UPANDE wa mashitaka umekiri katika kesi inayowakabili mkurugenzi wa zamani wa Utawala na Utumishi Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Miradi wa benki hiyo, Deograthias Kweka kuwa hati ya mashtaka inayowakabili washitakiwa hao ina makosa.
Hayo yalifahamika jana mara baada ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema kutupilia mbali pingamizi lilotolewa na upande wa mashitaka na kuunga mkono maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi ya kutaka hati ya mashtaka ifutwe na washtakiwa waachiwe huru.
Pingamizi lililotupwa ni madai kuwa vifungu vya sheria vilivyotumiwa na upande wa utetezi kuwasilisha maombi yao mahakamani kutaka kesi hiyo ifutwe vina makosa.
Akitoa uamuzi huo Hakimu Lema alisema anakubaliana na maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa utetezi kuwa hati ya mashitaka inayowakabili wateja wao ina makosa.
Uamuzi huo ulifuata baada ya Jopo la Mawakili wa upande wa utetezi kuwasilisha maombi ya kutaka hati hiyo ya mashitaka ifutwe kabisa na wateja wao waachiwe huru kwa sababu ina makosa kisheria.
Mawakili hao wanataka wateja wao kwa kuwa uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa kuwashitaki wateja wao una dosari za kisheria, hivyo wanataka ifutwe kabisa.
Pia mawakili hao wanataka shitaka la tatu linalowakabili wateja wao la kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya Sh 221 bilioni liondolewe kwani halijawekwa wazi kwamba washitakiwa wamefanya kosa gani.
Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Wakili wa Serikali, Boniface Stanslaus alikiri kuwa hati yao ya mashitaka ina mapungufu na kuomba washitakiwa wasiachiwe huru kama hawana hatia, bali kwa sababu hati ya mashitaka yanayowakabili ina makosa.
Stanslaus alifafanua kuwa washitakiwa wangeweza kuachiwa huru kabisa iwapo mahakama ingekuwa imesikiliza ushahidi na kuthibitisha kama washitakiwa wana hatia au la lakini katika shauri hili halijafikia hatua hiyo.
Source: Mwananchi