McLaren
JF-Expert Member
- Feb 19, 2025
- 1,076
- 3,400
Kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na kinachoendelea Tanzania, Muswada huu ambao umetengenezwa na Seneta Ted Cruz na Shaheen unasema yafuatayo:
(1) Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kinoma Afrika, kukiwa na ukuaji thabiti wa kiuchumi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kutokana na kuimarika kwa sekta muhimu, ikiwemo kilimo, madini, na utalii.
(2) Uaminifu wa Tanzania kama mshirika wa Marekani unazidi kutiliwa shaka kutokana na ukandamizaji wa kisiasa unaoendelea, kuvunjwa kwa uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza, na vizuizi vya kudumu dhidi ya uwekezaji wa Marekani.
(3) Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, uligubikwa na uingiliaji mkubwa wa kisiasa, ikiwemo uchezaji (wizi) na dosari kwenye kuhesabu kura, mambo yaliyombeba Rais aliyekuwepo madarakani Samia Suluhu Hassan na wagombea wengine wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
(4) Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, matukio mengi ya utekaji nyara na kupotea kwa watu kisiasa yalifanyika Tanzania; la hivi karibuni likiwa ni kutekwa na kupotea kwa Balozi wa Tanzania Humphrey Polepole mnamo Oktoba 6, 2025.
(5) Hatua mbalimbali za CCM, chama cha kisiasa ambacho kimeshikilia wingi wa viti bungeni na kudhibiti serikali kuu tangu kuundwa kwake mwaka 1977, zimeharibu vibaya demokrasia nchini.
(6) Kesi ya uhaini inayoendelea dhidi ya kiongozi wa upinzani wa Chadema, Tundu Lissu, mashtaka ya ugaidi dhidi ya Naibu wa Chadema John Heche, na kukamatwa kwa wanachama wengine wa upinzani, vyote vina malengo ya kisiasa na vinakusudiwa kuwazuia viongozi wa upinzani wasigombee uchaguzi.
(7) Serikali ya Tanzania imejihusisha na ukiukaji wa uhuru wa kidini, ikiwemo kufuta usajili wa taasisi za dini, unyanyasaji, kukamatwa, na mashambulizi dhidi ya viongozi wa dini, na kuweka vizuizi kwenye ibada na kutoa maoni.
(8) Wakati wa maandamano makubwa ya raia kupinga uchaguzi huo wa uongo na haramu wa Oktoba 29, 2025, Polisi wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi (JWTZ) waliua mamia ya Watanzania na kuhatarisha maisha ya raia wa Marekani na watalii waliokuwa nchini.
(9) Wakati waandamanaji wakishambuliwa na Vikosi vya Usalama, Serikali ya Tanzania ilizima intaneti, jambo lililoathiri mawasiliano, biashara, na mambo ya benki, na kuvuruga biashara ya kikanda huku nchi ikipoteza takriban dola $238,000,000.
(10) Kutokana na vurugu hizi ambazo hazijawahi kutokea, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa Tahadhari ya Usalama mnamo Oktoba 30, 2025, ukiwataka raia wa Marekani walioko nchini kujifungia ndani (shelter-in-place).
(11) Baada ya maandamano ya uchaguzi, tume ya uchaguzi ya Tanzania ilitoa matokeo yaliyopingwa, ikimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kama mshindi kwa asilimia 98 ya kura.
Msimamo wa Bunge (Sense of Congress)—
(1) Kwamba ni kwa maslahi ya usalama wa Marekani kusaidia kuzuia kufifia kwa demokrasia kwenye nchi washirika ambapo Marekani imetoa mabilioni ya dola za uwekezaji, maendeleo, na misaada;(2) Kwamba hatua za Serikali ya Tanzania zimehujumu demokrasia, zimevunja wazi haki za binadamu, zimevuruga biashara, na kuhatarisha usalama wa Watanzania, watalii, na wanadiplomasia;
(3) Kwamba hatua hizi zinaweka maslahi ya Marekani hatarini na kutishia utulivu wa kikanda;
(4) Kuunga mkono uamuzi wa kusitisha mpango wa Millennium Challenge Corporation (MCC) kwa Tanzania; na
(5) Kuonyesha mshikamano na watu wa Tanzania na kuunga mkono wito wa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu ghasia za kabla na baada ya uchaguzi ili waliofanya ukatili wawajibishwe.
FUNGU LA 4. TATHMINI UPYA YA MAREKANI NA TANZANIA
(a) TATHMINI YA UHUSIANO: Waziri wa Mambo ya Nje, akishirikiana na Waziri wa Ulinzi na wakuu wa idara nyingine, watafanya tathmini ya kina kuhusu uhusiano kati ya Marekani na Tanzania.(b) VIPENGELE: Tathmini hiyo itajumuisha -
- Uchambuzi wa mwelekeo wa demokrasia Tanzania;
- Mkakati wa mageuzi ya kidemokrasia yanayohitajika;
- Tathmini ya misaada ya usalama ili kuhakikisha Jeshi na Polisi wanaheshimu haki za binadamu na kulinda usalama wa raia na wageni;
- Tathmini ya jinsi ghasia na kuzimwa kwa intaneti kulivyoathiri biashara na uwekezaji wa Marekani;
- Tathmini ya uhusiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, ikijumuisha
(A) ushirikiano wa kijeshi na kiusalama, ikiwemo mafunzo, mazoezi, uuzaji na usambazaji wa silaha, na ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi, intelijensia, au vyombo vya doria na usalama;
(B) ushirikiano wa kiuchumi, ikiwemo uwekezaji, mikopo, na ufadhili unaohusisha mashirika ya umma ya China au kampuni zilizounganishwa nayo, na athari za shughuli hizo kwenye fursa za masoko, uwezo wa kulipa madeni, na ushindani wa kampuni za Marekani; na
(C) ushirikiano wa kisiasa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China unaolenga kudhoofisha misingi ya kidemokrasia, kuimarisha mfumo wa chama kimoja, na kujenga chuki dhidi ya Marekani na mataifa ya Magharibi ndani ya nchi na kimataifa
FUNGU LA 5. RIPOTI KUHUSU BAADHI YA VIONGOZI WA NCHINI TANZANIA
Ndani ya siku 180, Waziri wa Mambo ya Nje atatoa ripoti yenye orodha ya watu wa kigeni ambao:- Wana vyeo vya juu Serikalini, CCM, Polisi, JWTZ, au Usalama wa Taifa (TISS); na
- Wanahusika na:
- (A) Kuagiza au kusimamia utekaji na upoteaji wa watu au kukamata wapinzani na waandishi wa habari kiholela;
- (B) Kunyanyasa, kutishia, au kutumia nguvu dhidi ya waandishi wa habari na wanaharakati;
- (C) Udhibiti au kuzima intaneti na vyombo vya habari;
- (D) Ukiukaji mkubwa wa uhuru wa dini;
- (E) Kutumia mbinu za ukandamizaji wa kimataifa dhidi ya raia walioko nje ya nchi;
- (F) Mauaji ya kiholela, utesaji, au uvunjifu wa haki za binadamu;
- (G) Hatua nyingine zinazovunja Katiba ya Tanzania.
FUNGU LA 6. VIKWAZO
(a) KWA UJUMLA: Ndani ya siku 30 baada ya ripoti kutolewa, Rais anaweza kuweka vikwazo kwa watu waliotajwa.(b) VIKWAZO HIVYO NI:
- KUZUIA MALI: Rais anaweza kuzuia miamala yote ya mali za watu hao zilizoko Marekani au chini ya udhibiti wa Wamarekani.
- KUNYIMWA VISA NA KUINGIA: Hawataruhusiwa kuingia Marekani, na visa zao za sasa zitafutwa mara moja.
(d) MAANA YA MANENO: Hapa inafafanua bidhaa za kilimo, vifaa vya tiba, na dawa.
(e) KUSITISHA VIKWAZO: Rais anaweza kuondoa vikwazo ikiwa atathibitisha kuwa mtu huyo ameacha vitendo hivyo na kuna uhakika hatafanya hivyo tena.
(f) MAMBO AMBAYO HAYAHUSIKI:
- Misaada ya kibinadamu (chakula, dawa, vifaa vya tiba).
- Makubaliano ya kimataifa (kama yale ya Umoja wa Mataifa) au mambo ya usalama (intelejensia).
- Uingizaji wa bidhaa za kawaida (isipokuwa data za kiufundi).
FUNGU LA 7. MARUFUKU YA MISAADA NA UWEKEZAJI WA MAREKANI KWA TANZANIA
(a) MARUFUKU: Hakuna fedha za Marekani zitakazotolewa kwa taasisi yoyote Tanzania kwa ajili ya:- Misaada ya kiusalama;
- Mikopo, bima, au uwekezaji kutoka mashirika ya DFC, Export-Import Bank, au USTDA.
- Mageuzi ya uchaguzi ili uwe huru na wa haki;
- Kufuta kesi za kisiasa na kuwaachia huru wapinzani;
- Kuchukua hatua dhidi ya viongozi na askari waliohusika na utekaji na vurugu;
- Kuacha kuwatishia na kuwabana waandishi wa habari na wanaharakati.
FUNGU LA 8. MARUFUKU YA FEDHA ZA MCC KWA TANZANIA
(a) MARUFUKU: Hakuna fedha za MCC zitakazotolewa kwa ajili ya miradi yoyote Tanzania.(b) SHARTI: Marufuku hii itaisha tu ikiwa uongozi wa MCC utathibitisha kwa Bunge kuwa Serikali ya Tanzania imeonyesha dhamira ya dhati katika utawala wa kidemokrasia na haki.
FUNGU LA 9. KAMATI ZA BUNGE ZINAZOHUSIKA
Katika sheria hii, kamati hizo ni:- Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Matumizi ya Fedha ya Seneti;
- Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Matumizi ya Fedha ya Baraza la Wawakilishi