Ulitima unaweza kuvunja ndoa………..

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,810
15,393
Ni watu wachache sana ambao hawababaishwi na kuwa au kutokuwa kwao na fedha. Kuna ukweli kwamba fedha huvunja udugu, huharibu uhusiano kati ya watu na kati ya wapenzi. Ni vigumu na hatari kulikataa hilo. Kuna ukweli wa kutosha kwamba, kwenye ndoa, fedha ina athari kwa wengi sana. Taarifa za kiutafiti zinaonesha katika takwimu zake kwamba, wanandoa wanaoishi katika ulitima, wako kwenye nafasi kubwa ya kuburuzana na kusukumana hadi kufikia mahali mpaka kuachana na hata kuuana. Kwa wale ambao kipato chao ni kidogo wanajua ni kwa namna gani, ndoa zao wanavyozioa chungu.

Mtu anaweza kuuliza, inakuwaje mwanaume anamwambia mkewe kwamba, ana nuksi ndio maana hawapati fedha? Ni kwa sababu kukosa fedha kunataka subira kubwa ili mtu asiweze kupoteza mwelekeo kimaisha. Wataalamu wanasema watu ambao kipato chao ni kidogo sana, wanaposhindwa kukubaliana na hali halisi, huingia mahali ambapo husongeka sana. Wanaposongeka huanza kuwa na tabia zenye kuwakera wao wenyewe na kuwakera wale wanaowazunguka. Hali ya kusongeka huzalisha hasira za ziada, huzalisha hisia za kutojitosha, kufikiri kusikofaa, kukosa hamu ya tendo la ndoa, kukata tamaa na mengine ya aina hio. Hayo yanapojitokeza, ndoa huanza kuingia kasoro.

Hali hiyo huwatokea wote, yaani wanawake na wanaume. Kumbuka kuna wanawake ambao, hata kama ni mama wa nyumbani, bado wanatamani kama wangekuwa kwenye ndoa zenye nafuu ya kipato. Hii huwajengea kusongeka ambapo. Nao huweza kuvuruga uhusiano. Jarida la Psychosomatic Medicine, linasema kwa mfano, suala la kipato kidogo husababisha msongo ambao, baadae huweza kuvunja ndoa na hili sio suala la watu wa rangi fulani, kabila fulani, au jinsia fulani. Ni binadamu yeyote anapokuwa na pato dogo, ambalo hakubaliani nalo.

Lakini wataalamu wanasema kinachoweza kuvunja ndoa siyo kipato kidogo, bali zaidi ni namna wanandoa wanavyokitafsiri hicho kipato chao. Mmoja au wote wakishindwa kukubaliana na hali hiyo, ni wazi hali itaanza kubadilika na msukosuko katika ndoa utaanza.
Watu wasio na kipato cha kutosha au masikini ambao wamekata tamaa, mara nyingi huwa ni wavuta bangi, wanywa pombe kupindukia wavuta sigara na watu wasio na mtandao wa kutosha kijamii. Hali hizi huchangia sana katika kufanya uhusiano wa watu hawa kushindwa kudumu. Kwa wale wanandoa ambao wanautazama umasikini kama changamoto, ambapo wanaamini kwamba, kwa kuwa karibu, kushirikiana na kuamini katika kumudu, mara nyingi hufika mbali kiuhusiano na hata kimafanikio pia. Kama ilivyo kwenye kukosa fedha, yaani kwenye ulitima, hali kadhalika fedha nyingi nazo huweza kuvunja kabisa ndoa. Lakini kinachovunja ndoa hapo siyo fedha nyingi, bali mitazamo mibovu ya wanandoa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom