Ugumu na Urahisi wa Kuing'oa CCM Oktoba 2010 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ugumu na Urahisi wa Kuing'oa CCM Oktoba 2010

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kulikoni Ughaibuni, Aug 12, 2010.

 1. Kulikoni Ughaibuni

  Kulikoni Ughaibuni JF-Expert Member

  #1
  Aug 12, 2010
  Joined: Dec 12, 2007
  Messages: 235
  Likes Received: 115
  Trophy Points: 60
  Katika uchaguzi mkuu ujao,Watanzania watakuwa na sababu nyingi za kuiondoa CCM madarakani kuliko za kuirejesha tena.Makala moja haiwezi kutosha kutaja sababu zote kwani ni nyingi mno.Hata hivyo,miongoni mwa sababu kubwa ni usaliti wa chama hicho tawala kwa Watanzania.Na si usaliti wa kawaida bali uliopelekea madhara makubwa kwa taifa letu.Pasipo kuingia kwa undani kuhusu uharamia unaoendelea kufanywa na CCM,chama hicho kimekuwa kikijibidiisha kukwangua kila raslimali tulizojaliwa na muumba kana kwamba kinataka kiondoke madarakani huku nchi ikiwa imekwaushwa kila kitu.Ni kwa sababu hiyo ndio maana baadhi yetu tunasisitiza umuhimu wa kuiondoa CCM sasa,na si baadaye,kwani kila dakika ya chama hicho kukaa madarakani ni dakika nyingine ya kifo cha "utajiri" wetu wa asili.

  Kuna ugumu na urahisi wa kuing'oa CCM madarakani.Tuanze na ugumu.Mtaji mkubwa wa CCM umekuwa katika historia kuliko hali halisi ya sasa.Kila mara chama hicho kimekuwa kikijigamba kuwa ndicho kinachodumisha "amani na utulivu" wetu.Kwa minajili ya kufanya makala hii iwe fupi sintoingia kwa undani kwenye mjadala kama kweli tuna "amani na utulivu".Hata hivyo,kila Mtanzania mlalahoi katika nafasi yake anaweza kuhoji kama mshahara kiduchu anaopata unaleta amani na utulivu katika familia yake,au mkulima anayekopwa mazao kila msimu huku vitambi vya viongozi wa vyama vya ushirika vikizidi kukua ana amani na utulivu rohoni.Katika makundi ya kijamii yanayoweza kuhoji "majigambo" hayo ya CCM tunaweza kujumuisha wazee wetu waliotelekezwa licha ya mchango wao katika kujenga nchi yetu,akinamama wanaolazimika kujifungua njiani kwa vile zahanati zenye upungufu wa madawa hazifikiki aidha kutokana na umbali au barabara mbovu,watoto na wadogo zetu wanaosomea sakafuni kutokana na uhaba wa madawati ilhali walimu wao wakitafakari namna ya kumudu gharama za maisha yao kutokana na mishahara kijungujiko na inayochelewa kuwafikia.

  Kwa vile CCM ilirithi mfumo dhalimu wa chama kimoja ambao haukutoa nafasi ya kuhoji mapungufu ya viongozi, sambamba na kila kauli ya kiongozi ikiwa na nguvu mithili ya zile za Muumba (na hata kama kauli hizo zilikuwa sahihi bado zilipaswa kudumisha....refer zidumu fikra sahihi).Kwa lugha nyepesi,mfumo huo wa kidikteta ulipelekea utiifu wa lazima kwa wananchi.Hata baada ya mageuzi ya kisiasa,CCM iliendeleza mazingira ya mfumo wa chama kimoja huku vyombo vya dola vikiendelea kutumika kwa maslahi binafsi ya chama hicho,na vikitumika pia kukandamiza kila aina ya jitihada za walalahoi "kujikomboa".

  Na ni hali hii ya "chama kushika hatamu" kwenye vyombo vya dola inayopelekea miongoni mwa ugumu wa kuing'oa CCM madarakani hapo Oktoba.Teuzi za viongozi wa vyombo vya dola zimeendelea kuwa mapendezeo binafsi ya Rais ambapo wateuliwa wameendelea kuwa na utiifu zaidi kwa Rais (kama mtu na sio "urais" kama taasisi) kuliko kwa taifa au vyombo wanavyoongoza.Katika mazingira tuliyonayo,viongozi wa vyombo hivyo wanageuka wanasiasa wasio rasmi kwa vile salama yao (na kubaki kwao madarakani) kunatafsiriwa nao kama kunategemea ushindi wa aliyewateua.

  Angalau basi teuzi hizo zingezingatia uwezo wa wateuliwa.Lakini hilo lina sababu yake,kwani kama mtu akiteuliwa kutokana na uwezo wake anaweza kabisa "kupuuza zawadi" aliyopewa na Rais kwa imani kwamba "niliteuliwa sio kwa vile Rais ananipenda bali ni kwa vile ameona uwezo wangu".Na ndio maana wenzetu wa nchi zilizoendelea wanatoa uzito mkubwa kwa uwezo wa kiongozi kwa vile wanafahamu kuwa pindi atakapokabidhiwa madaraka sio tu atataka kuthibitisha kuwa uteuzi wake haukufanywa kimakosa bali pia atatumia uwezo huo katika kutekeleza majukumu yake.Uteuzi wa fadhila unamfunga mteuliwa kwani anabaki na deni la fadhila kwa aliyemteua.Kwa kifupi,wateuliwa hawa wa Rais watapigana kufa na kupona kuona aliyewateua anaendelea kubakl madarakani.

  Kuna ugumu mwingine wa kihistoria kwa upande wa wapiga kura.Kutokana na CCM kuwa madarakani kwa muda mrefu,na kwa kutumia vibaya raslimali za serikali pamoja na fedha za walipakodi kujiimarisha,wengi wa wapigakura wanaaminishwa na chama hicho kuwa kuondoka kwake madarakani ndio itakuwa "mwisho wa dunia" kwa Tanzania.Ni rahisi kwa mie na wewe tunaoweza "ku-google" au kutofautisha kati A na B lakini hali ni tofauti sana katika rural areas ambazo yayumkinika kuamini kuwa zinanyimwa baadhi ya huduma muhimu kwa minajili ya kudumisha "ukoloni wa kifikra".

  Kwa mfano,baadhi ya maeneno ya vijijini yameendelea kutegemea Radio Tanzania (TBC) kujua kinachoendelea duniani.Unfortunately,chombo hicho kinachoendeshwa kwa fedha za walipa kodi kimeendelea kuipendelea CCM kana kwamba ni tawi la chama hicho.Kwa sie tuliobahatika kuwa na access ya vyombo mbalimbali vya mawasiliano tunaweza ku-underestimate role ya mass media katika kudumisha utawala dhalimu au kusambaza "sumu" dhidi ya kundi flani.Lakini tunaweza kujifunza kwa kuangalia role ya vyombo vya habari (vyenye mrengo dhalimu) katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda.Licha ya Radio Tanzania (TBC) baadhi ya maeneo ya vijijini yaliyobahatika "kuletewa maendeleo ya runinga" yanaendelea kupata "habari za upande mmoja" kutoka televisheni ya "taifa",wanazi wengine wa CCM.

  Kikwazo kingine katika kuing'oa CCM kipo tena zaidi kwenye rural areas ambapo ugumu wa kutenganisha serikali na chama ni mithili ya ilivyo ngumu kutenganisha CCM na ufisadi.Wakuu wa Mikoa na wakuu wa wilaya wamegeuka kuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya.Badala ya kufanya kazi za serikali pekee wao wamekuwa watumishi wa CCM.Kwa ujumla,serikali katika ngazi za mikoa na wilaya (na mlolongo huo unaendelea hadi ngazi ya mtaa) katika maeneo mengi nchini ni sehemu muhimu ya utawala wa CCM.Hali inakuwa mbaya zaidi unapojiri uchaguzi kwa vile watumishi wa umma ambao wanapaswa kutekeleza majukumu yao pasipo kuegemea chama flani wanaishia kuwa mawakala wa CCM na hivyo "kuviminya" vyama vya upinzani.

  Hali hiyo ya taasisi zinazopaswa kuwa "neutral" kumezwa na CCM inajitokeza tena kwenye taasisi mbalimbali za kiserikali katika ngazi ya Taifa,kwa mfano tume ya uchaguzi na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.Tatizo hapa linaweza kuwa linasababishwa na teuzi zinazofanywa na rais kutafsiriwa kama zawadi kwa viongozi wa taasisi hizo,na wao kuweka utiifu wao kwa rais na chama chake badala ya umma wanaopaswa kuutumikia bila kujali itikadi za siasa.

  Tukiachana na ugumu unaosababishwa na structures zilizofinyangwa ili kudumisha utawala wa CCM,kuna ugumu mwingine unaotokana na uoga wa CCM na mafisadi kuwa kuondoka madarakani kwa chama hicho kunaweza kupelekea hatma mbaya kwao.Unadhani mafisadi wanaokwangua utajiri wa taifa kila kukicha hawajui kuwa CCM ikiondoka madarakani wanaweza kuishia magerezani?Unadhani viongozi wa taasisi za umma waliojaza ndugu na hawara zao kwenye ajira za taasisi hizo hawajui kuwa kuondoka kwa CCM kutaweka wazi uharamia wao na hivyo pengine vibarua vyao "vitaota nyasi"?Unadhani mafisadi wa Kagoda hawajui kuwa,kwa mfano,Dokta Slaa akifanikiwa kuingia Ikulu watawekwa hadharani pasipo kujali nyadhifa walizoshika huko nyuma (na ambazo walitumia kufanikisha ufisadi huo)?Hawa wote wameunda unholy alliance na CCM kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi ujao ili waendelea kutufisadi.

  Sasa tuhamie kwenye urahisi wa kuing'oa CCM madarakani.Kwa kifupi,mchecheto ulioanza kuwaingia CCM unatokana na ufahamu wao kuwa mwaka huu wanakumbana na mgombea makini na ambaye rekodi yake haihitaji kufafanuliwa.Hapa namzungumzia Dokta Wilbroad Slaa.Mchecheto huo ni muhimu katika kupatikana urahisi wa kuiondoa CCM.Wameshtukizwa,hawakutarajia upinzani wa maana kumkwaza JK kurejea Ikulu,na hawana uhakika wa mkakati gani utakuwa bora katika kukabiliana nae.

  Of course,watajaribu character assassination lakini hilo sio rahisi sana kwa vile wanafahamu vyema characters za mgombea wao na pia wanajua kuwa zikipata "a better assassin" basi hawako salama.Kwa kifupi wanafahamu kuwa wanaishi kwenye nyumba ya vioo na wakianza kurusha mawe wataishia kuharibu nyumba yao pia.Lakini hiyo haimaanishi kuwa hawatatumia mbinu hiyo japo huenda isiwe mkakati mkubwa zaidi.

  Kingine cha kuleta matumaini ni hili songombingo linaloendelea la kura za maoni ndani ya chama hicho.Kwa upande mmoja,wengi wa watakaochojwa watabaki na kinyongo na hivyo kuwa tayari kumaliza hasira zao kwa kuchangia jitihada za kuran ya hapana kwa mgombea/wagombea wa CCM.Japo JK "aliwatuliza mzuka" watakaoshindwa kwa kudai kuwa "nafasi za kuteuliwa zipo" lakini ili teuzi hizo "za kishkaji" zifanyike itabidi JK ashinde kwanza uchaguzi.Sasa kipindi cha transition kati ya kampeni na uchaguzi kumalizika kinaweza kabisa "kulipua" hasira za walioshindwa hao.

  Baadhi ya wana-CCM "safi" watakaobwagwa wanaweza kupata sababu ya msingi ya kuachana na chama hicho.Hawa wanaweza kuwa mtaji muhimu hususan wale wenye majina na ushawishi.Siafikiani na wazo la kuzoa kila "reject" wa CCM kwani kuna wengine ni mafisadi na wanaweza kabisa "kuambukiza" ufisadi huo huko wanakokimbilia.

  Jingine linaloweza kuleta urahisi wa kuing'oa CCM ni kile wanachosema waswahili kuwa "ushirika wa wachawi haudumu".Wengi wetu tunafahamu namna fedha za EPA zilivyoliwa kabla hazijamwagwa kwenye kampeni.Naamini baadhi yetu bado tunakumbuka habari kuwa msambaza rushwa mmoja "aliingia mitini" na takriban shilingi milioni 80 kati ya milioni 100 alizopaswa kupeleka mikoani.Sasa,wakati huo Rais alikuwa Mkapa ambaye hakuwa mgombea kwenye uchaguzi huo.Kwa namna flani,uwepo wa Mkapa ulisaidia "uangalizi" wa namna fedha za umma zinavyoweza kufanikisha ushindi wa Kikwete.Na kwa vile alikuwa akikabiliwa na tishio kutoka kwa wanamtandao (ambao walikuwa tayari kuivuruga CCM kama asingetoa sapoti kwa Kikwete),Mkapa alijitahidi kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika "ipasavyo" (japo haikuzuwia waliokabidhiwa kuzifuja.Lakini by that time yeye alikuwa ameshatimiza wajibu wake kwa wanamtandao).

  Safari hii hali ni tofauti kabisa.Hakuna wa kumshikia mtutu wa bunduki kwa vile JK mwenyewe ndio mgombea.Hakuna wa "kumchimbia mkwara" kwa vile Rais ni Kikwete na si Mkapa au mtu mwingine.Japo kwa namna flani inaweza kurahisisha ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya "kununua ushindi" tatizo linakuja kwa wahusika wa kukusanya na kusimamia matumizi ya fedha hizo.Yani kukurahisishia uelewa wa hoja yangu hapa ni kwamba ni rahisi kwa mwizi kuiba akiwa mwajiriwa kuliko anapokuwa mmiliki wa sehemu aliyozowea kuiba.

  Hali ya fedha ya serikali yetu inafahamika.Wanaweza kukwangua huku na kule lakini wanafahamu kuwa takriban nusu ya fedha hizo zimetolewa na wahisani (na napenda kuamini kuwa wanafuatilia kwa karibu kuhakikisha fedha zao-at least some of it- haziibiwi kirahisi.Ilikuwa rahisi wakati wa Makapa kwa vile ni yeye ambaye angekuwa answerable,na pia alishurutishwa kusaka kila avenue ya ku-finance oparesheni ya mtandao kuingia Ikulu.Sasa hivi watamshurutisha nani wakati wao wenyewe ndio wenye dhamana,and therefore answerable?

  Okay,pengine utasema kuwa sasa wako kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujichotea fedha wapendavyo.Ugumu unakuja kwenye aina ya mgombea wanayekabiliana nae.Tayari tumeanza kuona "zama mpya" za kuripoti diversion ya fedha za umma ku-finance kampeni za CCM (Rejea habari za Mwanahalisi kuhusu Salva na utengenezaji wa "vifaa" vya CCM).Wanamjua vema Dokta Slaa,japo hawajui vema ni wapi anapopata nyaraka zilizotumika kuwaumbua for the past 5 years.Ni dhahiri kuwa hata kama fedha za umma ziko at their disposal watalazimika kuwa makini kupita kiasi ili siri zisivuje na kumfikia Slaa.Lakini wanakuwaje makini ilhali among them kuna wenye hasira na visasi vyao,sambamba na wale wanaotaka kutumia fursa hiyo kujitajirisha?Huo ndio mwanzo wa fisadi kumfisadi fisadi mwenzie.

  Ikumbukwe pia kwamba 2005 kulikuwa na mtandao wa aina moja na wenye lengo moja tu.Sote tunafahamu namna mtandao huo ulivyozaa matawi mbalimbali including kuibuka kwa watu kama Samuel Sitta ambaye kwa namna flani amewageuka wanamtandao waliomweka madarakani.Kwa ujumla nguvu za mtandao wa 2005 ni pungufu kuliko ilivyokuwa awali.Na hapo kuna suala la kuamininia.Je watakaokabidhiwa majukumu ya kukwapua fedha za umma kufanikisha kampeni hawawezi kuwasiliana na akina Kubenea,if not Dokta SLAA mwenyewe?Je watalishana yamini kabla ya kuiba fedha hizo?Lakini je muda unatosha kufanya oparesheni kubwa kiasi hicho?Ndio maana yayumkinika kusema CCM wameshtukizwa sana na uteuzi wa Slaa.Time is essence katika wizi mkubwa kwa vile kunakuwa na haja ya ku-cover tracks na wizi kuwa foolproof.Katika mazingira ya sasa wanafahamu kuwa wanaweza kuiba kisha wakashinda lakini nyaraka za wizi wao zikatumika kutengua matokeo ya uchaguzi.Remember,mpinzani wa Kikwete ni Dkt SLAA,and that speaks volumes.

  Nimalizie kwa mambo mawili.KWANZA,naamini kuna watu kadhaa ndani ya CCM ambao kwa hakika wamechoshwa na utawala wa JK lakini hawakuwa na jinsi ya kumdhibiti asigombee mara ya pili.Hawa ni pamoja na wale ambao have got nothing to lose JK au CCM ikishindwa.Hapa tunaweza kuwakuta watu kama akina Salim,Warioba,Butiku, hata Sumaye,nk.Hawa wanaweza kuendelea kubaki CCM na kuwa assets muhimu kwa Chadema kwa kufanya "legal sabotage" including kupenyeza taarifa za wizi wa fedha za umma kwa minajili ya kufanikisha ushindi wa CCM.Pia katika kundi hili wanaweza kuwepo watakaobwagwa kwenye kura za maoni lakini wasihame chama hicho kisha wakaishia kumalizia hasira zao kwa kuisapoti CHadema wakiwa ndani ya CCM.

  Lakini kubwa zaidi ni ukweli kwamba wasifu wa Dkt SLAA unajiuza wenyewe (japo haimaanishi kuzembea katika kampeni).Watanzania wengi wanaelewa kuwa mwanasiasa huyu anauchukia ufisadi kwa dhati,na kwa hakika akipewa nafasi ya kuongoza nchi yetu anaweza kubadilisha mwenendo wa taifa letu in a posotive way.Ni dhahiri kuwa Slaa atakuwa na mabomu mengine mazito yatakayotumika kuwanyong'onyeza CCM wakati wa kampeni.Na tofauti na ilivyokuwa wakati Slaa akilipua mabomu hayo bungeni,this time CCM watakuwa na muda mchache wa kujibu kila shambulizi (kama wana cha kujibu at all) kwa vile watapaswa kuwa busy na "kuuza sera zao" kwa wapiga kura.Sasa kama watatumia muda wote "kujibu mapigo" ni dhahiri watajikuta waki-run out of time pasipo "kuendeleza ahadi zao waliazoanzisha 2005".

  Well,pengine naota tu,lakini hata ndoto hutimia.Nia ipo,sababu zipo,na uwezo upo.Kilichobaki ni kwa kila mwenye uchungu wa dhati wa nchi yetu kumuunga mkono Dkt Slaa ili atuwezesha kuuzika ufisadi.Hakuna cha "if" au "but",let's make it "a MUST".Kama tuliweza kumwondoa mkoloni na nyenzo zetu hafifu kabisa,na tukamtandika nduli Idi Amin,basi tunaweza kabisa kuuangamiza ufisadi kwa kuion'goa CCM hapo Oktoba.

  Inawezeka iwapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.
   
 2. Kiby

  Kiby JF-Expert Member

  #2
  Aug 12, 2010
  Joined: Nov 16, 2009
  Messages: 5,209
  Likes Received: 1,010
  Trophy Points: 280
  Mimi kwa sasa nimfuasi na muumini wa kuingoa ccm kirahisi kuliko kiugumu.
   
Loading...