DOKEZO Uchunguzi: 'Makanisa ya Kiroho' na shuhuda FEKI kuwahadaa Watanzania - 2

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'
A

Anonymous

Guest
Andiko hili ni mwendelezo wa kilichoandikwa katika Makala iliyopita ambayo ilielezea yanayofanyika nyuma ya pazia kwenye nyumba za ibada hasa katika makanisa maarufu kwa jina la 'Makanisa ya Kisasa' Nchini Tanzania.

Zaidi andiko lilielezea mbinu na shuhuda za uongo (feki/za mchongo) zinazofanyika ili kuwavuta watu kwa lengo la kujipatia fedha kwa mgongo wa sadaka.

Ni vema kama hukusoma andiko hilo, pitia hapa ili kupata uelewa mzuri wa mwendelezo huu wa sehemu ya pili >> Uchunguzi: 'Makanisa ya Kiroho' na shuhuda FEKI kuwahadaa watanzania

Chachu ya uchunguzi huu ni matukio mfululizo yasiyoelezeka yanayotokea Tanzania na Nchi jirani ikiwemo Kenya, ambapo watu wengi wanajua kilichotokea, mamia ya watu wamepoteza maisha.

Kwa Tanzania moja ya kumbukumbu ya kushangaza ni ile ya Wilayani Kakonko Mkoa wa Kigoma Mwaka 2014, ambapo kuna Waumini walikatazwa kuwapeleka Watoto shule kutokana na imani walizodai ni dhambi kujifunza elimu Dunia.

Kuna lile la Babu wa Loliondo ambalo watu waliacha dawa za hospitali kwenda kwa Babu huyo japo hiyo haikuwa na uhusiano na Kanisa moja kwa moja.

Mwanza pia kuna Mchungaji alidaiwa kuwafungia ndani waumini kwa sababu za kiimani, hali iliyopelekea kuathiri hali za kiafya za waumini waliokumbwa na mkasa huo.

Uchunguzi uliofanyika unaonesha kama hatua hazitachukuliwa mapema kuna mazingira hatari zaidi kujitokeza siku za usoni kwa kigezo cha imani ya Dini hasa hizo ambazo ni ‘huduma za upako’.

Hivyo, lengo la makala au andiko hili sio kukosoa imani au makanisa, bali inajulikana wapo ambao kweli wanamtukuza Mungu lakini pia wapo wanaotumia mwamvuli wa Kanisa kufanya mambo mengi mabaya na yanayotishia afya, maadili na mtazamo wa jamii, pia ni kuiamsha Serikali kuwa makini na kinachoendelea nyuma ya pazia.

Michezo ya Hospitali kudanganya

Aidha, kuna viashiria vya baadhi ya hospitali na vituo vya Afya hasa binafsi, kutumika vibaya kutoa matokeo ya uongo ya vipimo vya Afya kwa wacheza “Shaba” (watoa shuhuda za uongo), ili yatumike katika makanisa kama shuhuda za uongo ikiwa lengo ni kuwaadaa waumini wengine kuwa huduma zao zimewawezesha kupona.

Baadhi ya vyeti feki vya vipimo ni vile vinavyoonesha wahusika wamepona magonjwa kama Saratani, UKIMWI, Kisukari na hata presha.

Michezo hiyo imekuwa ikifanywa hasa katika taasisi kubwa za Afya, moja ya mifano hai zinapatikana Dar es Salaam na Kilimanjaro. Majina hayatatajwa hapa kwa sababu maalum.

Pia wapo wanaoshawishiwa kwenda hospitali wakiambiwa changamoto zao za afya zinatokana na imani za kishirikina, hivyo hawaendi kupata tiba inayotakiwa wakiamini maombi pekee ya mchungaji au mitume yatawasaidia.

Kula/kunywa vitu hatarishi kiafya

Kuna baadhi ya waumini wanakunywa mafuta yanayodaiwa kuwa ya ‘upako’ bila kujua ubora wa kimiminika husika kiafya au kinakuwa katika mazingira gari.

Ni afadhali wale wanaotoa maji masafi kwa Waumini wao, lakini kunywa mafuta inaweza kusababisha changamoto kiafya kama hayapo kwenye mazingira safi.

Makongamano/Mikusanyiko kukosa utaratibu

Kuna waumini wengi wamekuwa wakikusanyika sehemu zenye mazingira hatarishi mfano ni tukio la watu kupoteza maisha Mkoani Kilimanjaro wakati wa kukanyaga mafuta katika kongamano, Serikali ilichukulia ‘poa’, inawezekana hofu ilikuwa ni kuingilia imani.

Lakini kuna umuhimu wa kuwa na utaratibu maalum wa kuratibu mikusanyiko kwani kunapotokea magonjwa ya maambukizi ni rahisi kusambaa, mbali na hapo kutokuwa na utaratibu wa kujipanga ni rahisi kutokea mkanyagano kama ilivyotokea Kilimanjaro.

Kufunga kula mfululizo

Baadhi ya waumini wanatengenezewa mazingira ya kuamini kufunga kula mfululizo ni sehemu ya ibada, wanafanya hivyo bila kuzingatia uhalisia wa hali za afya zao japo hii ni kwa baadhi ya nyumba za ibada.

Kutelekeza familia kisa maombi

Baadhi ya waumini wanatumia muda mwingi kwenye nyumba au maeneo ya ibada kutafuta huduma mbalimbali, wakiacha familia zao hasa Watoto wakiwa katika hali ya uhitaji wa huduma muhimu wakati wao wanawasikiliza kila wanachoambiwa na viongozi wao wa dini.

Hiyo inachangiwa pia na tabia ya baadhi ya watoa mahubiri kuwalemaza waumini katika juhudi za utafutaji wa kujikomboa kiuchumi.

Utitiri wa michango ya fedha

Uwepo wa michango mingi ambayo waumini au wafuasi wanatakiwa kuitoa unaweza kuchangia kupunguza nguvu ya uzalishaji kwa kuwa watu wanapeleka fedha nyingi huko na kusahau kufanya uwekezaji wao binafsi.

Ndio maana ni kawaida kukuta viongozi wa waumini wakiwa na maisha mazuri na ya kifahari wakati Waumini au wafuasi wao wakiwa ni wale wenye maisha duni, lakini bado wanaaminishwa kumchangia kiongozi wa dini awe na maisha mazuri ndio ibada yenyewe.

Ndoa au familia hatarini kuvunjika

Hii ni kutokana na Wanafamilia hasa Wanawake kutumia muda mwingi sehemu za ibada huku baadhi ya Wanandoa wakilalamika wenza wao kuelekea nguvu ibadani na kusahau majukumu yao ya kila siku kwenye ndoa zao.

Migogoro ya ardhi

Ni vitu vya kawaida kutokea na wengi wao hawafikishi malalamiko kwenye mamlaka za Kiserikali badala yake wanaamini katika maombi kuwa kila kitu kitakaa sawa.

Shuhuda mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa anaelezea "Nilitapeliwa eneo na Shemeji zangu baada ya Mume wangu kufariki nimekuja hapa Dar es salaam kutokea Dodoma nione kama nitapata msaada wenzangu waliniambia nije nichukue maji kwa kuhani ili nikaikomboe hiyo ardhi yangu.

"Sijaenda Mahakamani maana wale Shemeji zangu wana hela ya kuwawezesha kufanya chochote wanavyotaka, nina ndugu yangu yupo Dar aliniambia nije leo (siku aliyosimulia mkasa wake) kwenye Kongamano na udongo kutoka kwenye ardhi niliyoporwa nichukue na maji ya baraka nikamwagilie eneo lile ardhi yangu itarejea kwenye umiliki wangu."

Hivyo, tahadhari isipochukuliwa kwenye baadhi ya nyumba za Ibada kuna hatari zaidi zinaweza kutokea, iwe ni kwa kuwa na jamii yenye mtazamo ya kipekee au kuibuka kwa matukio ya ajabu zaidi au kuwa na kizazi kinachoamini maombi pekee ndio yatawaokoa bila kufanya kazi au kufanya uwekezaji.

Itaendelea sehemu ya 3...
 
ngoja tungoje hadi mwisho kuona nani ataangushiwa jumba bovu
 
Kama huamin baki na imani yako..waache wanaoamin waendelee kuamini....uwa sielew kwann tunalazimisha usichokiamin wewe na wengine wasikiamini na unataka waamini chako....kuna watu wanapona/walipona na kuna watu hawaponi/hawakupona.
 
Haya makanisa yanatutoa stress, unaenda unalia weeee baada ya hapo umetua mzigo mzito. Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.
Kuongea uongo ni hulka ya mtu binafsi. Mbona kuna taahira huko jeshini kasema JWTZ ni jeshi la sita kwa ubora duniani. Hiyo ⁹ ni kauli ya mtu na si ya jeshi.

Ndivyo ilivyo na makanisani
 
Haya makanisa yanatutoa stress, unaenda unalia weeee baada ya hapo umetua mzigo mzito. Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.
Kuongea uongo ni hulka ya mtu binafsi. Mbona kuna taahira huko jeshini kasema JWTZ ni jeshi la sita kwa ubora duniani. Hiyo ⁹ ni kauli ya mtu na si ya jeshi.

Ndivyo ilivyo na makanisani
Nakazia. "Taahira."
 
Back
Top Bottom