Upekee vivutio Hifadhi ya Taifa Saadani kuongeza watalii

Upekee vivutio Hifadhi ya Taifa Saadani kuongeza watalii

Pfizer

JF-Expert Member
Joined
Mar 25, 2021
Posts
726
Reaction score
953
TANZANIA imebahatika kuwa na hifadhi 21 za Taifa zenye vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo baadhi havipatikani katika hifadhi za nchi zingine Afrika Mashariki na kwingineko.

Hifadhi ya Taifa ya Saadani inayopatikana Mkoa wa Pwani wilaya ya Bagamoyo na Tanga katika wilaya za Muheza na Pangani ina vivutio vingi vyenye masjabu yakiwamo makutano ya bahari na nyika na kuwafanya wanyama na binadamu kukutana kwenye fukwe kuvinjari na kuifanya kuwa hifadhi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki.
IMG-20250627-WA0009.jpg

Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani, Daud Gordon. Akielezea mambo vivutio mbalimbali vilivyopo hifadhini.

Akielezea upekee huo wa aina yake, Kaimu Mkuu wa hifadhi hiyo, Daud Gordon alisema hilo haliishii kwenye mandhari ya kuvutia tu, bali pia makundi ya wanyama zaidi ya matano wenye hadhi ya juu kama simba, tembo, twiga na pundamilia kuweza kufika ufukweni kupumzika, jambo ambalo ni adimu katika hifadhi zingine duniani.

Alisema mbali na hayo, Hifadhi ya Saadani inao msitu wa Zalaninge ambao una uoto wa asili kabisa unaochangia upatikanaji wa mvua pamoja na miti ya mikoko inayosaidia viumbe hai kama kasa kuzaliana kwa wingi katika eneo hilo.

Gordon alisema; “Saadani tunashughulika na utalii wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na utalii wa kutembea kwa miguu, utalii wa kuangalia wanyama mchana na usiku kwa wanyama kama bundi, chui na wengineo ambao macho yao yanaona zaidi usiku, utalii wa kwenye maji kwenye mto Wami ambao pia una eneo la makutano na Bahari ya Hindi lakini maji yake kamwe hayachanganyiki kupoteza uasili wake.

“Hifadhi hii ina utalii wa aina nyingi, pia tunasimamia kituo cha malikale chenye kumbukumbu ya biashara ya utumwa cha Caravan Serai cha mjini Bagamoyo, magofu yaliyotumika kuhifadhi watumwa, mbuyu uliotumika kunyongea watumwa maarufu mbuyu kinyonga, makaburi ya wamisionari waliokuja kueneza dini katika eneo hili la Pwani.

“Aidha tunao utalii wa dini, tuna eneo la mti wa Mbuyu ambao una nembo ya sanamu ya Bikra Maria, huenda ni kumbukizi, ni asili ambayo hakuna aliyeichora bali imekutwa hapo, huu ndiyo upekee wa Saadani” alisema Gordon.

Kaimu huyo ambaye pia ni Ofisa Mhifadhi anayesimamia kitengo cha utalii, alisema ili kuendelea kuimarisha hifadhi hiyo, wametenga maeneo tisa kwa ajili ya uwekezaji upande wa huduma za malazi, utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

Alieleza kuwa hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2005 kutoka kuwa pori la akiba ina malango makuu ya nchi kama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius (JNIA), Bandari Kuu, miji ya kihistoria ya Bagamyo na Zanzibar na kuifanya kufikika kwa urahisi kwa kutumia usafiri wa anga, majini na barabara.


IMG-20250627-WA0011.jpg

Mti wa mbuyu uliogunduliwa kuwa una mchoro wa sanamu ya Bikira Maria ambao umekuwa kivutio kipya katika Hifadhi ya Taifa Saadan eneo la Pangani mkoani Tanga.

Mmoja wa viongozi wa dini kutoka Kanisa la KKKT, Usharika wa Alei Levorosi Arusha Mjini Lucas Mollel alisema mambo mbalimbali aliyoyaona kwenye Hifadhi ya Saadani yamemuimarisha zaidi kiimani kwani ameshuhudia uumbaji wa Mungu usiokuwa wa kawaida.

“Tuna kila sababu ya kumshuru Mwenyezi Mungu, sijawahi kuona maji ya kusima kikucho karibu kabisa na bahari lakini hayana chumvi, haya ni maajabu, pia nimeona vifaa vilivyotumika kufunga watumwa. Niwaombe sana taasisi za dini na za Serikali kuwaleta viongozi wao kuja hapa kupumzisha akili na kujifunza mambo ya kale, kutafakari ukuu wa Mungu.”alisema Mollel.
 
Safi kabisa, ngoja nianze safari ya Saadani sasa kujionea vivutio
 
Back
Top Bottom