CCM hawana mbinu.Hicho wakifanyacho ,ambacho wao wanakiita "mbinu" kwangu mimi si mbinu.Ninavyofahamu,mbinu za kweli zinaanzia katika hatua za awali kabisa:kupata mgombea kwa kutumia njia za wazi,huru na zenye usawa,ikifuatiwa na kuweka mpango makini wa kampeni, kutafuta kura kwa kufanya mikutano mingi ikilenga kufafanua sera,mipango na mikakati mbalimbali kulingana na matatizo ya sekta mahususi na hivyo kuvutia uungwaji mkono wa wananchi, kupigiwa kura za hiari na wananchi na hatimaye kulinda kura.
Mathalani,kamanda Nassari ameweza kufanya jumla ya mikutano 109.Hakuna kiijiji hata kimoja ambacho hakukifikia na baadhi ya maeneo ameenda hadi katika vitongoji. Sumari, huenda kwa "ushauri" wa walopokaji wake, ameenda vijiji 40! Sasa ,kama yeye hakuwafikia wapiga kura wa kutosha hana sababu ya kutafuta mtu wa kumlaumu isipokuwa yeye mwenyewe na wana - mikakati wake . Asitafute huruma ya Tume ya Uchaguzi wala polisi ikiwa wananchi hawakuweza kuwekwa katika mazingira ya kushawishika kumhurumia katika siku 21 za kampeni.
Katika uchaguzi wa leo Arumeru, imenuiwa kuwa ushindi hautapatikana mezani. Haiwezekani watu wazunguke vijiji vyote vya jimbo,wakijenga hoja makini,wakati mwingine wakose muda wa kupata chakula na kupumzika, halafu bado yupo mtu, kwa uchovu wa tafakuri anaota ushindi kwa kufanya miadi na viongozi wa Tume ya Uchaguzi! Haiwezekani.Ifahamike wazi kuwa,ushindi hautatolewa na Jaji Lubuva wala Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arumeru.Badala yake,ushindi utaamuliwa na kutolewa na wapiga kura wa Arumeru Mashariki.