lwaitama awshauri viongozi wa chadema wajibu tuhuma zifuatazo
MKAKATI WA MABADILIKO 2013
hususan kwa kuangalia maeneo nyeti yaliyowekwa alama nyekundu
Ni dhahiri kwamba uongozi uliopo umeishiwa mbinu na kuakisi jambo la msingi sana ambalo waasisi wetu waliliona tangu mwanzo na kuamua kuweka kipengele cha ukomo wa uongozi kwenye mwongozo wetu.Kuchoka kwa uongozi wetu kunaonekana dhahiri katika mipango na mikakati ya taasisi ya miaka kadhaa. Mfano mwaka 2008 uongozi ulianzisha mkakati wa operesheni samaki mkubwa (maarufu kama Oparesheni Sangara). Huo ulifanyiwa kazi katika mikoa kadhaa na hatimaye ikafa kimya kimya. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kulianzishwa matembezi ya maandamano ambayo nayo yalikuwa yakipeleka ujumbe kwa watu na yalipangwa kufanyika mikoa yote na wilaya zote.
Kumbukumbu zetu zinaonyesha kwamba yalikuwa yakianzia makao makuu ya mkoa na kwenda kwenye wilaya zote. Lakini kumbukumbu hizo zinaonyesha kwamba yalifanyika Mwanza, Musoma, Shinyanga, Kagera na mikoa ya Nyanda za Juu kusini (Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa) kisha nayo yakafa kifo cha mende. Kisha mwaka 2012 ikaanzishwa operation ya mabadiliko maarufu kama Movement for Change (M4C). Hiyo ilikuwa inakwenda kwenye mikoa na timu kama nne hivi ambazo kwa ujumla zilitathmini hali ya mtandao na uongozi wa taasisi, kuhamasisha umma kwa njia ya mikutano ya hadhara, kuingiza wanachama na kusimika uongozi na hatimaye kufanya mafunzo kwa viongozi. Hiyo ikafanyika Mtwara na Lindi, Morogoro na kisha ikaenda kufia Iringa. Mwaka huu viongozi wetu wamekuja na ugatuaji madaraka kutoka makao makuu ya taasisi na kupeleka madaraka kwenye kanda mbalimbali. Mkakati huu ulikufa kabla ya kuanza pale viongozi wakuu walipobadilisha maazimio ya kikao kikuu na kutekeleza matakwa yao ikiwa ni pamoja na kuleta suala la viongozi wa muda kwa muda mrefu badala ya kuajiri maofisa na wakahakikisha wanaweka watu wao kwenye uongozi wa muda. Kitendo hiki kwa peke yake, cha kufeli kwa kila mkakati unaoletwa na viongozi wetu katika hatua za utekelezaji unaofanywa na wao wenyewe waleta mkakati, ni kiashiria tosha kwamba uongozi uliopo umechoka.
Performance yetu kwenye chaguzi ndogo nayo ni ishara kwamba mabadiliko yanahitajika. Tangu uongozi huu uingie madarakani, kumefanyika chaguzi ndogo 8 za wawakilishi kwenye chombo kikuu, kati ya hizo tumeshinda 2 tu sawa na asilimia 25. Aidha baada ya mwaka 2010 kumefanyika chaguzi kadhaa za wawakilishi kwenye halmashauri. Mwezi Oktoba 2011, mwezi wa4 2012, mwezi Septemba 2012 na mwezi Juni 2013. Kote performance yetu imekuwa poor kupindukia. Mfano mwezi wa Juni 2013 tumepata viti 6 kati ya 22 (27%) na mwezi Septemba 2012 tulipata viti 7 kati ya 29 (24%). Ni dhahiri mabadiliko yanahitajika kwa kuwa wakuu waliopo wanatumia mbinu zile zile na kupata matokeo yale yale. Tunahitaji mbinu mpya. Kwa kifupi, ushindi ambao tumekuwa tukiupata katika chaguzi ndogo haulingani na ukubwa wa hamasa kwa taasisi yetu iliyopo mitaani. Hii ni kwa sababu tumekuwa tukitumia mbinu hizohizo katika kila chaguzi. Aidha, tu wepesi mno wa kuridhika na kujisifu kwa mafanikio madogo badala ya kukaa chini na kutafakari kwa kina mahala tunapojikwaa.
Matumizi ya fedha za taasisi.
Hakuna mtu anayejua hivi sasa fedha za chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu yaani mkuu kabisa, mtendaji mkuu na mkuu wa fedha kwenye taasisi yetu. Maamuzi ya vikao hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi wa 2010 vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa bali zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Lakini leo si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha. Watu watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje. Mfano mwingine ni maamuzi ya kikao cha juu mno cha hivi karibuni kilichoamua kwamba kiasi cha fedha inayotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa na wilaya na kiasi kingine kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa tano maamuzi hayo hayajatekelezwa. Lakini kuna michango ya watu binafsi kama yule mtanzania mwenye asili ya kihindi, hizo nazo hazijulikani zimechukuliwa lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje. Hapo hatujataja fedha zinazopatikana kutoka kwenye fundraising events mbalimbali kama ile ya Dar es salaam na Mwanza. Hizo nazo hazijawahi kuonekana na walioendesha hizo fundraising, uaminifu wao kwenye masuala ya fedha ni questionable.
Taarifa za fedha.
Tokea baada ya uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna kikao chochote kilichowahi kupokea na kujadili hadi mwisho ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za taasisi. Kila kikao agenda hiyo inarushwa kiaina. Wanaojua mchezo huo ni watu watatu tu tuliowataja hapo juu na malengo ya kurusha hiyo agenda kila wakati na kukwepesha isijadiliwe pia wanayajua wao. Ni dhahiri tukiendelea na hawa watu tutafika 2015 tukiwa hatuna pesa hata ya kuweka mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa tumesimama. Kwa kiasi kikubwa mkuu aliyepo anatengeneza mazingira yaleyale ya mwaka 2005 na 2010 ya kutaka chama kiwe hakina hela ili ikifika wakati wa uchaguzi kimpigie magoti. Kisha atatoa pesa bila kumbukumbu zozote na mara baada ya uchaguzi anapeleka lundo la deni na kudai alipwe hela aliyekikopesha chama wakati wa uchaguzi. Alifanya hivyo katika chaguzi za 2005 na 2010. Wakati wote wa kampeni za mwaka 2010, kwa mfano, taasisi yetu ilihangaika sana kwa kukosa hata hela ya kununua maji kwa wajumbe wa ngome. Lakini ajabu ni kwamba baada ya uchaguzi mkuu wa taasisi na baadhi wa wapambe wake walilete deni kubwa la takribani shililingi milioni mia tano akiadi kuwa walikikopesha chama. Taasisi imewalipa pesa zote hizi kwa muda mwaka mmoja. Sasa anatengeneza mazingira hayohayo kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Mipango ya kukipatia chama mapato ya ziada kutoka nje ya chama. Wakuu waliopo hawana hata ndoto ya namna ya kupata fedha za ziada. Wanachokijua ni kukusanya sadaka kwenye mikutano ya hadhara na kuwapatia kazi watu wanaoonekana kuwa matapeli eti waendeshe harambee za kuchangisha fedha kwa njia ya matukio. Mawazo mazuri kama lile la kuanzisha kampuni la uwekezaji la taasisi yetu litakalowekeza kwenye miradi mbalimbali, halijawahi kufanyiwa kazi, na hivyo uanzishaji wa miradi mbalimbali ya kuiingizia taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana. Hatuwezi kufika hata siku moja bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa hapa jirani juzi juzi wakuu wetu ingawa walishiriki lakini hawaonekani kama wamejifunza chochote.
Njia haramu za kubaki madarakani.
Ili kuhakikisha wakuu wanabaki madarakani, wameanzisha vikundi vikundi ndani ya taasisi yetu. Siku hizi ni rahisi sana kuambiwa kwenye taasisi yetu eti huyu ni wa boss ( muda eight, lissu lema msigwa) na huyu ni wa dogo. Na wale walio wa boss kwa kuwa boss ndo anashikilia raslimali za taasisi anatumia mfumo haramu kuwaneemesha watu wake kwa kutumia raslimali za taasisi na kuwakandamiza wote wanaoonekana wanapishana naye kimtazamo. Jambo hili limewaibua wachumia tumbo, wapenda madaraka, na vibaraka lukuki wanaokwenda kujipendekeza kwa wakuu wa taasisi kwa malengo ya kujinufaisha binafsi. Katika kufanya hivyo vibaraka hao wamekuwa wakiwaendea wakuu wa taasisi na kuwajaza maneno mabaya dhidi ya viongozi wenzao na kuzidi kuwafarakanisha viongozi wa juu.
Kuna mchezo umeanzishwa na wakuu wa taasisi unaitwa ulinzi wa chama uliogawanyika katika makundi mawili yaani visible na invisible. Visible ni ule unaoonekana ambao uko chini ya kikosi chetu chekundu ambacho kinajulikana kwa kila mtu lakini invisible wanajulikana kwa mkuu wa taasisi na mtendaji mkuu peke yake. Wanafanya kazi kwa maelekezo ya wakubwa hao wawili na hawajulikani kwa viongozi wengine wa juu. Ni hawa hawa ambao wanatumika vibaya pale wanapoleta taarifa za kiintelijensia ambazo zinawahusisha viongozi wasiopendwa na wakuu na usaliti dhidi ya taasisi. Hakuna kamati maalum inayowathibitisha maaintelijensia hao bali wakuu wenyewe wanawachukua wanaowataka. Ni katika mfumo huu wa kipuuzi mida eight amekuwa akitumika vibaya kwa kumshambulia mtendaji mkuu msaidizi hadharani kwa kutumia mitandao ya kijamii na wakuu wanafurahia na kumlipa pesa.
Udhaifu wa utendaji wa mtendaji mkuu.
Mtendaji mkuu ni dhaifu mno na ni mara nyingi sana tumeshuhudia mkuu wa taasisi akifanya mambo ya kiutendaji kinyume na utaratibu kama vile yeye mwenyewe kuja kwenye kamati ya makatibu na wakurugenzi na kupangua mipango yao na ku-inject ya kwake na mtendaji mkuu kuadopt tu kana kwamba yeye hawezi kupanga mambo ya kiutendaji, hata tunapokuwa kwenye operesheni maalum tumeshuhudia mkuu wa taasisi ndo akipanga watendaji, posho zao na hata kusimamia matumizi ya pesa na shughuli mbalimbali za kiutendaji. Udhaifu wa mtendaji mkuu ni udhaifu wa mkuu wa taasisi kwa kuwa amemteua yeye mara mbili tena mara ya pili alileta jina moja mbele ya Baraza la juu kuonyesha kwamba aliridhika na utendaji wake kiasi cha kutotaka kumpambanisha na mwingine. Lakini baada ya kumpendekeza mara ya pili ndipo tumeshuhudia yeye kuingilia kati mara nyingi sana mambo ya kiutendaji kana kwamba anamfichia aibu mtendaji wake. Swali kwa nini alimteua tena? Jibu lake litakuwa rahisi tu kwamba ni kwa sababu mtendaji huyu ni passivekwa kila takwa la mkuu wake.
Matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi.
Taasisi yetu inayo kamati ya tenda ambayo iko chini ya kamati ya makatibu na wakurugenzi. Lakini uzoefu unaonyesha kwamba kamati hii haifanyi kazi imezimwa kimya kimya na wajumbe wote wa kamati ya tenda kwa kuwa ni wachumia tumbo wanaojigonga kwa wakuu, wamekubali kuzimwa. Leo ikidaiwa kamati hiyo ilete nyaraka za mchakato wa manunuzi ya magari, pikipiki, vifaa vya kueneza taasisi, set ya televisheni iliyofungwa ofisini kwa mtendaji mkuu, hawana. Manunuzi haya yote yote yanafanywa na wakuu hasa hasa mkuu wa taasisi bila utaratibu wowote jambo ambalo ni hatari na linarahisisha matendo ya kifisadi. Bila aibu, mkuu wa taasisi ndio amekuwa mnunuzi wa vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na ambaye haihojiwi popote. Huu ni mfano wa wazi wa mgongano wa kimaslahi jambo ambalo ni hatari kwa kiongozi mkubwa wa taasisi kama yetu inayojitambulisha katika kupinga vitendo vya ufisadi na uvunjifu wa maadili ya uongozi kwa ujumla.
Makubaliano ya kifisadi na mtu binafsi anayeuza vifaa vya kueneza taasisi.
Hakuna kikao chochote cha juu kilichojadili ama kilichowahi hata kupewa taarifa tu kwamba sasa kuna mtu binafsi kapewa tenda ya kuuza vifaa vya taasisi na taasisi inanufaika vipi na mauzo hayo na kwa nini vifaa muhimu vya taasisi vinauzwa. Jambo hili linajulikana kwa wakuu tu.
Mifumo ya uteuzi wa maofisa wa makao makuu ya taasisi imevurugwa na siku hizi wakuu wa taasisi hasa mtendaji mkuu anateua na kutimua ofisa anavyotaka na mara nyingi bila hata kamati ya makatibu na wakurugenzi kujua. Mambo haya yanafanyika mbele ya macho na masikio ya mkuu wa taasisi jambo ambalo linazidi kuthibitisha kwamba mkuu na mtendaji mkuu wanajuana na wanafanya kwa kulindana.