DOKEZO Ujenzi wa VETA, Mkuranga (Pwani) kuna vitu havipo sawa, TAKUKURU, Serikali ichunguze kinachoendelea nyuma ya pazia

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'
A

Anonymous

Guest
Mwaka 2020 Kijiji cha Shungubweni, Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani, sisi Wananchi wa Wilaya kwa kushirikiana na Mbunge wetu Abdallah Ulega tuliwasilisha maombi ya kujengewa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA).

Tuliamua kufikisha maombi hayo kwa kuwa asilimia kubwa ya vijana wenzangu wa huku Kijiji cha Shungubweni hatukupata nafasi ya kuendelea na masomo ngazi za juu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufeli shule na mambo mengine kadhaa.

Maombi hayo yakapitishwa na Serikali Kuu, ndipo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Shungubweni kukatoa eneo lenye ukubwa wa karibu hekari 50 (niwe mkweli sina uhakika wa hizi hekari), taratibu zote zikafuatwa kwa ajili ya upimaji n.k hadi kufikia kupatikana kwa Hati Miliki.

Mzabuni akapatikana kihalali kabisa na matangazo yakawekwa kusubiri ujenzi uanze rasmi, muda wote huo mchakato ulikuwa ukisimamiwa na viongozi kadhaa ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Wananchi tukawa na furaha kuwa Serikali inawatendea jambo jema sisi Wananchi wake.
d98c334b-e5b3-4cc8-9af1-163f385cf174.jpg

Eneo la Kijiji cha Shungubweni, ambalo limetelekezwa

Ghafla, matangazo na mabango yaliyokuwepo eneo la tukio ambapo kulitakiwa ujenzi uanze yakaanza kutolewa.

Wananchi tulipojaribu kuuliza ikatoka amri kuwa lazima mpango wa ujenzi usimame, hakuna kuendelea na ujenzi na mradi unahamishwa.

Mkuu wa Wilaya wa Mkuranga, Khadija Nasri Ally na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama wakasema ujenzi wa VETA utafanyika kwenye shamba ambalo linatumika kwa ajili ya utafiti wa zao la korosho.

Bila kutaja sababu wakasisitiza ujenzi wa VETA lazima ufanyike hapo, Bwana shamba ambaye naye ni mwajiriwa wa Serikali anayesimamia shamba la Mikorosho akagoma kuwaruhusu DC (Mkuu wa Wilaya) na watu wake kuendelea na taratibu za ujenzi wa VETA katika eneo hilo.

Kilichofuata ni nguvu kuanza kutumika ikiwemo kumpa vitisho wasimamizi wa eneo husika kuwa lazima waachie shamba.

Walipoona wanagoma simu ikapigwa kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Mohamed Bashe akatoa maagizo kuwa DC na watu wake wachukue shamba hilo la Mikorosho na ijengwe VETA.
bf801577-35bc-43e4-bc40-3cff77f10250.jpg

ecd0ce70-6262-4be3-a1eb-7df7e8dd658a.jpg

Eneo la pili ambapo ndipo mradi unafanyika fastafasta

Kila tukihoji sababu ya mabadiliko hayo hatupati majibu zaidi vitisho vinatawala, huku lile eneo la wazi lililotolewa na Wanakijiji likiachwa wazi.

DC akawa anawatishia viongozi wenzake wanaoonekana kupinga maamuzi yake.

Baada ya wasimamizi kuona vitisho vinazidi wakaamua kuliachia shamba hilo bila kuwa na nyaraka zozote kutoka Serikalini kuwa eneo hilo la shamba litumiwe kwa ujenzi wa VETA.

Kinachotushangaza wengine ni kuwa mchakato wa awali kila kitu kilifanyika kwa kufuata taratibu zote lakini huku eneo la pili ambalo lipo Kiparang’anda, Mkuranga Mjini taratibu zilizofanyika kwa ajili ya kupata eneo hilo.

Kama nia ni nzuri ya kusaidia jamii, kwanini DC na watu wake wanatumia nguvu kubwa, vitisho na njia za mkato kufanikisha hilo.

Japokuwa inadaiwa DC anashinikizwa na Mbunge wa eneo husika kufanya maamuzi hayo kwa maslahi binafsi ambayo sisi Wananchi hatuyajui.

Mfano hiki karibuni kulikuwa na DAS ambaye anapinga huo mchakato, wenyewe (wanaosimamia mradi) wakatamba kuwa watamuondoa, kweli mkeka wa mama ulivyofuata jamaa akaondoka.

Inakumbukwa kuwa Tarehe 8 wakati wa Sikukuu ya Wakulima, Rais Samia Suluhu akiwa Mkoani Mbeya alitoa onyo na kupiga marufuku uuzwaji au uchukuliwaji wa mashamba ya utafiti kama hilo la Mikorosho lililochukuliwa, sasa inakuwaje hawa watu wanafanya wanavyojua wao na kukiuka maelekezo ya Rais?

Wito wangu na wito wetu sisi Wananchi wa Mkuranga kwenda kwa mamlaka za juu ikiwemo Taasisi ya TAKUKURU kufuatilia kinachoendelea nyuma ya pazia na kutafuta kiini cha mambo kadhaa:

1. Kwa nini mradi umehamishwa eneo bila ridhaa ya Wananchi?
2. Kwa nini viongozi hawajafuata taratibu kuhamisha eneo la mradi?
3. Eneo la awali lililotolewa na Wananchi na Hati Miliki kutolewa litatumika kufanya nini?
4. Kwa nini DC anatoa vitisho kwa watu wanaopinga mchakato unaofanyika kuwahoji?
5. Mbunge wa eneo husika anajua kinachoendelea lakini yupo kimya, je ni kweli anahusika?
6. Kwa nini wameenda kuharibu Shamba la Utafiti wa Mikorosho wakati eneo la wazi lilikuwepo?
7. Kwa nini Bwana Shamba aliyekuwa akisimamia shamba la Mikorosho hakupewa nyaraka ya kutakiwa kukabidhi shamba hilo?
 
Back
Top Bottom