TCRA watupa suala hilo kwa polisi.Wewe ni kiongozi wa kundi la mtandao wa WhatsApp? kama jibu ni ndiyo basi soma kwa makini kinachoweza kutokea namba yako ikidukuliwa.
Umeibuka uhalifu mpya ambao mtu mwenye nia ovu hudukua namba ya simu na kuitumia kwenye WhatsApp, ilhali simu ikiwa mikononi mwa mhusika.
Licha ya mdukuzi kutumia namba hiyo kuwasiliana na watu na kufanya vitendo vya utapeli, anaweza kuingia kwenye makundi ya WhatsApp na kufanya anayotaka hasa mwenye siku iliyodukuliwa akiwa kiongozi wa kundi (admin).
Mfano wa hilo umetokea juzi baada ya zaidi ya makundi sita kuvamiwa baada ya mmoja wa ma-admin, kudukuliwa namba yake. Iwapo kundi lina ma-admin wengine, mdukuzi anachofanya kwanza ni kuwaondoa wote na kubaki pekee ili afanye anachotaka.
Mdukuzi huyo akiwa ndiye kiongozi wa kundi ana uwezo wa kuwatumia watu ujumbe akiwaelekeza watume fedha kwa namba nyingine, kwa kile anachodai amepata dharura.
Miongoni mwa walioathiriwa na uhalifu huo ni mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe, Salome Kitomari ambaye pia ni admin wa makundi kadhaa baada ya namba yake ya simu kudukuliwa na mtu ambaye hamfahamu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kitomari alisema mhalifu huyo amekusanya Sh630,000 kutoka kwa watu watatu tofauti ambao alikuwa akiwatumia ujumbe akijifanya ni Kitomari.
Alisema baada ya kugundua hilo alikwenda ofisi za kampuni ya simu ambayo amesajili laini yake, lakini hakupata msaada kwa wakati kutokana na mdukuzi kuweka namba ya siri.
Msemaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala alipoulizwa kuhusu udukuzi huo alijibu: “Hilo ni suala la polisi wale wana kitengo cha cyber crime hao ndiyo tunashirikiana nao. Kudukua namba ya mtu kwa matumizi yoyote ni kosa la jinai na watu wanapobainika wanakamatwa.”
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz alipopigiwa simu yake ya mkononi baada ya mwandishi wa habari kujitambulisha simu ilikatwa
Chanzo: Mwananchi