KAMPENI za kugombea nafasi ya urais katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), sehemu ya Mlimani zimetawaliwa na itikadi za vyama vya siasa pamoja na uzawa.
Hali hiyo ilishuhudiwa na Tanzania Daima jana, ilipotembelea chuoni hapo katika siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi huo unaofanyika leo, na kuelezwa kuwa baadhi ya wagombea wamegeuka kuwa kama mawakala wa vyama vya siasa.
Hali hiyo inatokana na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo, kutumia nafasi zao kuwanadi wagombea hao, huku wakiwapigia kampeni kwa kutumia madaraka yao.
Akizungumza na Tanzania Daima, mwanafunzi wa mwaka wa pili anayechukua masomo ya Biashara na Uongozi, Owawa Steven, alisema kuwa, anapinga kampeni za kuwania uongozi katika serikali ya wanafunzi kuchukua sura ya kampeni ya vyama vya siasa.
Alisema mmoja wa wagombea watatu wa nafasi ya urais (jina tunalo), anahusishwa kusaidiwa na moja ya vyama vya siasa nchini katika kampeni zake.
Ninasema hivyo kwa sababu kuna wenye viti waliitwa Millennium Tower kupewa pesa ili wampitishe mgombea huyo. Pia mgombea huyo ametumia zaidi ya sh milioni sita kwenye kutengenezea mabango, kuchapishia makala na kukodishia ma-Fuso ambayo yamewekwa muziki mkubwa kwa ajili ya kampeni, alisema Steven.
Wakati hilo likitokea, baadhi ya wanafunzi waliokerwa na hatua hiyo ya chama hicho cha siasa, wameazimia kumpa kura zao mgombea mmoja wa urais anayetoka nje ya nchi, ili kuepusha kuingia kwa masuala ya itikadi za vyama katika uongozi wa chuo kikuu hicho kikongwe kuliko vyote nchini, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za chuo.
Tumeamua kumpa mgeni kura zetu, kwa sababu anatetea haki ya wanafunzi. Aliteuliwa na uongozi kwa kuwa walifikiri kuwa hatapigiwa kura kwa sababu si raia, huku wakijua watu wao watachaguliwa, alisema Steven.
Hata hivyo, mgombea anayetuhumiwa kuungwa mkono na chama hicho cha siasa, alipohojiwa kuhusu hilo, alikanusha akieleza kuwa hizo ni kashfa kutoka kwa wapinzani wake, ambazo anasema amejizatiti kukabiliana nazo.
Nagombea hii nafasi nikitokea katika hali ya kawaida. Pia tuhuma kuwa mimi naungwa mkono na chama cha siasa, hilo mimi silijui na sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote. Kampeni zangu nazifanya na wanafunzi wenzangu ambao tunachangishana pesa kidogo kidogo kwa ajili ya kusukuma kampeni hii. Kumbuka ukiingia sehemu kwa kununuliwa hutafanya chochote, alisema mgombea huyo.
Kwa upande wake, mgombea mwingine kutoka nje ya nchi alilieleza Tanzania Daima kuwa, kampeni zinaendelea vizuri kwa kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi wanamuunga mkono. Hata hivyo, mgombea huyo alilalamika akisema amekuwa akipata vitisho kutoka kwa watu asiowajua.
Alisema endapo atachaguliwa, moja ya mambo atakayofuatilia ni mradi wa Mlimani City, ili kujua unawanufaishaje wanafunzi wa UDSM, kwa sababu upo katika ardhi yao, lakini hawaoni faida yake.
Ninasimama kwenye ukweli, ndiyo maana napata ushirikiano mzuri kutoka kwa wenzangu. Japo kampeni zinazoendeshwa zinanichafua na kusema kuwa nduli amerudi tena, lakini nashukuru kuwa nakubalika, alisema.
Mgombea wa tatu aliyezungumzia suala hilo yeye alisema mazingira ya kufanya kampeni kwa mwaka huu chuoni hapo yamekuwa magumu tofauti na miaka iliyopita.
Uchaguzi utakuwa mzuri kwa kuwa kampeni zimekuwa na ushindani. Hii ni changamoto kwetu sisi wagombea, alisema mgombea huyo asiyehusishwa na kundi lolote.
Uchaguzi huo umekuwa ukilalamikiwa na wanafunzi mbalimbali kwa kuwa umekuwa na itikadi za kisiasa zaidi, kwani baadhi ya wanasiasa na watoto wao wameonekana wakimpigia kampeni au kuwa karibu na mgombea wa kwanza.
Mtoto wa kigogo mmoja mkubwa serikalini, alionekana mara mbili chuoni hapa akiwa na mgombea huyo. Siku ya Ijumaa ambayo ilikuwa ni ya mchujo, alionekana chumba namba 1515, Hall 6, alisema mmoja wa wanafunzi ambaye hakupenda kutaja jina lake.
Wakati huo huo, Rais wa Daruso anayemaliza muda wake, Deo Daud alisema kuwa taratibu za uchaguzi chuoni hapo zinakwenda sawasawa, ila kampeni za mwaka huu zimekuwa na upungufu tofauti na miaka mingine, kwa kuwa hakukuwa na muda mrefu wa kufanya kampeni.
Leo wanafunzi wa UDSM wanamchagua rais wa serikali ya wanafunzi ambaye atakuwa madarakani kwa kipindi cha mwaka mzima. Kampeni hizo za rais zilianza Aprili 7, mwaka huu.
Wagombea wanaochuana katika kinyanganyiro hicho ni, Odong Odwar, Juma Faustine na Mlowe Pesience.
Source: Tanzania Daima