Unamfundisha vipi mwanao kuwa muungwana?

MMASSY

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
290
193
Na Jerome Mmassy,Arusha

Ulishaona unampatia mtoto kitu anachokihitaji ama alichokuomba na asiseme asante?Ulishaona mtoto ama mtu mzima ana kukosea na haoni tatizo wala hajishugulishi kuomba msamaha?.Katika jamii tunamoishi hujawahi kuona mtu anakukosea na ukimweleza anakwambia basi yaishe?

Wengine wakikosea badala ya kuomba msamaha wanakuambia “basi kama nimekukosea nisamehe” hapa neno kama linaonyesha waziwazi kuwa mhusika hayuko tayari kuomba msahama bali kalazimishwa na hali Fulani.Wapo wengine hata ufanye vizuri namna gani kusema, ‘hongera umefanya vizuri’ wanaona kama adhabu na kujishushia hadhi.

Hizi ni baadhi ya tabia zinazoweza kuonyesha namna mtu asivyo muungwana na zinaweza kumpunguzia thamani yake mbele ya jamii.

Uungwana ni namna mtu anavyoweza kujali hisia za wengine. Kuelewa mwenzako anataka nini, anajisikiaje unaposema maneno fulani, anachukuliaje unapomfanyia mambo fulani na mengineyo kama hayo. Kuna msemo uliozoeleka kuwa tabia za watoto ni sura ya walivyo wazazi wao. Tafsiri ya msemo huu ni kuwa kile anachokifanya mtu, kwa kiasi kikubwa, kinatokana na yale anayojifunza kwa wazazi wake. Ndio kusema uungwana anaojifunza mwanao unakutegemea namna wewe mzazi unavyojiweka mbele yao, kwa maneno, kwa matendo na hata kwa tabia.Mzazi tambua kuwa,ukiwa unapewa chakula na mzazi mwenzako haushukuru,ikiwa mkikosana nyumbani hauombi msamaha,tegemea mwanao atakuwa kama wewe kuanzia utotoni hadi atakapokuwa mtu mzima.Ile methali ya Kiswahili isemayo mtoto umleavyo ndivyo akuwavyo ina maana hii inayozungumziwa katika Makala hii. Tutazame sasa mambo muhimu unayoweza kuyawekea mkazo unapomfundisha mwanao uungwana.

Kushukuru

Kushukuru ni kitendo cha kurudisha fadhila unazotendewa na wengine. Unapopewa huduma nzuri dukani, kwa mfano, ni uungwana kushukuru hata kama ni kweli umeilipia huduma hiyo. Tabia ya kushukuru ni matokeo ya mafunzo tuliyopitia maishani mwetu, hatuzaliwi nayo.

Ikiwa unataka mwanao awe mtu mwenye uwezo wa kutambua mema anayotendewa na wengine, ni muhimu uitilie mkazo tabia hata ikibidi kwa kuweka mazingira ya kulazimisha ilimradi tu mwanao ajifunze kuwa mtu wa kusukuru pale anapopatiwa kitu. Mfano, jenga utaratibu wa kudumu unaomlazimisha kila aliyeshiriki chakula hapo nyumbani kusema, ‘asante’.

Utamaduni huu wa kushukuru unawezekana ikiwa wewe mwenyewe utaanza kuonesha mfano. Mshukuru mwezi wako mbele ya watoto wako. Washukuru watoto wako wanapokutendea kile unachokipenda. Kadhalika, wakumbushe kushukuru kila wakati.Kupitia kitendo hiki utakuwa unawajenga wanao kuwa waungwana katika Maisha yao yote n ahata ukipata wageni nyumbai watajonea namna gani watoto wako waliyo na maadili mazuri.

Kupongeza

Jiwekee utaratibu wa kuwapongeza wanao wakifanya jambo zuri,mpongeze mwenzi wako akifanya jambo jema mbele ya watoto wako.Mtu mwingine anapofanya jambo zuri ni uungwana kumpongeza. Pongezi humfanya anayepongezwa kujisikia vizuri. Mfundishe mtoto kutambua mazuri yanayofanywa na wengine na kutamka maneno sahihi.

Kuwa mfano kwa kutoa pongezi. Tafuta kutambua jitihada zinazooneshwa na wanafamilia na toa pongezi kwa moyo wa dhati. Kwa mfano, wapongeze watoto kwa jitihada wanazoonesha katika masomo yao hata kama hawajafaulu kwa kiwango cha juu. Mpongeze mke/mume wako anapofanya vizuri mbele ya watoto na bila aibu. Wahimize wanao kupongezana ili kujenga tabia ya kupongeza wengine.Ikiwezekana kuwa na tabia ya kuwanunulia zawadi wanao wanapofanya vizuri katika masomo yao.Ikiwa ni familia yenye utaratibu wa kusali Pamoja kifamilia basi teua mtoto mmoja aongoze sala na akiweza mpongeze mbele ya wenzao.

Kupitia kitendo hiki unamwandaa mwanao kuwa ni mtu wa kutambua juhudinza wengine maishani n ahata atakapokuwa mtu mzima atasifiwa na jamii na awapo kiongozi atakuwa ni mtu wa kutambua juhudi za wafanyakazi wake katika kufikia malengo ya taasisi anayoiongoza.

Kuomba msamaha

Wafundishe wanao kutambua ya kuwa, kukosea ni sehemu ya mapungufu yetu kama binadamu na hii inatokana na mantiki ya kidini kuwa hakuna alaiyekamilika yu ngali mwanadaamu. Lakini si kila mtu anaweza kuwa tayari kuomba msamaha hata pale anapojua amekosea.Utafiti unaonyesha kuwa wanaume ni wagumu zaidi kuomba msamaha pale wanapokosea. Wanafikiri kuomba msamaha ni kujishushia hadhi zao. Ikiwa unataka mwanao awe na tabia ya kuomba msamaha na kuwasamehe wanaomkosea unawajibika kumfundisha kuomba msamaha lakini zaidi kumfundisha maana ya msamaha na faida zake.

Kama mzazi, onyesha mfano wewe mwenyewe kwa kuomba msamaha mbele ya wanao. Mwombe msamaha mke/mume wako hata kwa mambo madogo unayomkosea. Waombe msamaha wanao unapogundua umefanya kosa.Kwenye Makala moja niliandika kuwa,kizazi cha sasa kinahitaji mbinu za malezi tofali na mbinu zilizotumika miaka ya nyuma kwa sababu ya muda tunaoishi,utengamano wa kijamii uliopo sasa na muingiliano na tamaduni nyingi zaidi kwa sababu ya utandawazi.Hivyo lazima tuwe na mbinu za kisayansi za malezi kuliko matumizi ya nguvu yanayozalisha watoto jeuri. Pale wanao wanapokuwa na makosa, walazimishe na wao kuombana msamaha na uwasamehe hapo watakuwa wamejifunza kuwa waungwana. Ukweli ni kwamba mtoto anapokuwa na tabia ya kuomba msamaha, ni rahisi kusamehe wengine pale anapokosewa.

Kuwajali wengine

Kwa bahati mbaya,wapo watoto ambao kutokana na malezi waliyolelewa wanajiona bora kuliko wengine.Watoto wanaotokea familia zenye uwezo wanawaona wengine kama vile wana hadhi ya chini kuliko wao.Watoto wanaosoma shulle za binafsi wanajiona bora kuliko wale wanaosoma shule za serikali na huko huko kwenye shule za binafsi wanaoenda shule kwa magari ya shule wanajiona bora kuliko wale wanaotembea kwa miguu au wanaopanda daladala.

Kuthamini wengine ni kitendo cha kiungwana sana na kwa maana rahisi ni kujiona kuwa huwezi kuwa bora kuliko watu wengine. Hiyo haina maana kuwa hujiamini. Hapana. Kimsingi unapojiamini ni rahisi sana kuwathamini wengine. Unao wajibu wa kumfundisha mwanao tabia ya kuwathamini watu wengine. Inawezekana, anza kwa kuwaonesha watoto wako vile unavyowathamini. Wanapoumia, onesha kujali na wape pole bila kuchelewa. Watakapojua unawajali, hawatapata tabu kuwajali wengine. Wakumbushe wajibu wao wa kutoa pole kwa wenye shida na wanaoumia. Waonyeshe kuwa watu wote duniani ni sawa,usiwaonyeshe kamwe kuwa watoto wa jirasni ama ndugu wanastahili kutothaminiwa kutokana na hali zao.Kwa kufanya hivyo utajenga mazoea mazuri ya kuwajali wengine na watoto wako watakuwa wakiwa na tabia njema na wakiwa waungwana hata wajapo shika nafasi za uongozi watakuwa ni viongozi wanaowajali wale wanaowaongoza.

Kuvaa mavazi yenye staha

Utakubaliana nami kuwa moja ya vitu vinavyomtambulisha mapema mtu ni muonekano wake kabla hajaanza kuzungumza.Jitahhidi sana kumfundisha mwanao kuvaa mavazi ya adabu na yanayokubalika na jamii.Mwanao ataanza kujifunza kwako unavyovyaa na unavyokaa na wengine katika jamii.Baadhi yetu tunavaa mavazi ambayo ukikaa tu watoto wako wanaona hadi sehemu nyeti,mengine ni yale ya fasheni ambayo yamechanwa chanwa na yanaonesha maungo yetu.Hii si tabia ya kiungwana.Tambua kuwa,ukifundisha wanao kuwa huo ndio utaratibu wa mavazi nao wataiga na watakuwa na hiyo tabia.Hakuna atakayekuja kuwaambia kuwa kuvaa vibaya sio uungwana wakamwelewa.

Niliwahi kufundisha shule moja na nikawa mwalimu wa mavazi.Mwanafunzi mmoja alikuwa hataki kabisa kuvaa sare ya shule inavyopaswa na kila akipewa sare ya shule lazima airekebishe anavyotaka yeye,siku moja akaniuliza,kuna uhusiano gani kati ya kuvaa mavazi ya heshima na kufaulu masomo?baada ya kumdadishi sana nikagundua anatokea kwenye familia ambayo baba,mama,dada na kaka zake wanavaa mavazi ya hovyo sana.Mtoto huyu alikuwa hapendwi kabisa na wenzake kutokana na tabia za kujiona pia bora kuliko wengine,uchono n.k.Hivyo tunajionea namna jamii inayolea watoto vibaya.Jitahidi sana kumlea mwanao vizuri ili siku moja ukiwa haupo duniani mwanao aweze kuishi na kila mtu.


mmassyfm@rocketmail.com
 
Mtoto anaelewa zaidi lugha ya matendo anayoiona kuliko lugha ya maneno anayoisikia.

Mtoto anajua maana ya maneno kwa kutegemea vitendo ambavyo vinafanyika wakati maneno hayo yakizungumzwa.

Kama kila siku ukiwa unakula ukawa unamuambia mwwnao "karibu tulime" mtoto atakua akimuona mtu anakula atajua hapo analima.

Kufanya mambo ambayo ungetamani mwanao awe ndio msingi bora wa kumkuza mtoto kwa sababu atakuwa anaichukua picha ya matendo yako na kuiweka akilini na baadae ataanza kuitumia kama mfumo wake wa maisha.

Ndio maana leo watoto wanaharibika kwa sababu baba yupo kazini na mama yupo kazini,toto linalelewa na housegirl ndani.

Hakuna taarifa anazoingiza ubongoni mwake,akikua huyu kuna mambo atashindwa kuyasolve vizuri na jamii inayomzunguka
 
Back
Top Bottom