WIZARA ya Maji na Umwagiliaji imekumbwa na kashfa kubwa baada ya ukaguzi maalumu uliofanywa kwenye miradi ya maji nchi nzima kubaini tuhuma za ufisadi, uzembe wa maofisa na matumizi mabaya ya mabilioni ya shilingi kwenye wizara hiyo.
Ukaguzi maalumu (special audit) uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye programu ya maendeleo ya sekta ya maji (2007-2010) umebaini malipo mengi ya utata kwenye miradi ya maji nchini na matumizi mabaya ya pesa za umma.
Katika moja ya tuhuma hizo za ufisadi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji imebainika kutumia zaidi ya dola za Marekani milioni 39 (takribani shilingi bilioni 63) kwenye mazingira ya utata bila kuzingatia miradi iliyopo kwenye mpango kazi wa mwaka wa wizara hiyo.
"Shughuli za manunuzi ndani ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji hazifanywi kuendana na mpango wa manunuzi wa kila mwaka," imesema sehemu hiyo ya ripoti mpya ya CAG kutokana na ukaguzi uliofanywa Septemba mwaka jana.