Richard Bukos na Makongoro Oging
ELIZABETH Florian Eliza, Mkazi Dar es Salaam, wiki iliyopita alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kukutwa na hatia ya kuvua nguo mahakamani.
Eliza, alifanya kitendo hicho kama sehemu ya kupinga mashtaka dhidi yake ambayo alisomewa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive, Dar es Salaam.
Mrembo huyo, alisomewa mashtaka ya ukahaba kisha akakiri kosa, alipohukumiwa kulipa faini ya shilingi 20,000, alivua nguo na kubaki mtupu.
Kutokana na kutenda kosa hilo waziwazi, tena mbele yake, Hakimu Mkazi, William Mutaki, alimhukumu kwenda jela miezi sita.
Binti mwingine, Evonia William (anaonekana ukurasa wa kwanza akilia), aliibua hekaheka ya aina yake mahakamani.
Evonia, baada ya kusomewa mashtaka ya ukahaba, alikana kosa, hivyo akatakiwa apate wadhamini.
Hata hivyo, baada ya kukosa wadhamini, aliamriwa kwenda mahabusu Gereza la Segerea, Dar, mpaka Januari 31, mwaka huu.
Kutokana na amri hiyo, Evonia aliangua kilio, hivyo kuibua hekaheka ya aina yake, ingawa askari wa mahakama hiyo walifanikiwa kumtuliza baada ya muda mrefu.