Ndugu zetu,
Assalaam Alaaykum,
UMOJA, UHURU, UADILIFU
Qauli ya Umoja wa Wazalendo
Kukhusu Siku ya Uhuru wa Zanzibar
Date::4/6/2009
NCCR Mageuzi wataka siku ya uhuru wa Zanzibar
Fidelis Butahe
CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimeibuka na hoja mpya ya kutaka kutambuliwa kwa siku ya uhuru wa Zanzibar, kama ilivyo kwa siku ya uhuru wa Tanganyika.
Shukrani za Dhati Kutoka Moyoni mwa Wazanzibari
Hapana shaka Wazanzibari tutakuwa si wenye fadhila iwapo hatutatoa shukrani zetu za dhati kwa ndugu zetu NCCR, Mageuzi; viongozi na wananchi, bali khasa kwa Mhishimiwa Bwana Faustin Sungura kwa hili pendekezo adhimu kabisa la kutaka, kutambuliwa kwa siku ya uhuru wa Zanzibar
., Disemba Kumi, 1963.
Dola Huru Ya Zanzibar
Kwa Rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala, na juhudi za pamoja za kila Mzanzibari; taarikh 10 Disemba, 1963; Nchi yetu Zanzibar, ilipata Uhuru wake na kuwa ni Dola Huru Kaamili miongoni mwa dola za ulimwengu.
Sherehe Za Uhuru
Wananchi wote, wakubwa na wadogo, wanaume na wanawake, waliupokea Uhuru wa nchi yetu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala na kwa fura*ha na bashasha kubwa. Mji ulingara kwa mapambo ya namna mbali mbali. Tamasha hizi na zile zilifanywa na wananchi kwa kufurahikia Uhuru wao. Sherehe na mapambo hayakuwa Mjini tu, bali mashamba kote. Na huko Pemba nako kulifanywa sherehe kama za Unguja, tangu mijini mpaka mashamba. Wazanzibari tulijaa tamaa na matumainiyo ya kwamba baada ya juhudi na kazi ngumu ya kuleta Uhuru wetu na kwa kuondoka mtawala Muingereza sasa tutaweza kujenga Nchi yetu kwa pamoja. Haya yalielezwa hivyo na kiongozi wa Afro-Shirazi Party (ASP), Mzee Abeid Aman Karume katika munasaba wa siku hii adhimu kwa kusema:
Leo mwezi 10 Disemba, 1963, ZANZIBAR imekuwa Huru. Hii leo sisi watu wa visiwa hivi tumepata haki ya kuchukuwa mahala petu kuwa ni Dola sawa na nyengine katika umoja wa Nchi za Dola za Commonwealth. Kwa uchache, kuwa mwanachama katika umoja huo, kuna maana kwamba nchi hii ni huru chini ya mpango wa serekali ambayo msingi wake umejengwa juu ya kuendeleya kwa ridhaa ya wananchi.
Ili kufikiliya matarajiyo yetu hayo tunayo moja katika Katiba zenye msingi madhubuti iliyohusika na shuruti za haki za binadamu, haki za mambo ya siyasa na uhuru wa dola yoyote nyengine. Ni wajibu wa watu wote wa dola yetu mpya, kila mmoja katika sisi bila ya kujali fikra zetu za siyasa au madaraka yetu kusaidyia kweli kweli Katiba yetu iweze kufanya kazi. Pamoja na manufaa, haki na uhuru ambayo yote hayo yamepatikana baada ya nchi kuwa huru.
Tuliyoyapata leo mwezi 10 Disemba ni mipango ya mwanzo tu ya kuweza kufanya juhudi kwa ukamilifu dhidi ya maadui zetu nao ni ujinga, umasikini na maradhi na kuweza kuleta imani penye khofu na shaka na kuleta masikilizano mahala ambapo hata hivi sasa adawa ipo, na kuleta mapenzi mahala ambapo pana chuki, ili dola yetu mpya ichomoze katika neema, umoja na furaha.
Kwa hivyo katika hii siku ya leo na tumwombe Mwenye Enzi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala, Inshaallah atuweke tuifanye na tuitimilize kazi kubwa ya kujenga taifa letu ili dola yetu mpya ya ZANZIBAR ipate baraka ya matunda mema ya kazi zetu. Uhuru na Umoja, Uhuru na kazi!
Kusitishwa Kumbukumbu za Uhuru wa Zazibar
Baada ya Tanganyika chini ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kuivamia Dola Huru Kaamili ya Zanzibar na kuitia chini ya makucha yake kwa kisingizio cha huu wenyekuitwa muungano, hata pia bila ya ridhaa ya ndugu zetu wananchi wa Tanganyika; hapohapo ilisitishwa siku hii adhimu, siku ya Uhuru wetu, Disemba Kumi, 1963. Ilisitishwa kumbukumbu za Uhuru wetu na kuletwa hii nyimbo tunayoendelea baadhi yetu kuiimba mpaka hii leo uhuru wa bandia.
Wazanzibari Wanaikumbuka Siku ya Uhuru Wao
Kwa Rehma za Mola wetu Mlezi Subhaanahu wa Taáala na kwa kuzidi Uzalendo nchini mwetu, Zanzibar; Wazanzibari siku ya Disemba Kumi, 2008 walikusanyika kuikumbuka siku hii adhimu. Wazanzibari bila ya kuzingatia itikadi zao za kisiasa walikusanyika kwa kusoma maulidi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na kuwaombea duwa wazee wetu waliowania Uhuru wetu, walio tangulia mbele ya haqi na waliohai nasi. Sherehe hizi zilifanyika katika zaidi ya mitaa kumi na tano Nchini kote.
Pia waliwaombea duwa viongozi wetu, wa Sirikali na wa vyama vyote viliomo Nchini. Bali pia waliiombea duwa Nchi yetu kwa jumla, na khasa kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala atuondolee mfarakano na kutupa uwezo na tawfiiq ya kujenga Umoja baina yetu kwa maslaha ya Nchi yetu na vizazi vyetu. Alhamdulillah, kila ishara inathibitisha kwamba Wazanzibari tumo khatuwa na khatuwa katika kubomowa mfarakano na kujenga Umoja baina yeetu, wajibu shukra kwa kila hali na kila wakati kwa neema hii kuu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala atuzidishie tawfiiq kwa kila kheri kwa Nchi yetu na vizazi vyetu, Aamyn.
Wa Billahi Tawfiiq
Umoja wa Wazalendo
Zanzibar
April 07, 2009