Uchaguzi kwanza au Kilimo Kwanza? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uchaguzi kwanza au Kilimo Kwanza?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by kasyabone tall, Sep 21, 2009.

 1. k

  kasyabone tall JF-Expert Member

  #1
  Sep 21, 2009
  Joined: Sep 13, 2009
  Messages: 255
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 33
  MIOYO ya Watanzania wengi sasa imeanza kuwa juujuu hasa kutokana na pilikapilika zisizo za kipimo kuanza kwa kasi ya ajabu na kuwafanya watu wenye nia ya kutafuta kile wanachokitaka waanze kujipitisha kwenye kila kona ya nchi ili kupata ridhaa ya wananchi.
  Wapo wanaojipitisha kwa madai kuwa wameitwa na wazee, wapo walioahidiwa na wenye pesa kujipeleka huko na wapo wenye utashi binafsi wanaolilia uzalendo wa nchi yao kuwapigania makabwela wenzao nao wamo.
  Wakati watu wakiwa kwenye pilika pilika hizo ukiangalia juu angani utaona jinsi mawingu yalivyoanza kutanda, sehemu nyingine kukiwa na manyunyu ya mvua yanayoashiria kuanza kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2009/2010.
  Mambo haya mawili ndiyo yaliyonifanya niweke wazi ni kauli mbiu ipi inaweza kutekelezwa kwa haraka katika kipindi hiki, uchaguzi kwanza au Kilimo Kwanza; ni kauli mbiu ipi kwa hesabu za harakaharaka inaweza kupata ushindi dhidi ya nyingine.
  Kwa urahisi wa majibu naweza kuungana na wale watakaojipanga na kuthubutu kusema bila woga kuwa kauli mbiu inayofaa kwa wakati huu tukielekea mwaka 2010 ni uchaguzi kwanza, kilimo baadaye.
  Hakuna ubishi hapo kuwa uchaguzi ndiyo umeteka mawazo ya Watanzania wengi hivi sasa kwa kuwa hata nguvu zao wamezielekeza kwenye mikakati ya kuwapata viongozi wapya kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwa ni maandalizi tosha ya kuanza mchakato wa uchaguzi mkuu mwakani.
  Wanasiasa hivi sasa lugha kuu wanayoizungumza ni mipangi na mbinu za kuhakikisha vyama vyao vinapata idadi kubwa ya viongozi kuanzia ngazi za mitaa na hawafikirii kuimba wimbo wa kilimo kwanza.
  Wabunge waliopo madarakani wenye ‘Presha za kupanda na Kushuka’ wanajua fika kuwa muda wao wa kuwaongoza wananchi katika kipindi cha miaka mitano waliyoahidi kuwatumikia ndio inaelekea ukingoni, jua linakwenda machweo.
  Huwezi kunishawishi kuwa hivi sasa wabunge hawa wataacha kuwapigia kelele wenzao wanaonyemelea majimbo wanayoyashikilia ukawashawishi waimbe wimbo wa kilimo kwanza, kamwe hawawezi, wataulizwa na wapiga kura wao muda wote walikuwa wapi kusema kilimo kwanza?
  Ni wazi kazi kubwa na yenye kipaumbele na ambayo imepewa msukumo wa kwanza ni suala la uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani hiyo ndiyo kauli mbiu halisi na inayoweza kutekelezeka kwa urahisi kwa kuwa imo ndani ya mfumo wa kiutawala na itafanikiwa.
  Kauli mbiu ya kilimo kwanza naiona imekaa kisiasa zaidi na imekuja wakati ambao si wake nikiamini fika kuwa wanaoweza kutekeleza mageuzi ya kilimo ni wakulima wenyewe na hao hao ndio tulionao tangu nchi hii ilipopata uhuru, hayajawahi kutokea maajabu yoyote.
  Ikumbukwe kwamba kabla ya kauli mbiu hiyo kulikuwa na kauli mbiu ya Iringa, Siasa ni Kilimo ambayo kwa kiasi kikubwa iliweza kuonyesha mafanikio makubwa enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wananchi waliweza kutambua umuhimu wa kauli mbiu hiyo.
  Kwa msisitizo ndipo ulipofikia wakati wa kuwa na kiwanda cha mbolea cha Tanga kilichoweza kufanikisha kuinua kilimo na kuifanya baadhi ya mikoa minne ya nyanda za juu Kusini Magharibi, Rukwa, Mbeya, Iringa na Ruvuma iwike kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula; kufa kwa kiwanda hicho na kilimo kimekufa.
  Sasa kilimo kimegeuka kuwa kwenye midomo ya wanasiasa, kikiwaacha watalamu mahsusi waliosomea kazi hiyo ambao nao hawaonekani vijijini bali mijini kama washauri kwenye sekretarieti za wilaya na mikoa hawana jipya.
  Wataalamu wa kilimo waliokuwa wanategemewa kuimba kauli mbiu ya ‘Siasa ni kilimo’ nao wamegeuka wanasiasa, wameona kilimo hakilipi bora waingie bungeni wakabanane humohumo; ni madaktari na maprofesa, wameona hakuna kilimo kinachoweza kufanyika kwenye nchi isiyowajali wakulima.
  Hawa waligundua muda mrefu kuwa mkulima hakopesheki, hathaminiwi wala kuaminika benki au taasisi za fedha hawezi kuwa na dhamana yoyote isipokuwa siku zote Waswahili wamekuwa wakiimba “mkulima lake jembe” tena jembe la mkono, si trekta ndogo (Power tiller) au matrekta makubwa.
  Ni mkulima gani huyo anayeweza kulima kwa kutumia tekta ndogo na kumudu kununua lita moja ya mafuta ya dizeli kwa Sh 1,500 hadi 1800 huko vijijini? Ni mkulima wa aina gani huyo anayeongelewa hapa leo na wanasiasa anayeweza kushawishiwa aamini kuwa kilimo kinaweza kupewa umuhimu wa kwanza?
  Ni mwanasiasa yupi leo anayeweza kuingia kwa wapiga kura wake huku akiwa amewasambazia mkopo wa matrekta madogo huku akijua fika kuwa wananchi hao hawana uwezo wa kununua mafuta, vipuri au kumudu gharama za uendeshaji pale inapotokea hitilafu kwenye vimashine hivyo.
  Mkulima huyu anayekwama kununua mbolea ya ruzuku kwa bei inayouzwa huku akipewa habari kuwa fedha za malipo ya madeni ya nje (EPA) zilizorejeshwa na wezi, zitawanufaisha wakulima ili kuwapunguzia mzigo wa kulima, fedha hizo zipo wapi?
  Sioni na sifikirii kama kuna mwanasiasa yeyote hivi sasa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/2010 kama anaweza kusimama akawaambia wapiga kura wake waache uchaguzi kwanza na wageuzie mawazo yao kwenye kilimo kisichokuwa na miundombinu yoyote, hakuna umwagiliaji, hakuna mbolea ya kutosha, hakuna dawa za kutosha na zenye bei juu na hawana uwezo wa kununua trekta ndogo na kumudu gharama za kuendesha.
  Wazo la kukipa kipaumbele kilimo halikuanza jana wala leo, nimesema ni mapambano ya muda mrefu ambayo angalau, Baba wa Taifa alithubutu kuwaunganisha wananchi katika zoezi la operesheni Vijiji vya Ujamaa, kilimo cha bega kwa bega ndicho kilichowafanya hata wale wavivu wa kulima kujifunza kulima.
  Sasa hivi hakuna msukumo wowote unaowafanya wananchi walime kwa nguvu ndio maana wengi wanakimbia kilimo na wanajiingiza kwenye kazi nyingine kama siasa, wamachinga, mama ntilie (mama lishe), wafanyabiashara wa kati na wakubwa na wengine wasiokuwa na ajira rasmi hao ndio wengi.
  Mazingira hayo yote yanaonyesha mashaka kuwa lazima kauli mbiu hizo zitagongana, japokuwa moja inaonyesha kuwa rasmi lakini inaweza kumezwa na nyingine ya Uchaguzi Kwanza na Kilimo Kwanza ikaja baadaye hapo ndipo panapohitaji ushawishi wa mtu katika kuzitofautisha kauli hizo mbili na kila moja ina faida na madhara yake na kwa wahusika.
  Ili kila kauli iweze kutimia wakulima hawapaswi kutumiwa kama kichaka cha wanasiasa kuweza kutekeleza malengo yao, amueni kama kilimo kwanza, mvua zinakuja na chaguzi zinakuja kipi kiwe kipi, na nini kianze?
   
 2. e

  echonza Senior Member

  #2
  Sep 21, 2009
  Joined: Jun 25, 2009
  Messages: 163
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Kimsingi masuala yote mawili ni muhimu katika ustawi wa watanzania wote. Katika uchaguzi ndipo tunaweza kupata viongozi bora watakaoongoza wananchi katika Sera yeyote itakayotengenezwa na Serikali husika. Kilimo kwanza nacho vivyo hivyo ni muhimu kuleta mabadiliko ya uchumi kwa wa-Tanzania walio wengi (wakulima) kama itatekelezwa vizuri.
  Hata hivyo, wasiwasi wangu ni kwamba "Kilimo Kwanza" sina uhakika kama ni Sera iliyotengenezwa kupitia misingi yote ya kutengeneza Sera yeyote ile. Kwamba, faida na hasara za utekelezaji wake zimefanyiwa uchambuzi wa kina na hatimaye kufikia uamuzi ambao faida ya utekelezaji lazima iwe kubwa kuliko hasara zake. Pia wasiwasi wangu ni kwamba je, uchambuzi huo ulizingatia wataalamu tulio nao nchini katika sekta zote ndani ya sekta ya kilimo kwamba tumewaweka tayari kushiriki kikamilifu kutekeleza hicho kinachoitwa "Kilimo Kwanza". Kwa mfano, wataalamu kama Maafisa Ughani, Wahandisi wa Kilimo, Wachumi wa Kilimo, Wakulima wenyewe (katika makundi mawili-wazalishaji wakubwa na wazalishaji wadogo), wafanyabiashara wanaoweza kuwekeza katika sekta ya kilimo kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ili kuyaongezea thamani kabla hayajauzwa kwa watumiaji kwa bei yenye faida zaidi na wataalamu wengine zaidi.

  Sielewi kama kuna maandalizi ya kutosha katika kuhakikisha wakulima wetu wanapata pembejeo za kilimo kwa wakati unaofaa na pia sina uhakika kama wakulima watawezeshwa kwa kupewa mikopo yenye masharti nafuu na kuwawezesha kuzalisha mazao yao kwa gharama ndogo zaidi.
  Baada ya hayo napenda tu kusema kwamba, kwa mazingira yaliyopelekea "Kilimo Kwanza" kutangaza rasmi kama mpango wa kuboresha uzalishaji wa mazao kwa wingi zaidi, sikuona nyuma yake kama kulikuwa na michakato yeyote ya kuchambua masuala mbalimbali ya kisekta kabla ya kufikia uamuzi uliofikiwa. Ninauhakika kwa asilimia zaidi ya 60 kwamba utekelezaji wake utakwama kwa vile "Kilimo Kwanza" siyo kauli mbiu iliyoletwa kama matokeo ya uchambuzi wa kitaalamu kwa kutumia wataalamu wetu kutoka Ofisi zetu za Umma na Taasisi za Kilimo kama (SUA, na vyuo vingine vya utafiti wa Kilimo). Mara nyingi Serikali yetu imekuwa ikiibua miradi au Sera fulani pasipo kuangalia matokeo ya Tafiti mbalimbali kuhusiana na suala husika. Na matokeo yake hakika ni kutumia fedha za Umma katika kutekeleza kitu kisicho na majibu mwafaka kubadilisha maisha ya wananchi. Huishia kupata hasara tu!

  Natumia fursa hii kuiomba Serikali yetu (Tanzania) ibadilike na kuvipa nafasi vyuo vikuu tulivyonavyo nchini katika kutupa majibu ya wasiwasi au maswali ya kutatua tatizo fulani. Naweza kuandika sana kuelezea suala hili la kilimo na mfumo wa utendaji ndani ya nchi yetu na nikachosha wasomaji wa hatimaye kutofikisha ujumbe. Wataalamu tupo lakini Serikali bado inatumia mbinu za miaka ya 47 zisizozingatia ushauri wa kitaalamu kwa kuwabeza wasomi (vijana) kwamba ni Voda Faster. Hebu Serikali yetu ipate mifano kutoka nchi jirani kama Rwanda ambao hakika baada ya kuona kuwa walikuwa na matatizo mengi kutokana na "Mauaji ya Halaiki". Serikali kupitia ushauri wa kitaalamu imewekeza katika TEKNOHAMA kuwa uti wa mgogongo wa uchumi wa nchi. Wamepeleka vijana kusoma katika sehemu mbalimbali za dunia. Vijana wamepewa nafasi za kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Taaluma zao na tunaona jinsi Rwanda sasa hivi inavyokuja kasi hata wamekuwa washindani wetu katika masuala mbalimbali ya kiuchumi ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

  Hakuna nchi inayoweza kuendelea bila ya kutumia wataalamu walionao, na badala yake watu kujali maslahi binafsi kama kwa mfano, mimi kama afisa ndani ya Wizara fulani kushauri Utawala na wakakubaliana na nilichowasilisha ni vigumu sana maana unakuta wazee wanao ugonjwa wa kuita wewe kijana mdogo nawe utasema nini!!!

  Hata hivyo, naamini tukipata uongozi bora ngazi zote hakika Tanzania inao wataalamu wanaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa watu wao. Mfano mzuri ni jinsi watanzania hao hao wanavyoleta mafanikio katika nchi zingine wanakofanyia kazi nje ya Tanzania (km vile Botswana na kwingineko duniani).
   
Loading...