Wapendwa, kila uamuzi wa kushiriki uchaguzi wowote ni uamuzi bora kwa chama cha siasa makini. Kila uchaguzi una mafunzo makuu kwa wahusika. Washindi na wale walioshindwa huwa wana somo fulani huwa wanalipata. Kusema ukweli hupatikana mafunzo muhimu ambayo huwa mtaji kwa chaguzi zinazofuata.
Kwa utangulizi huu, nawapongeza wote walioshiriki katika uchaguzi wa Igunga. Naamini walioshindwa wanapata mafunzo makuu zaidi kuliko walioshindwa. Kwangu mimi nimefarijika sana kwa Wanaigunga kusema siasa za udini hazina nafasi, japo sijui kama walioanzisha dhambi hii wameadhibiwa ipasavyo! Yeyote yule, awe CCM au CUF, aliyeko nyuma ya dhambi hii alistahili adhabu kali. Najua hakuna chama chenye sera rasmi ya udini, ila baadhi ya wanachama wachovu wantafuta njia ya kutokea. Ni juu ya chama kujichunguza na kujua ni mwanachama yupi kati yao anayo mawazo hatari ya udini. Chama kikiisha baini ni nani kinatakiwa kumtenga na kutangaza hadharani. Kikishindwa kufanya hivyo, unapashwa kuwapo mfumo rasmi wa kisheria wa kukichukulia hatua kali.
Ni waulize nyote, tunao mfumo wa aina hiyo katika mfumo wetu?