Ujumbe maalumu kwa mheshimiwa Tundu Lissu

Nilipata taarifa za kupigwa kwako risasi muda mfupi tu baada ya tukio kupitia kwa mmoja wa watu ninaowaamini sana! Ingawa ulikuwa ni mchana lakini mwili wangu ulitetemeka sana! Mungu anajua nilichokifanya muda ule. Baadaye niliandika katika ukurasa wangu kuomba Mungu akuponye. Mungu amejibu maombi ya wengi na sasa umepona jambo ambalo linafaa kuitwa muujiza wa Mungu. Jambo lililokutokea linatosha kabisa kwa mtu kama alikuwa hamjui Mungu basi huo ndio unakuwa mwanzo wa kuutafuta uso wa Mungu.

Usiku wa leo ninao ujumbe kwako. Unapoendelea na harakati zako za siasa, huna budi kusamehe na kumuomba Mungu akuondolee chuki na uchungu moyoni mwako dhidi ya mtu au kikundi cho chote unachoweza kufikiri au kuhisi kuwa kilikuwa nyuma ya tukio la kushambuliwa kwako. Jambo hili sio jepesi hata kidogo bali unahitaji kumuomba Mungu akupe neema hiyo na ujasiri huo. Uchungu ukiruhusiwa kukaa katika kifua chako inaweza kuwa ni vigumu kwa mbingu kukupa nafasi kubwa zaidi baadaye! Ndiyo, mbingu zitaruhusuje mtu mwenye uchungu au chuki kushika madaraka makubwa? Kwa sababu akiruhusiwa ataweza kuyatumia kulipa kisasi jambo ambalo Mungu hataki kwa sababu kisasi ni cha kwake yeye Mungu.

Nelson Mandela alipokuwa tayari kusamehe ndipo Mungu akaruhusu atawale. Kwa mtazamo wangu, ukuu wa Nelson Mandela haupo katika mateso aliyopata na muda aliokaa gerezani pamoja na harakati zake. Bali ukuu wa Mandela ulitokana na kitendo cha yeye kusamehe waliomtesa miaka mingi. Nelson Mandela wakati mwingine alifikia hata hatua ya kumpa nafasi aliyekuwa mtesi wake mkuu kukaimu Urais wakati yeye hayupo.

Ninasoma, ninasikia na wakati mwingine ninaona yanayoendelea. Siyo siri, baadhi ya watu wananena mambo magumu na mabaya dhidi ya watu wanaowadhania walikuwa nyuma ya tukio lako. Ninaogopa kuwa 'huruma' za watu wa aina hii ukizisikiliza sana zitaweza kuujaza moyo wako uchungu badala ya rehema. Ninakusihi katika Jina la Yesu usikubali moyo wako ujazwe au ujae chuki.

Ukuu wa Jenerali Obasanjo na hata heshima aliyokuja kuipata baadaye ulitokana na unyenyekevu alioupata akiwa gerezani. Katika mazingira ambayo hayakutegemewa, baada ya Jenerali Abacha kufariki ghafla, Mungu alimuondoa 'mrithi halali' Abiola ili kuhakikisha tu Obasanjo anatawala. Siandiki ujumbe huu kama mtabiri, hapana. Na wala siandiki ujumbe huu kwa lengo la kukuandaa au kutokukuandaa kwa nafasi za uongozi, la hasha. Ninaandika ujumbe huu ili kuiandaa roho yako na nafsi yako kumruhusu Mungu aliyekuokoa kutoka katika bonde la uvuli wa mauti ili akuelekeze vizuri yakupasayo kufanya.

Ni dhahiri kuwa nafsi iliyoumizwa na inayoruhusu uchungu kifuani haiwezi kusikia ipasavyo sauti ya Mungu.
Kwa kuwa wewe ni mwanasiasa, utakuwa pia umemsoma Mahtma Gandhi yule kiongozi mashuhuri wa India aliyeiruhusu Biblia iongoze harakati zake ingawa yeye mwenyewe hakuwa Mkristo.

Ninajua kuwa ujumbe huu unaweza usipendwe na baadhi ya watu hasa wale waliojaa uchungu mioyoni mwao kwa kuwa unalenga kukutaka usamehe. Lakini ni wajibu wangu kama Askofu kukutaka hivyo. Watu hao watakaposoma ujumbe huu nao watasaidika. Ni dhahiri kuwa Mungu akitaka ufike sehemu utafika na akitaka usifike sehemu hautafika.

Kuna uhuru katika kusamehe! Kuna baraka katika kusamehe (Zaburi 32). Kuna ushawishi katika kusamehe! Kuna ulinzi na usalama katika kusamehe kwani mtu anayetangaza msamaha huwasababisha hata adui zake waweke silaha zao chini. Kinyume chake, mtu asiyesamehe anawafanya adui zake wajihami zaidi na hapo ndipo mapambano yanakuwa mazito kuliko ya awali.

Ninakutia moyo upate nafasi ya kuisoma Sala ya Bwana kwa tafakuri nzito. Mungu akikujalia neema na utayari kuchukua hatua ya kutangaza msamaha hadharani atakuongoza na atakuinulia watumishi wa Mungu watakaoandaa ibada kwa ajili hiyo au kukutia moyo kwa namna ambayo Mungu atakuongoza. Unaweza kutumia tukio lililokupata kwa ajili ya kumpa Mungu utukufu kwa njia ya kutangaza msamaha.

Utukufu uwe kwa Mungu awapae wakuu uwezo wa kutawala; awakwezaye wanyenyekevu na awashushaye wenye kiburi.

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania (KMUT) & Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani
Nimebarikiwa kweli kweli na ujumbe huu!
 
Kama alikuwa anajiuliza ataanzaje kurudi na kusamehe lakini zaidi sana kutuomba msamaha Watanzania kwa maana hakututendea haki, umempa ufunguo. kama ana akili autumie sasa tena bila kuchelewa.
Fala wewe, awaombe msamaha watanzania kwa lipi alilowakosea?? Haya nyie mnaojivika kofia ya watanzania mlifanya lipi kumsaidia pale alipokua na hali mbaya ya kupigania uhai wake baada ya kushambuliwa??
 
Back
Top Bottom