Unyenyekevu na Kiburi

John Magongwe

Member
Jan 4, 2024
30
31
Unyenyekevu na Kiburi

Kiburi ni nini
Kulingana na Biblia kiburi ni hali ya mtu kujiinua kifikra, na kuamini kuwa hahitaji msaada wowote kutoka kwingine. Hali hii inaambatana na kudhihirisha tabia nyingine ndogo ndogo kama majivuno, matukano, au kuwadharau wengine, au kuwa na ujasiri kupitiliza na hata kukufuru.
Katika maandiko tunaambiwa kuhusu madhara ya kiburi. Mithali 16:18-19 inatuambia kwamba kiburi hutangulia uangamivu; na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi. Shetani alitupwa kutoka mbinguni kwa sababu ya kiburi (Isaya 14:12-15). Alikuwa na ujasiri na ubinafsi kwa jaribio la kuchukua nafasi ya Mungu mwenyewe kama mtawala halali wa ulimwengu. Lakini Shetani atatupwa jehanamu katika hukumu ya mwisho ya Mungu. Nami nitainuka, nishindane nao; asema Bwana wa majeshi; na katika Babeli nitang’oa jina mabaki, mwana na mjukuu; asema Bwana (Isaya 14:22).

Kwa nini kiburi ni dhambi hivyo
Kiburi ni kujitukuza wenyewe na kujinutukia sifa kwa ajili ya kitu ambacho Mungu ndiye amekamilisha. Kiburi ni kuchukua utukufu wa Mungu pekee na kuweka kwa wenyewe. Kiburi ni ibada nafsia. Kitu chochote sisi hukamilisha katika dunia hii hakingewezekana kama isingekuwa ni Mungu anatuwezesha na kututunza. "Maana ni nini anayekupambanua na mwingine? Nawe una usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea, wajisifia nini kana kwamba hukupokea?" (1Wakorintho 4: 7). Hiyo ndiyo sababu sisi humpa Mungu utukufu anaostahili peke yake.

Unyenyekevu ni Nini
Unyenyekevu unaweza kuelezwa kama ifuatavyo:
1. Hali ya mtu kujishusha licha ya hadhi, haki au kiwango alicho nacho.
2. Hali ya mtu kuonyesha heshima na kujali kwake watu wengine bila kujali ukubwa wala udogo wa kiwango chao cha maisha nk.
3. Hali ya kuudhibiti moyo wako usitawaliwe na kiburi, jeuri, majivuno wala dharau kwa mtu wa aina yeyote.
4. Hali ya kuinua kiwango cha thamani ya watu wengine na kuwaleta katika kiwango chako na kuwaona kuwa wao pia wana thamani kubwa kama wewe ulivyo.

Tunapaswa kuwa wanyenyekevu kwa sababu:
1. Hatujui kesho yetu. Yakobo 4:13-15 inasema: 13 Haya basi, ninyi msemao, leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; 14 walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka; 15 Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.
2. Kiburi kinaleta madhara makubwa na unyenyekevu unaleta baraka. Mithali 18:12 inasema "Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu."
3. Mungu huwapinga wasio na unyenyekevu na huwapa neema wanyenyekevu.
Yakobo 4:6 inasema: "Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu."
4. Hatujui sana kuhusu madhaifu yetu na tunahitaji watu wengine watusaidie kwa upendo. Zaburi 141:5 inasema: "Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; kichwa changu kisikatae, maana siachi kusali kati ya mabaya yao".
5. Bila ya unyenyekevu hatutauona ufalme wa mbinguni. Mathayo 18:3-4 inasema: 3 Akasema, Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. 4 Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.

Tukio fulani katika maisha ya Mfalme Daudi linaonyesha tofauti kati ya kiburi na unyenyekevu wa kweli.
Ilikuwa baada ya Daudi kushinda Yerusalemu na kulifanya kuwa jiji lake kuu. Daudi alimwona Yehova kuwa Mfalme halisi wa Israeli, hivyo akapanga kwamba Sanduku la Agano, lililowakilisha kuwapo kwa Mungu, lipelekwe jijini humo. Tukio hilo lilikuwa muhimu sana kwa Daudi hivi kwamba alionyesha shangwe yake waziwazi akifuata makuhani waliobeba Sanduku la Agano. Wakaaji wa Yerusalemu walimwona mfalme wao “akirukaruka” na “kucheza dansi kwa nguvu zake zote" (1Mambo ya Nyakati 15:15-16, 15:29; 2Samweli 6:11-16).

Hata hivyo, Mikali, mke wa Daudi hakujiunga na msafara huo wenye shangwe. Alitazama kutoka dirishani na badala ya kufurahia jinsi Daudi alivyomsifu Yehova, “akaanza kumdharau moyoni mwake” (2Samweli 6:16). Kwa nini Mikali alihisi hivyo? Inaonekana kwamba alijiona kuwa mtu wa maana sana kwa sababu ya kuwa binti wa Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli, na mke Daudi ambaye alikuwa mfalme wa pili wa Israeli. Huenda alihisi kwamba mume wake, mfalme, hakupaswa kujiunga na watu wa kawaida kusherehekea kwa njia ya kujishushia heshima. Majivuno yake yalionekana kwa jinsi alivyomsalimu Daudi aliporudi nyumbani. Alisema hivi kwa dhihaka: “Lo! Jinsi mfalme wa Israeli alivyojitukuza leo wakati alipojifunua leo mbele ya macho ya vijakazi wa watumishi wake, kama vile mmoja wa watu wapumbavu anavyojifunua!” (2Samweli 6:20).

Daudi alitendaje alipochambuliwa na Mikali? Daudi alimkemea Mikali kwa kumwambia kwamba Yehova alimkataa Sauli, baba yake, na badala yake akamchagua yeye. Daudi akaongeza hivi: “Nitajipuuza hata zaidi kuliko hivi, nitajishusha machoni pangu mwenyewe; nami nimeamua kujitukuza pamoja na wale vijakazi uliowataja” (2Samweli 6:21-22).

Daudi aliazimia kuendelea kumtumikia Yehova kwa unyenyekevu. Mtazamo huo unatusaidia kuelewa sababu iliyomfanya Yehova amwone Daudi kuwa “mtu anayekubalika kwa moyo wangu” (Matendo 13:22; 1Samweli 13:14).
Kwa hakika, Daudi alikuwa anafuata kielelezo bora zaidi cha unyenyekevu, yaani, unyenyekevu wa Yehova Mungu. Ingawa Yehova ndiye Mtu mkuu zaidi katika ulimwengu wote, andiko la Zaburi 113:6-7 linasema kwamba “anajishusha [yaani, anajiweka chini au kujiondoa katika cheo chake au ukuu wake anaposhughulika na mtu aliye chini yake] kutazama mbingu na dunia, akimwinua mtu wa hali ya chini kutoka kwenye mavumbi; humwinua maskini kutoka kwenye shimo la majivu”.

Kwa kuwa Yehova ni mnyenyekevu, anachukia macho ya majivuno ya watu wenye kiburi (Methali 6:16-17). Kwa sababu ya kuonyesha sifa hiyo mbaya na kutomheshimu yule ambaye Mungu alimchagua kuwa mfalme, Mikali alinyimwa pendeleo la kumzalia Daudi mwana, naye akafa bila kupata mtoto (2Samweli 6:23).

Hilo ni somo kwetu! Wote wanaotaka kupata kibali cha Mungu lazima watii maneno haya: “Jifungeni unyenyekevu wa akili kuelekeana ninyi wenyewe, kwa sababu Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwapa wanyenyekevu fadhili zisizostahiliwa” (1Petro 5:5).
 
Back
Top Bottom