mgonjwa, likidhani kuwa kifo chake kitamaliza sera za kikomunisti za nchi hiyo ya Marekani Kusini. Hata katika hilo inajidanganya.
‘‘Kwa hakika CCM Zanzibar inapaswa kutambua kwamba Maalim Seif ameshafika hatua ya kujijenga na kuwa taasisi, na kwa bahati, kwao alipata kuwa kada mwaminifu wa chama hicho tawala ambacho kimsingi kuondoka kwake kulikuwa ni kwa kulazimika kama si kwa kulazimishwa.
‘‘Kwa sababu hiyo basi, Maalim Seif ndiye mtu wanayeweza kukaa naye meza moja wakazungumza kutokana na kuwa kwake na chembe chembe za damu ya CCM, tofauti na ilivyo kwa vijana Wazanzibari wanaoiunga mkono CUF, waliosambaa dunia nzima na ambao hawajawahi kunusa harufu ya U-CCM.
‘‘Viongozi wetu wa kisiasa na kiserikali wanapaswa kutambua kuwa, vijana hao walio ndani na nje ya Zanzibar, ndani na nje ya Tanzania, wana hasira kubwa na CCM. Wao ndio waliopiga kura ambazo wanaamini ziliibwa mwaka 1995, 2000 na 2005.
‘‘Watakapobaki wenyewe bila ya kuwapo kwa Maalim Seif, mwanasiasa mliberali, vijana hao ambao miongoni mwao wako wale waliochinja polisi mwaka 2001 na kuvishambulia kwa mawe vituo vya polisi, wakijaribu kuzifikia silaha na wengine kukimbilia nje ya nchi wanaweza wakaamua kufanya lolote litakalofanana na mapinduzi ya mwaka 1964.
‘‘Ingawa juhudi za sasa za CCM na mwenyekiti wake Kikwete, zinaweza zikawa na lengo kama lile la kina Benjamin Mkapa la kutaka kuwaridhisha wafadhili badala ya kuutazama mustakabali wa Zanzibar ki kweli kweli, mtazamo wa namna hiyo unaweza ukaja kuliweka taifa hili katika wakati mgumu siku zijazo.” (mwisho wa kunukuu).
Leo, takriban mwaka mmoja tangu makala hiyo ichapishwe, naiona haja ya mapinduzi hayo ikizidi kuongezeka. Naiona kiu, njaa na haja ya kuwa na mapinduzi hayo, likiwa ni jambo ambalo si mimi wala mwingine yeyote anayeweza kulizuia.
Sihitaji kuwa nabii kuiona dhuluma hii inayoendeshwa na CCM kwa Wazanzibari wakiwamo mashabiki wao, kwa sababu tu ya hofu yao kwa Maalim Seif na CUF yake, eti kwa kuingia katika mseto itanyakua nchi mwaka 2010, ikipanda mbegu ya anguko la awali la chama hicho tawala.
Ingawa sote tunasononeshwa na Azimio la Butiama ambalo kimsingi ni la kisaliti, bado tunaiona kazi hiyo ya CCM ikifanana na ile ya Yuda Iskariote katika Biblia, ambayo usaliti alioufanya kwa Bwana wake, ndio uliozaa dhana ya ukombozi wa Wakristo.
 
Back
Top Bottom