Mgogoro wa ACT sasa
watinga mahakamani
 Posted by: Saed Kubenea
 2 days ago  0 Comments
 300 Views
HATIMAYE yametimia. Alliance for Change
and Transparency (ACT-Tanzania), chama
kipya cha siasa nchini na ambacho
kilitarajiwa kuongozwa na Zitto Zuberi
Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini,
kimemfungulia kesi Samson Mwigamba na
genge lake. Anaandika Saed Kubenea.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama
Kuu, Kanda ya Dar es Salaam na
Lucas Kadavi Limbu, mmoja wa
waasisi na mwenyekiti wa taifa wa
chama hicho na wenzake watano.
Viongozi wengine wa ACT walioungana na
Limbu kumfungulia kesi Mwigamba,
aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho
na ambaye amefukuzwa uwanachama, ni
Leopald Mahona, naibu katibu mkuu
(Bara) na Grason Nyakarungu, katibu
mwenezi na mwenyekiti wa vijana taifa.
Wengine walifungua kesi hiyo, ni
Ramadhani Suleiman, makamu
mwenyekiti (Zanzibar) na mwenyekiti wa
ngome ya wanawake, Dotto Chacha
Wangwe. Kesi hiyo ni Na. 1 ya mwaka
2015.
Katika hati ya kiapo kilichowasilishwa
mahakamani, Limbu, Nyakarungu,
Mahona, Ramadhani na Wangwe, wanadai
kuwa Mwigamba na Prof. Kitila, mshauri
mkuu wa chama hicho, wamefanya
mapinduzi ndani ya chama kinyume na
katiba ya ACT.
Prof. Kitila aliyekuwa mjumbe wa Kamati
Kuu (CC), ndani ya Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), alifukuzwa
uanachama mwaka mmoja uliopita; ndipo
akajiunga na ACT-Tanzania.
Alituhumiwa kushiriki njama za kuhujumu
chama na kuandaa mipango isiyo halali ya
kubadilisha uongozi Chadema. Alikiri
kushiriki njama.
Katika ACT, Prof. Kitila anakabiliwa na
tuhuma zilezile. Naye Mwigamba ambaye
alikuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa
wa Arusha, alifukuzwa kwa madai ya
kuhujumu chama, usaliti, kukashifu
viongozi wakuu wa chama na
uchonganishi.
Katika chama kipya sasa, Mwigamba na
Prof. Kitila wanatuhumiwa makosa
yaleyale na hasa kile kinachoitwa kutaka
kuleta mapinduzi ili Zitto Kabwe, ambaye
pia alifukuzwa Chadema, aweze kuwa
mwenyekiti wa ACT-Tanzania.