EMT
Platinum Member
- Jan 13, 2010
- 14,477
- 15,347
Ukubwa hauna ngoma ya utambulisho, kadhalika uzee hauna parapanda. Pindi yanapokufika basi utayaona na huna budi kuyakubali. Hayupo awaye yote aliyejaribu na kufanikiwa kukwepa majukumu haya yasiyo ya hiyari. Ukimwona mtu anayakwepa, basi uwe na uhakika kuwa anajaribu kukitoroka kivuli chake bila mafanikio,
Jimama mmoja aliketi jirani yangu kule katika viwanja vyangu vya kujidai. Tofauti na wateja wengine, mwenyewe alimkera karibu kila mteja pale. Alivaa wigi, kimini, kitopu, mikufu, bangili, hereni na zaga zote unazozifahamu. Usoni lilipaka marangirangi, wanja na rangi za mdomo na macho.
"We, DJ unapiga nyimbo gani?" Aling'aka baada ya kusikia zilipendwa zikirindima kutoka kwenye vipaza sauti. "Ulitaka kusikiliza nyimbo gani?" Nilimuuliza taratibu ili asiendelee na bwato litakalosababisha stimu zangu ziruke. "Au taarabu?"
"Koma wewe!" Alinitolea macho, "Umeona hii ni namba ya kusikiliza taarabu?" Kisha akamgeukia tena DJ, "Kuwa kama mtoto wa mjini wewe. Piga ngoma za kileo. Madude mapya kibao yameingia. Wa wapi wewe?"
Nikaona huyu sasa ana yake. Wanywaji wote wamezikubali nyimbo zinazoendelea kusikika, basi angefanya subira hadi wakati wa mchanganyo wa nyimbo, hata zile anazozipenda zitapigwa tu. DJ anajua kazi yake na anajua apige nini kwa wakati gani. Tena basi, nyimbo za kipindi kilichopita zilikuwa zimegawanyika vizuri sana. Ukiingia baa utapigiwa nyimbo za baa, ambazo hata mlevi anacheza. Sikiliza wimbo wa "Embe Dodo". Kwanza hupati shida ya kuumiza kichwa kutafuta tafsiri. Just embe dodo limelala mchangani, kwisha!
Pili, unaweza kucheza kwa kutingisha kidole tu, huku ukipiga funda zako. Siyo lazima uinuke, ushushe suruali hadi magotini (zamani tulipandisha hadi kifuani), wala kukaza misuli ili kurukaruka. Hata wazee waliweza kucheza. Basi nilimuuliza tena mama huyu: "Lakini mama na uzee huu unazimudu nyimbo za sasa?"
"Nimekwambia koma wewe! Uzee huko kijijini kwenu, Dar uzee unaishia Mkoa wa Pwani!" Alibwata na safari hii alikuwa ameshakasirika. Kwa hasira tena alinyanyua bilauri na kupiga funda kubwa, pombe ikampalia na akaanza kukohoa mfululizo. Alikohoa hadi akaketi sakafuni, wazee tukambeba na kumpa huduma ya kwanza.
Mnaambiwa mkitaka kuruka basi muagane kwanza na nyonga zenu… Uzee hauna baragumu. Hakuna malaika anayekuja kuteua wazee wapya kila mwaka, bali ukiona mambo yamekuwa nyuma mbele; juu chini ujue ndiyo tayari. Unaweza ukajifanya kijana wakati ukiwa mzee, lakini huwa ni kiini macho cha muda tu. Mtu wa aina hii hutumia muda mrefu mbele ya kioo akinyofoa mvi kwa kucha.
Wakati nikiyatafakari haya, nilipata mgeni mwingine mezani kwangu. Alikuwa kijana mtanashati, ambaye shepu, mavazi na lafudhi alifanana na mwanasheria au mhasibu mwenye mafanikio. Alivaa shati la buluu bahari na suruali nyeusi iliyopigwa pasi vizuri (yawezekana ilinyunyiziwa wanga wakati ikinyooshwa) na viatu vyeusi vilivyopigwa dawa kiusahihi.
Alinipendeza kwa maongezi yake. Alichangia mada na akaanzisha mpya. Tuliongea sana juu ya mabadiliko ya hali ya nchi na mabadiliko ya hali ya mifuko. Alidokeza kuwa siku hizi wabunifu wa mavazi wanashona mifuko ya suruali kwa vitambaa vigumu, tofauti na zamani waliposhona kwa vitambaa laini. Nilipomuuliza sababu alijibu kuwa wanaume sasa hutembea wakiwa na sarafu mifukoni badala ya noti kwenye pochi.
Tuliafikiana kuwa hali ya uchumi imekuwa mbaya. Lakini mwenzangu aliona ni zaidi ya uchumi. "Kila kitu kinaharibika kwa muda mfupi," alilalamika. "Hela zinachakaa mapema hali watoto wanaozihitaji wanakua haraka. Juzi tu alikuwa darasa la pili, leo anadai hela ya mtihani darasa la saba. Nauli nazo wamepandisha. Majuzi nilipanda basi Chang'ombe kuja Temeke shilingi tano; Ndiyo, lilikuwa daladala la ukweli lililoitwa "Riziki kwa Mungu".
"Sasa leo ati shilingi 400, safari moja tu hiyo. Nikaamua kutembea kwa mguu. Mungu wangu! Kumbe kile kilima cha Wailesi kimeongezeka! Nilipumzika mara mbili kabla ya kukimaliza. Nikasema ngoja nisome na gazeti bwana, kumbe na nyinyi mmepunguza ukubwa wa maandishi! Yaani tuneno tudogo tudogo…"
Nikamwangalia vizuri huyu kijana. Nikagundua kuwa weusi wa nywele na ndevu zake haukuwa orijino. Nikagundua kuwa hata ngozi yake imepigwa msasa kuondoa mikunjo iliyofanana na ya limao changa. Haraka nikamalizia kinywaji changu na kuondoka.
Na Gaston Nunduma
Chanzo: HEKAYA ZA MLEVI: Ujana maji moto, uzee maji baridi