UMAFIA: Tanzania kama Mexico mafisadi wana nguvu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

UMAFIA: Tanzania kama Mexico mafisadi wana nguvu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Halisi, Jun 17, 2010.

 1. Halisi

  Halisi JF-Expert Member

  #1
  Jun 17, 2010
  Joined: Jan 16, 2007
  Messages: 2,810
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  TAFAKURI JADIDI

  Tanzania na Mexico: Simulizi ya nchi mbili!


  Johnson Mbwambo
  Juni 16, 2010

  YAWEZEKANA kichwa hicho cha leo cha makala yangu kimekuchanganya, lakini nimeona nimuige kidogo mwandishi maarufu wa vitabu wa Uingereza, Charles Dickens. Nina hakika baadhi ya wasomaji wangu wamesoma kitabu chake kinachoitwa A Tale of Two Cities (simulizi ya miji miwili).

  Kitabu hicho cha riwaya, ambacho mauzo yake kote duniani ni zaidi ya nakala milioni 200, kimekita katika miji miwili ya Paris na London, na kinazungumzia maisha kabla na wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 - 1799.

  Kwa kufuata nyayo hizo za Dickens, nimeshawishika leo kukita safu yangu katika simulizi ya nchi mbili – Tanzania na Mexico (tales of two countries?!) ambazo kila moja inapigana vita ya aina yake, lakini inayofanana kwa namna moja au nyingine.

  Labda tuanze na Mexico. Kwa karibu miongo mitatu sasa nchi hiyo imekuwa ikipigana vita ya kukomesha biashara ya madawa ya kulevya; lakini badala ya kupungua, biashara hiyo imekuwa ikishamiri mwaka hadi mwaka.

  Kila rais mpya aliyeingia madarakani Mexico aliapa kupambana na biashara hiyo na kuitokomeza, lakini hakuna aliyefanikiwa. Hata Rais wa sasa, Felipe Calderon, licha ya kusaidiwa mno na Marekani, yaelekea vita hiyo inamshinda.

  Jambo muhimu kwa wasomaji wangu kufahamu ni kwamba biashara hiyo ilianza kidogo kidogo. Na ingawa umma ulipiga kelele ukisaidiwa na vyombo vya habari, lakini watawala waliziba masikio.

  Kidogo kidogo mashamba ya kulima mimea inayotengeneza madawa hayo ya kulevya, yakaongezeka vijijini. Ikafikia hatua kikaanzishwa kikundi cha kiharamia cha kusimamia biashara hiyo haramu; lakini bado watawala waliendelea na upofu na ukiziwa wao.

  Na kwa sababu ya ukiziwa na upofu wao, sasa biashara hiyo Mexico imekuwa zimwi kubwa ambalo halikamatiki. Kutoka katika kuwa na kikundi kimoja tu cha kiharamia kinachosimamia biashara hiyo, sasa Mexico ina vikundi (cartels) vikubwa visivyopungua sita.

  Baadhi ya vikundi hivyo vya kiharamia, kama kile kinachoitwa Sinaloa Cartel, kinachoongozwa na Joaquim “El Chapo” Guzman, kimefikia hata hatua ya kuwa na jeshi lake kwa ajili ya kupambana na vikundi vingine kugombea maeneo na ruti za biashara hiyo, na pia kwa ajili ya kupambana na polisi au vikosi vya serikali.

  Watawala wa Mexico walipozinduka na kuanza kupambana na biashara hiyo, wakakuta zimwi limeshakuwa kubwa. Hivi sasa, si tu kwamba vikundi hivyo vina majeshi yake, lakini pia vina mtandao mkubwa kiasi kwamba vimechomeka ‘watu wao’ ndani ya serikali – kuanzia kwenye polisi na majaji hadi kwenye wanasiasa na watawala serikalini.

  Lakini si hivyo tu; kwani kina Joaqiun “El Chapo” walianza kuyatumia mabilioni ya mapesa wanayoyavuna katika biashara hiyo, kuwaletea wananchi maendeleo!

  Pale ambako hapakuwa na barabara, kina “El Chapo” wanajenga. Pale ambako hapakuwa na shule au hospitali, kina “El Chapo” pia wanajenga nk. Kwa maneno mengine, pesa chafu inayotokana na madawa ya kulevya inatumiwa kuwarubuni wananchi kwa kuwajengea vitu hivyo vya maendeleo.

  Na kwa kuwa pia hutoa pesa nyingi kwa wanavijiji wanaolima mimea inayotengeneza madawa hayo, kina “El Chapo” wametokea kupendwa mno katika baadhi ya maeneo ya Mexico kuliko wanavyopendwa viongozi wa serikali! Naambiwa hali ni hiyo hiyo huko Colombia.

  Ni katika mazingira hayo ambapo Rais Felipe Calderon anaelekea kuishindwa vita hiyo; licha ya kusaidiwa na Marekani. Ingawa Calderon alihakikisha sheria kali zinapitishwa na bunge kupambana na biashara hiyo, hakuna mafanikio makubwa aliyoyapata katika vita hiyo.

  Ingawa pia alianzisha vikosi maalumu kupambana na biashara hiyo na kuviimarisha, bado vita dhidi ya kina “El Chapo” inamuwia ngumu.

  Na ingawa pia amepokea mabilioni ya pesa za misaada kutoka Marekani kupambana na biashara hiyo, na hata kuchangia na nchi hiyo taarifa za ujasusi, lakini bado biashara hiyo inazidi kushamiri mwaka hadi mwaka.

  Ni kwa nini vita hiyo inaelekea kumshinda Calderon licha ya hatua zote hizo alizochukua? Sababu ni nyingi, lakini kubwa ni kwamba Calderon amejikuta amezungukwa na mtandao mkubwa wa wafuasi wa cartels hizo ambao hutumia rushwa, na hata baadhi ya maafisa wake mwenyewe wako kwenye orodha ya wanaolipwa kila mwezi na kina “El Chapo”!

  Isitoshe, Calderon ameshindwa kuwashawishi wananchi wa maeneo ambako vikundi hivyo vinatamba, kufanya uasi dhidi ya vikundi hivyo. Wananchi wamegoma kuasi dhidi ya vikundi hivyo kwa sababu wanawaona kina “El Chapo” kama miungu yao kwa vile wanawaletea maendeleo pale ambako serikali ilishindwa!

  Ndugu zangu; hiyo ni Mexico, na labda sasa tuigeukie Tanzania yetu (kumbuka mada ni A tale of two countries – simulizi ya nchi mbili!). Wakati ambapo vita ambayo Mexico inapigana nayo ni dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya, hapa Tanzania vita ambayo tunapigana nayo ni dhidi ya ufisaadi; ingawa humo ndani imo pia biashara hiyo!

  Kwa karibu miongo miwili sasa Tanzania tumekuwa tukipigana vita ya ufisadi, lakini bila ya kupata mafanikio yoyote ya kujivunia. Kama Mexico, nasi tumebadilisha marais; lakini hakuna rais ambaye amefanikiwa kutokomeza vita hiyo ukimwondoa Nyerere.

  Kama Mexico; nasi tumeimarisha TAKUKURU yetu, lakini hakuna dalili za mafanikio. Kama Mexico; nasi tumefanya mabadiliko katika sheria zetu kadhaa na hata kutunga mpya (kama hii ya kudhibiti matumizi ya pesa wakati wa uchaguzi), lakini hakuna mafanikio ya wazi yanayoonekana.

  Isitoshe, sasa tumefikia hatua mbaya kabisa ambapo fedha chafu za mafisadi zinatumika kutuchagulia viongozi wa kututawala (rejea skandali ya Kagoda Agriculture).

  Ni kwa nini vita hii inaelekea kutushinda Watanzania? Jibu ni kama lile lile la Mexico; nalo ni kwamba tumechelewa kujitosa katika uwanja wa mapambano, na tulipoamua kufanya hivyo tukakuta mtandao wa ufisadi umeshakuwa mkubwa mno na unaogusa kila sekta.

  Kama Mexico, watawala wetu waliziba masikio na kujitia upofu dhidi ya kelele za wananchi na za vyombo vya habari kuhusu kushamiri kwa ufisadi huo nchini, na sasa wanapozinduka wanajikuta wamezungukwa na mafisadi kila kona!

  Kama Mexico, mtandao wa ufisadi katika Tanzania nao umefanikiwa kupenyeza katika ajira mapolisi wao, mahakimu wao, majaji wao, wabunge wao, mawaziri wao, madiwani wao, madaktari wao, watu wao katika vyama vya siasa, watu wao katika mabenki (ikiwemo BOT), watu wao kwenye bureau de change, na hata waandishi wao wa habari nk!

  Kama Mexico, mtandao wa mafisadi katika Tanzania nao umeachiwa utumie pesa chafu zilizovunwa kwa njia za kifisadi (kama vile EPA na ten percent za mikataba) kuwaletea wananchi ‘maendeleo’ katika majimbo ya wabunge wao.

  Ni jambo la kawaida kabisa hivi sasa katika Tanzania kusikia mwanasiasa (mbunge, waziri au mfanyabiashara) akijenga jimboni kwake visima kadhaa, sekondari kadhaa, zahanati kadhaa na hata kukarabati barabara, lakini ilimradi yupo chama tawala CCM, hakuna asasi inayoweza kumhoji alipata wapi mapesa yote hayo.

  Na kama serikali inataka uadui na wananchi wa majimbo hayo yaliyojengewa vitu hivyo na ‘mbunge wao mfanyabiashara’, basi, ionyeshe tu hisia za kutaka kumhoji aliyapata wapi mapesa hayo! Itatishwa kwamba jimbo litakwenda kwa wapinzani; hata kama kitisho hicho ni upuuzi mtupu!

  Kama ilivyo Mexico, mafisadi katika Tanzania nao wanaonekana kama miungu watu kwa wanavijiji majimboni kwa kuwa tu wamewajengea visima, shule na zahanati kwa pesa chafu mahali ambako serikali ilishindwa kuwaletea maendeleo hayo!

  Na kama ilivyo Mexico, ni vigumu kwa wanavijiji wanaonufaika na visima, zahanati na shule hizo kufanya uasi wa kutowapigia kura za ubunge mafisadi hao waliowajengea vitu hivyo. Huwa wanajihoji; watamchinjaje kuku anayewatagia mayai ya dhahabu?

  Ndugu zangu, nimetumia mfano wa Mexico kujenga hoja ya kwa nini vita ya ufisadi katika Tanzania inaelekea kutushinda. Kama Mexico, tulishindwa kuchukua hatua mapema pale umma ulipoanza kulalamika, na sasa zimwi la ufisadi limekuwa kubwa.

  Kwa wiki mbili hizi, Raia Mwema limekuwa likiandika habari ya uchunguzi wa ufisadi mkubwa unaofanyika Idara ya Ushuru wa Forodha ambapo familia moja ya Kiarabu inaelekea kufanikiwa kuwaweka mfukoni baadhi ya vigogo wetu wa serikali na TRA, na hivyo kujipatia mabilioni ya fedha kila mwezi kwa njia ya ukwepaji kodi wa makontena ya bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam.

  Wafanyakazi wa kawaida ndani ya TRA wanalalamika kuhusu ‘kuogopwa’ na kulindwa kwa makampuni ya kutoa mizigo bandarini ya familia hiyo. Moja ya sababu za kulindwa eti ni kwa kuwa familia hiyo inaichangia CCM mamilioni ya pesa za kampeni.

  Wafanyabiashara nao wanalalamika kwamba wanalazimishwa kuzitumia kampuni za familia hiyo kutoa mizigo yao. Na hata baadhi ya maofisa wa serikali wanajua kuwepo mtandao wa familia hiyo, lakini wanauogopa kwa sababu ni ‘mradi’ wa wakubwa.

  Yaelekea wote wamekata tamaa kwa sababu kampuni hiyo inalindwa na vigogo. Kukata huko tamaa kumewafanya baadhi ya wafanyabiashara hao kuanza kupitishia mizigo yao bandari za Beira (Msumbiji) na Mombasa (Kenya), na hivyo kuzidi kuikosesha serikali mapato.

  Lakini wakati serikali inakoseshwa mapato ya kodi ya mabilioni ya pesa na familia hiyo moja tu, serikali hiyo hiyo inawakamua wananchi wa kawaida kodi kibao za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja!

  Majuzi hapa (kwa mfano) nilikwenda na Sh. 10,000 kununua umeme wa luku, na nilichoambulia ni kupata umeme wa Sh. 5,000 tu. Sh. 5,000 zingine ziliishia kwenye makato ya kodi kama vile Vat (asilimia 20), EWURA (asilimia moja) na REA (asilimia 3).

  Sasa mimi si mlalahoi wa kiwango cha kinyozi; lakini mfikirie kinyozi ambaye anakwenda na Sh. 10,000 kununua umeme wa luku kwa ajili ya saluni yake, na kisha anaambulia umeme wa Sh. 5,000 tu!

  Maana yake ni kwamba hata kabla hajaanza kunyoa kichwa kimoja, tayari serikali imeshatwaa shilingi zake 5,000! Kwa hali hii, ni lini huyu kinyozi atajikwamua kutoka kwenye umasikini?

  Sasa naamini kweli kwamba umeme katika Tanzania ni ghali kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika iliyo Kusini mwa jangwa la Sahara, lakini hiyo nayo ni simulizi nyingine mpya!

  Lakini wakati serikali inamkamua kinyozi huyo kwa kumkata kodi kama hizo, inakubali kupoteza mabilioni ya pesa za kodi kutokana na ufisadi unaofanywa na familia moja tu wa kukwepa ushuru wa forodha katika bandari ya Dar es salaam.

  Ufisadi huo wa ki-Mafia katika idara ya Ushuru wa Forodha, ni mfano mmoja tu wa mtandao wa mafisadi ambao ni mpana mno hapa nchini, na ambao tusipoangalia utapanuka na kuwa na ‘watu wao’ katika kila sehemu ya maisha yetu kama ilivyo Mexico.

  Hivi sasa mtandao wa mafisadi katika Tanzania unahaha kufanya kila aina ya mbinu ili wabunge wanaopiga kelele kuhusu ufisadi wasichaguliwe tena katika uchaguzi mkuu wa Oktoba. Wanataka bunge zima lijae ‘watu wao’. Wanataka pia chama tawala CCM kijae ‘watu wao’, na ikiwezekana mawaziri na rais pia wawe ‘watu wao’.

  Na kama tutawaachia wajaze ‘watu wao’ kila kona inayogusa maisha yetu; basi vita dhidi ya ufisadi itatushinda kabisa kama ambavyo Mexico inaelekea kuishindwa vita dhidi ya drug cartels.

  Ndugu zangu, tutakuwa na rais mpya kila baada ya miaka 10 lakini kama CCM ni ile ile, na kama tutaacha mtandao wa mafisadi uwe na ‘watu wao’ katika kila idara za serikali na katika asasi nyeti, ukiongozwa na kina “El Chapo” wao, hakuna kitakachobadilika. Kwa Watanzania wengi itakuwa ni kilio na kusaga meno tu!

  Hiyo ndiyo simulizi ya A Tale of Two Countries (Mexico na Tanzania).

  Itafakari.

  Barua-pepe: mbwambojohnson@yahoo.com
   
 2. Halisi

  Halisi JF-Expert Member

  #2
  Jun 17, 2010
  Joined: Jan 16, 2007
  Messages: 2,810
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
 3. Ndahani

  Ndahani JF-Expert Member

  #3
  Jun 17, 2010
  Joined: Jun 3, 2008
  Messages: 14,324
  Likes Received: 1,791
  Trophy Points: 280
  Mitandao wanayoiunda kwa ajiri ya kupata maslahi yao ya kisiasa ni sisi walipa kodi ndio tunahenyeka nayo kwasababu ya kujaza watu ambao ni "wajanja" wa mitaani na deal zao, bila kuwa na uwezo wa kulisukuma gurudumu la maendeleo mbele. Hii mitandao sasa ifike mahala iwe na kikomo.
   
Loading...