Ugomvi mwengine; masha na mweka hazina ccm | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ugomvi mwengine; masha na mweka hazina ccm

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ngekewa, Apr 5, 2009.

 1. N

  Ngekewa JF-Expert Member

  #1
  Apr 5, 2009
  Joined: Jul 8, 2008
  Messages: 7,730
  Likes Received: 23
  Trophy Points: 135
  Waziri Masha, Mweka Hazina Mansor washtakiana CCM

  Na Frederick Katulanda, Mwanza


  UGOMVI wa kugombea majimbo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa umehamia katika Mkoa wa Mwanza baada ya Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha na Mweka Hazina wa chama hicho mkoani humo, Shanif Mansoor , kufikishana kwa katibu wa mkoa.


  Habari zilizopatikana ndani ya CCM zinasema kuwa, Waziri Masha amefikisha malalamiko kwa katibu huyo wa CCM akilalamikia ziara ya Mweka hazina wa CCM kuimarisha matawi ya chama hicho, akidai kuwa zina lengo la kumuimarisha kisiasa ili agombee ubunge wa jimbo hilo mwakani.


  Imeelezwa kuwa Mweka hazina huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mansoor Oil Ltd, tayari ameanza ziara ya kuimarisha chama kwenye kata za jimbo hilo na kuzungumza na mabalozi wa shina wa chama, jambo ambalo limeonekana kumtia hofu Masha.


  Mansoor katika ziara yake hiyo, amekuwa akizungumza na mabalozi hao na kuwahimiza kuingiza wanachama wengi na kwamba katika kila kata amekuwa akimwaga kadi za chama na kudaiwa kutoa posho ya Sh 10,000 kwa mabalozi hao.


  “Hii ni kampeni unadhani kuna kiongozi anaweza kufanya ziara akatoa fedha zake mfukoni kuwalipa posho wajumbe kama hana faida nazo. Angalia anatoa posho kwa kila mjumbe, huku siyo kukiimarisha chama ni kujiimarisha yeye ana mpango wa kugombea,” alieleza mmoja wa viongozi katika kata ya wilaya ya Nyamagana ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini.


  Katibu wa CCM mkoani Mwanza, Kundya Rajabu alipoulizwa kuhusiana na jambo hilo alisema amekwisha pokea malalamiko kutoka kwa Mbunge wa Nyamagana Lawrence Masha ambaye alimweleza kuwa amepata taarifa za Mansoor kufanya kampeni za kuwania ubunge katika jimbo hilo .


  Kundya alisema, kutokana na taarifa hizo aliamua kumwita na kumuuliza Mweka hazina wake, lakini alimjibu kuwa hana dhamira ya kugombea kutokana na kutekeleza kauli ya Rais kuwa wanapaswa kutenganisha biashara na siasa.


  “Binafsi niliamua kumuuliza Mweka hazina kama atagombea akanijibu hapana, familia yake haijamruhusu na kwamba anatekeleza agizo la Rais Kikwete la kutenganisha biashara na siasa na kama kugombea aliwahi kufikiria kugombea Jimbo la Kwimba la Bujiku Sakila, lakini mkewe alimkataza” alieleza Kundya huku akimnukuu.


  Alisema malalamiko yanayotolewa dhidi yake ni mengi ikiwa ni pamoja na ziara ya sasa ambayo anaifanya katika kata kwa faida na maslai ya chama kwa vile amekuwa akihimiza kata kuongeza wanachama.


  “Ziara hii ya Mweka hazina ni kweli ni ya kuimarisha chama, hajaifanya Nyamagana peke yake, amefanya hata Magu na Kwimba, lengo ni kuinua uhai wa ofisi za chama katika kata zote ili zijenge utamduni wa kuingiza wanachama na kuuza kadi za chama, akifika hapo anatoa kadi za kianzio na anawaeleza kuwa zikiisha wanapaswa kurejesha fedha zake na kununua nyingine tena,” alifafanua zaidi Kundya.


  Kundya alisema ingawa kugombea ni haki ya msingi ya kila mwanachama, lakini kulingana na maelezo aliyopewa na Mweka hazina wake anaamini kuwa, kweli hana nia ya kugombea ubunge.


  Hata hivyo, Mansoor alipopigiwa simu yake ya mkononi jana alimtaka mwandishi wa habari hii kumwandikia maswali anayotaka kuuliza na kupeleka ofisini kwake.


  “Nilikwisha sema waandishi wanaotaka kunihoji waandike maswali yao waniletee, siwezi kujibu kwenye simu maswali yako andika kwa maandishi uniletee” alieleza na kukata simu.


  Baada ya kufika ofisini kwake na maswali hayo mwandishi wetu alijibiwa kuwa mkurugenzi huyo yuko safari.


  Naye Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha amekiri kuitambua ziara ya Mweka hazina huyo katika jimbo hilo, lakini akakanusha madai kuwa ameilalamikia kwa katibu mkuu.


  "Mimi sina mgogoro na Mweka hazina, labda mgogoro huo muutengeneze nyie waandishi. Ninachojua anafanya ziara na mwenyekiti wa mkoa ya ujenzi wa chama. Sijawaji kuilalamikia ziara hiyo wala kufika kwa Kundya," alisema.


  Tayari CCM taifa imesuluhisha ugomvi wa makada wawili wa chama hicho wa kugombea jimbo kati ya Mweka hazina wa CCM Taifa, Amos Makala na Sadiq Murad mbunge wa Mvomero mkoani Morogoro.


  Pia hivi sasa baadhi ya wanachama wa chama hicho wapo katika malumbano makali ya kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali mikoani.
   
 2. Abdulhalim

  Abdulhalim JF-Expert Member

  #2
  Apr 5, 2009
  Joined: Jul 20, 2007
  Messages: 16,472
  Likes Received: 126
  Trophy Points: 160
  Ningekuwa na nafasi, kitu cha kwanza ningelikifanya ni kufuta vyama vyote vya siasa. Vyama vya siasa vimekuwa chanzo cha kila aina ya upupu na umasikini wa nchi hii.. Hebu tazama hawa mabalah..
   
 3. G

  Gozigumu JF-Expert Member

  #3
  Apr 5, 2009
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 254
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Hili suala la kutenganisha siasa na wafanyabiashara litawagusa pia wale wenye Makampuni? Au biashara lazima iwe kwa Bidhaa tu? Kama biashara ni mtaji wa kujinufaisha kwa fedha nashindwa kuona atakaekuwa na sifa katika safu ya Wabunge wa hivi sasa.
   
Loading...