Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,713
SERIKALI imeazimia kuwapatia wananchi wake umeme wa uhakika na wa bei nafuu ifikapo mwakani baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme na gesi uliopo Kinyerezi,jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza matumizi ya mitambo ya kukodi inayogharimu Serikali kiasi kikubwa cha fedha.
Alisema kuwa mitambo ya kukodi iliyopo nchini ilikuwa inazalisha zaidi ya megawati 300 na hadi sasa tayari wamesharudisha mtambo mmoja iliokuwa unazalisha megawati 105. 55 zilikuwa zinatumika Arusha na 50 zilikuwa zinatumika Dodoma na kwamba hadi kufikia Novemba wanataka wawe wamerudisha mitambo yote.
"Tuna uhakika na hiki tunachokifanya kwani mtambo wetu wa Ubungo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 105 hauna gesi, mtambo wa Ubungo mmoja unazalisha megawati 68 badala 100 huku ule wa Symbion ukitumia mafuta ya ndege, hivyo kuanza kwa matumizi ya gesi kutafanya tuwe na umeme wa uhakika", alisema Maswi.
Alisema ifikapo mwakani Serikali itaokoa zaidi ya sh. trilioni 1.6 zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa kituo cha kuzalishia umeme cha Kinyerezi, Mhandisi Simon Jilima, alisema kuwa wanaendelea na awamu ya pili ya ujenzi na wameshakamilisha majengo ya utawala pamoja na majengo ya kuendeshea mitambo.
Alisema, kwa sasa wameanza ujenzi wa laini ya kilovote 220 iliyo na kilomita 8 na kilovote 132 upande wa viwanda iliyo na kilomita tatu.
"Mtambo huu utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 150 zitakazounganishwa katika gridi ya Taifa na kwa upande wa Kimara wataunga katika mtambo unaotoka Morogoro huku kilovote 132 zikinufaisha upande wa viwanda pamoja na wakazi wa Mbagala na Gongo la Mboto", alisema Mhandisi Jilima.
Alisema, mradi huu ni wa Serikali kupitia TANESCO na unagharimu dola milioni 183 sawa na sh. bilioni 240 na hadi sasa Serikali imeshatoa dola milioni 139.5 sawa na sh. bilioni 180.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa upande wa Afrika Mashariki, Philippe Dongier, alisema mradi huo unaridhisha kwani ujenzi wake unaendelea vizuri.
Alisema, Serikali inatakiwa kufungua milango zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje ili kuwekeza sehemu mbalimbali za maendeleo na wigo mpana wa ajira kwa Watanzania.
"Serikali pekee haiwezi kuwapatia ajira vijana wote, hivyo kufungua milango kwa kupitia wawekezaji kutatengeneza wigo mpana wa ajira na kupunguza tatizo la ajira linalokabili nchi nyingi duniani," alisema Dongier.
CHANZO: Majira