Urais CCM kaa la moto kwa vigogo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Urais CCM kaa la moto kwa vigogo

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MziziMkavu, Jul 2, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jul 2, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  [​IMG]Mgombea pekee wa urais CCM

  HAKUNA shaka kwamba Jakaya Mrisho Kikwete ndiye mteule wa CCM atakayegombea urais baada ya kuwa mwanachama pekee aliyechukua fomu na ambaye anazirejesha kwa mbwembwe leo, na sasa vigogo wa chama hicho watakuwa wameelekeza nguvu zao mwaka 2010.

  Hakuna sheria inayozuia wanachama wa CCM kupambana na rais aliye madarakani kuwania urais baada ya kumaliza kipindi cha kwanza, lakini chama hicho kikongwe ambacho mazingira yanatoa mwanya kwa mgombea wake kushinda, kina utamaduni wa kumuachia rais wao amalizie kipindi cha miaka kumi.

  Utamaduni huo, hata hivyo, ulipata changamoto kubwa baada ya baadhi ya wanachama kutangaza kuwa wangetumia haki yao ya kidemokrasia kuomba ridhaa ya wanachama kugombea urais, akiwemo mbunge wa Maswa, John Shibuda.

  Mbali ya Shibuda, ambaye baadaye alitangaza kwa lugha ya kishairi kutoingia kwenye kinyang'anyiro hicho, kulikuwa na habari kuwa vigogo wa CCM walikuwa wakijipanga kumsimamisha mtu mwingine kupambnana na JK kutokana na kutoridhika na utendaji wake, hasa kuwa mzito kufanya maamuzi magumu.

  Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuwa vigogo hao walijaribu hata kumshawishi waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aingie kwenye mapambano na wengine viongozi wa zamani.

  Lakini hadi jana saa 12:00 jioni alikuwa ni JK pekee aliyechukua fomu ya kuomba ridhaa ya wanachama wenzake apewe nafasi ya kumalizia kipindi chake na hakuna shaka Rais Kikwete atakuwa na kila sababu ya kurejesha fomu yake leo kwa mbwembwe.

  Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliliambia gazeti hili jana kuwa anaamini Rais Kikwete atakuwa mgombea pekee wa urais katika chama hicho kutokana na wanachama wengine kutojitokeza.
  “Sijamwona mtu mwingine (aliyekuja kuchukua fomu), labda aje kesho (leo) asubuhi. Lakini hadi sasa Kikwete yuko pekee yake,” alisema Makamba.

  Ikitokea amejitokeza kuna mwanachama ambaye atajitokeza kuchukua fomu, atalazimika kufanya kazi ambayo haitakuwa rahisi ya kuzungusha fomu hizo kwenye mikoa 10 kwa ajili ya kutafuta wanachama 250 wa kumdhamini.

  Lakini Makamba alipotakia kueleza endapo CCM imeandaa sherehe zozote kwa ajili ya kumsindikiza Kikwete, alijibu: “Haya mengine muulize naibu katibu mkuu. Mimi siwezi kusema kwa kuwa ni mkurugenzi wa uchaguzi na bado nasubiri kama kuna wagombea wengine.”

  Katibu wa itikati na uenezi wa CCM, Kapteni John Chiligati aliweka bayana kuwa wanachama wameandaa sherehe na maandamano kwa ajili ya kumsindikiza Kikwete wakati anarudisha fomu hizo.
  “Hawezi kurudisha fomu kimya kimya... huyo ni mgombea wetu pekee. Shughuli zitaanza saa 4:00 na atasindikizwa hadi ofisini kwa katibu mkuu wa CCM ambako atarejesha fomu hizo,” alisema.
  Kikwete alichukua fomu Juni 21 na kueleza kuwa serikali yake mpya itaongozwa na vipaumbele kadhaa vitavyosukumwa na misingi kumi.

  Alitaja moja ya misingi hiyo kuwa ni kuongeza kasi ya mapambano ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka itakayoenda sambamba na kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria, demokrasia na mapambano ya ubadhirifu wa mali za umma, huku akitumia kauli mbiu ya "ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi".
  Naye Habel Chidawali kutoka Dodoma anaripoti kuwa CCM jana ilikutana mjini hapa chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na kuchambua katiba ya Chama hicho kwa lengo la kuifanyia marekebisho.

  Moja ya mambo yaliyoangaliwa kwa karibu zaidi ni suala la wapigakura ambao awali katiba ilieleza kuwa wanatakiwa kuwa wawakilishi wachache na kuweka kipengele cha mabadiliko kinachotaka kura zipigwe na wanachama wote.
  “Kipengele hicho cha katiba kinapaswa kufanyiwa marekebisho kwa kuwa sasa mambo yamebadilika badala ya kura hizo kupigwa na wachache sasa CCM imepanua wigo na hivyo kura hizo zitapigwa na wanachama wote hai,” mmoja wa wajumbe wa kikao hicho alilidokeza Mwananchi.

  Lakini habari zaidi zimeeleza wajumbe pia waliipitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ili kujiridhisha kabla ya kumkabidhi mgombea wake wa urais wakati wa mkutano mkuu wa wachama hicho uliopangwa kufanyika Julai 10 hadi 11 mwaka huu.

  Ilani ya CCM ya mwaka 2010/2015 imeandaliwa na kamati maalum chini ya mwenyekiti wake ambaye ni mwanasiasa mkongwe na kada, Kingunge Ngombale Mwiru.

  chanzo Urais CCM kaa la moto kwa vigogo

  Ni nani aweza Kusimama na Kumtowa Mzee J.K. Katika Uchaguzi mkuu Ujao?
   
Loading...