UJUMBE KWA BINTI YAKo

Kalamu Yangu

JF-Expert Member
Dec 21, 2016
1,094
1,031
IMG_6975.JPG
KWAKO MWANANGU MPENZI

Naandika kwa furaha,furaha ya kuwa nawe,
Nataka upate raha,usilie juu ya mawe,
Upendo na uwe silaha,pendo lako uligawe,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Usiyashike maneno,kukashfu ulimwengu,
Ukaja yaficha meno,kuhofu ya walimwengu,
Ulishike langu neno,siogope ulimwengu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Mama na babako tupo,twakuombea kwa Mungu,
Hata ikiwa hatupo,usiuote uchungu,
Na wema wa Mungu upo,wastahili lako fungu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Brigita na Anita, majina tuu mwanangu,
Vyovyote tungekuita,hata jina la mamangu,
Majina ni ya kupita,hayo ni chaguo langu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema,

Usihofu ufukara,hicho ni kitu kidogo,
Ni akili pia busara,hutochukia mihogo,
Mwanangu kugangamara,si kutwa kupiga zogo,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Usiisake sababu,ya kuukosa ukapa,
Sijui tangu mababu,ufukara upo hapa,
Kujituma ni jawabu,kweli hutotoka kapa,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Pia usijidanganye,utaupata kwa mume,
Ukwasi akunyang'anye,moyo uje ukuume,
Mwanangu kutwa uhanye,matunda uje uchume,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Alice kipenzi changu,wewe ni faraja yangu,
Nimekupa damu yangu,umebeba sura yangu,
Faraja ya mke wangu,twasema asante Mungu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Utapata marafiki,pia hata maadui,
Pia kuna wanafiki,ambao huwatambui,
Uwe rafiki wa dhiki,upendo haubagui,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Kuna nyakati za dhiki,zisikutoe akili,
Kufuru usidiriki,muhimu kustahimili,
Hiyo mikiki mikiki,isije haribu mwili,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Wana maneno matamu,kutaka kukupoteza,
Wakikidhi zao hamu,ubaki kuomboleza,
Rahisi kuwafahamu,mama atakueleza,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Wengi wanaharibiwa,kila iitwayo leo,
Wengi wanajaribiwa,kwa maneno na vileo,
Akili za kuambiwa,zisije kupa vimeo,
Kwako mwanangu kipenzi,dunia mahali pema.

Mama msikize sana,atakushauri mengi,
Usiwaze kugombana,hekima iwe msingi,
Hakutokuwa na mana,ukimwekea vigingi,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema

Mungu muweza wa yote,mshukuru muamini,
Simwache siku yoyote,sipaparikie dini,
Siwaze kuwa Dangote,bila Mungu kuamini,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Malezi ni kazi ngumu,ya akili siyo mwili,
Usiongeze ugumu,ukiutumikia mwili,
Ukaja tamani sumu,ukaharibu akili,
Kwako mwanangu kipenzi,dunia mahali pema.

Mheshimu kila mtu,tajiri na hoe hae,
Ila uthamini utu,utu pipa ujae,
Ila usije thubutu,madume yakuhadae,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Dunia mahali pema,kila mtu na riziki,
Waza kuyatenda mema,na usiwe mzandiki,
Nikifa ‘talala vyema,Mungu ukimsadiki,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.
 
Back
Top Bottom