Ukweli kuhusu Demokrasia nchini Tanzania

Ukweli kuhusu Demokrasia nchini Tanzania

DaudiAiko

JF-Expert Member
Joined
Dec 2, 2012
Posts
409
Reaction score
343
Wanabodi,

Kwanza kabisa napenda kuipongeza serikali ya Rais Samia kwa juhudi zote zilizofanyika kuleta maendeleo Kigoma na Tanzania nzima kwa ujumla. Maoni yangu hayata egemea upande wowote bali ni uchambuzi mfupi kuhusu misingi ya demokrasia.

Ili demokrasia idumu kuna mambo fulani ambayo lazima yawepo. Cha kwanza ni uwezo wa wananchi kuchagua viongozi wao katika chaguzi mbalimbali kwa njia ya amani, pili, uhuru wa vyombo vya habari unao wezesha wananchi kuelimika kuhusu uendeshaji wa nchi yao, tatu, mahakama inayo endesha shughuli zake kwa uhuru na mwisho, uwepo wa kambi ya upinzani katika suala zima la kuhakikisha kwamba maamuzi ya serikali yana chambuliwa vya kutosha kwa madhumuni ya kuwasaidia wananchi.

Uhusiano kati ya maarifa ya umma na uhuru wa vyombo vya habari: Hayo yote niliyo yaeleza mwanzoni yana dhihirisha kwamba uelewa wa wananchi kuhusu mambo mengi ya serikali ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba wanafanya maamuzi sahihi kwenye kila chaguzi. Elimu hii mara nyingi, hutoka kwa vyombo vya habari. Nitatoa mfano mmoja kutoka kwenye demokrasia iliyo endelea ambapo ufahamu wa wananchi hutiliwa maanani kwenye uchaguzi.

Kwenye nchi ya Marekani, uzito wa ushindi wa mgombea wa urais hutofautiana kwenye kila jimbo uchaguzi. Mfumo huu huhakikisha kwamba maamuzi ya waelewa zaidi huchukuliwa maanani kuliko maamuzi yanayofanywa bila ya kuwa na taarifa za kutosha. Haya yote labda hayawezi kuigwa, labda yatahitaji mlolongo mrefu kufanyiwa kazi lakini ukweli wa mambo ni kwamba serikali haiwapi wananchi fursa yakujifunza kwa undani zaidi kuhusu uendeshaji wa nchi yao.

Kutatua tatizo hili serikali inabidi ipitie upya sheria zinazohusu vyombo vya habari haswa katika uwezo wake wa kufungia vyombo hivi. Ni muhimu kuwa na vipengele vya wazi na vinavyo eleweka kwenye katiba kuhusu mipaka ya vyombo vya habari na mipaka ya serikali. Demokrasia haiwezi tena kuwa demokrasia kama katika masuala kama haya, vyombo vya habari havipewi nafasi ya kujitetea.

Adhabu za kukiuka maadili yoyote lazima ziainishwe wazi na ziendane na makosa. Kwa mfano: faini kwa chombo cha habari au mwana habari, kufungiwa kwa muda kwa chombo cha habari au mwana habari na kufungiwa jumla kwa chombo cha habari au mwana habari. Ili kuzingatia weledi katika kazi zao, wana habari wote wangetakiwa kuwa na usajili baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina na kwa wao kudhibitisha kwamba watatii sheria zote kikamilifu.

Vilevile serikali ingetakiwa kuwa na kitengo maalum kushughulikia mambo haya ikiamini kwamba hata kiongozi afanye mema kwa kiasi gani, lazima kuna ambao hawata kubaliana naye katika masuala mengine. Midahalo ya mara kwa mara kuhusu mambo tofauti tofauti ni afya katika kila demokrasia na kwasababu hiyo, ni muhimu kwa wana habari kuwa huru kufanya "Investigative journalism" na "Editorials" kwenye magazeti. Tofauti na maoni kutoka kwa wananchi, kura za maoni ni muhimu katika maamuzi mbalimbali kwasababu kushiriki kwenye uchaguzi kila baada ya miaka mitano tu haitoshi.

Sambamba na hilo, maamuzi kwenye chaguzi yangekuwa sahihi kwa asilimia mia kama wananchi wangefahamu kwa undani kuhusu maisha binafsi ya wagombea. Hili sidhani kama linawezekana na kwasababu hiyo ni muhimu kwa wananchi kushirikishwa zaidi kwenye maamuzi ya mara kwa mara. Inabidi tukubali kwamba umma wenye maarifa sio tishio kwa serikali bali ni kichocheo cha utawala bora.

Umuhimu wa kambi ya upinzani serikalini: Miaka ya nyuma, Chama cha Demokrasia na Maendeleo kiliwapa matumaini wananchi ambao hawaku ridhika na utawala CCM. Sasa hivi, miaka kadhaa baadaye, matumaini hayo yanazidi kufifia. Tukubaliane kwamba viongozi wa CHADEMA wanaweza wasiwe wakombozi na viongozi wa CCM wanaweza wasipige hatua kubwa katika suala zima la kutu kwamua kiuchumi. Lakini demokrasia siku zote inahusisha pande zaidi ya moja. Matokeo ya chaguzi yoyote yana baraka ya wananchi lakini je, walio vutiwa na sera za chama chochote cha upinzani wanafaidika kwa njia zipi?

Je, ni sawa kuwa na wawakilishi wachache bungeni kutoka vyama vya upinzani?, kitu gani kinasababisha kufifia kwa vyama vya upinzani?. Kama nilivyo eleza demokrasia siku zote inastawi kwenye midahalo na majadiliano kuhusu kila jambo. Hata kama wahusika hawakubaliani kuhusu jambo lolote, uchambuzi wa kina na usio na upendeleo ni chachu kwa makubaliano. Je tupo tayari kuweka tofauti zetu pembeni na kukaa meza moja kujadili suala lolote?. Je kiongozi yeyote anayesema kwamba yupo tayari kufanya kazi na viongozi wa vya vyama vyote amedhamiria kweli?

Yote haya ni ya kuzingatiwa kama kweli tunataka kuwa na demokrasia ya kweli. Changamoto hizi zinaweza kutatuliwa kwa kuruhusu vyama vya upinzani kufanya shughuli zozote za siasa kama zinazofanywa na chama tawala na kama ilivyo ainishwa kwenye fungu la 18 na 20 la katiba. Naamini kwamba mipaka ya ruhusa hii na tafsiri ya uchochezi iki chambuliwa kwa kina na kuorodheshwa kwenye katiba itawa nufaisha wahusika wote. Sambamba na hilo, sheria ya kupitisha angalau robo tatu ya wabunge wa upinzani kwa kuteuliwa au kuwapa wabunge hawa asilimia arobaini ya "Voting rights" kwenye maamuzi yote lita tatua tatizo la wabunge wa CCM wote kuunga mkono hoja zingine bila kuwa na sababu za msingi. Vilevile wabunge wa vyama vya upinzani wanatakiwa kujifunza kupingana kwa hoja. Kususia mikutano au mijadala sio sahihi.

Uhuru wa mahakama:
Yote niliyo yaeleza mpaka sasa yana uhusiano mkubwa na uwezo wa mahakama kutekeleza wajibu wake. Kama mahakama haiko imara, kusimamia mabadiliko haya ni ngumu. Inawezakana kwamba haki hutendeka katika nyadhifa zote kwa wananchi lakini je viongozi?. Mahakama ya kimataifa ya ICC ilianzishwa ili kutoa haki kwenye kesi za watuhumiwa ambao hawawezi kuhukumiwa nchini mwao kwasababu ya umashuhuri wao.

Mtanzania yeyote kuhukumiwa ICC ni ishara ya kwamba mahakama nchini haziwezi kuwa hukumu watu wenye hadhi fulani. Je unaweza kuishtaki serikali na ushinde?. Je haki inaweza kutendeka kwa yeyote anaye pinga matokeo ya uchaguzi mahakamani?.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania
 
Back
Top Bottom