Ubadhirifu Bodi ya Mikopo

armanisankara

JF-Expert Member
Jul 15, 2011
283
49
Vigogo Bodi ya Mikopo (HESLB), wanakabiliwa na tuhuma nzito za ubadhilifu wa fedha kwa kujilipa mishahara minono na matumizi mabaya ya madaraka huku mmoja wao akidaiwa kuajiri ndugu zake 11 wasiokuwa na sifa.
Nusu ya vigogo walioajiriwa katika bodi hiyo wanadaiwa kutokuwa na sifa wala vyeti stahiki kama kibali na tangazo la kazi lilivyotangazwa gazetini.
Vigogo hao pia wanadaiwa kulipwa mishahara minono ya mamilioni ya fedha huku Bodi hiyo ikiwa haizalishi chochote.
Chanzo chetu cha habari ndani ya bodi hiyo kimedai kuwa kigogo wa ngazi ya juu analipwa Sh. 13,875,000 yakiwemo marupurupu na posho.
Anayefuatia analipwa Sh. 12,950,000 kwa mwezi ikiwemo posho wakati mwingine mshahara wake pamoja na posho ni Sh. 12,025,000.
“Watumishi wanaofuata baada ya menejimenti mishahara yao inaanza Sh. 3,000,000 kwenda chini bila posho yoyote,” kilisema chanzo hicho.
Tangu Bodi hiyo ianzishwe mwaka 2005 mikopo iliyotolewa na kupaswa kurudishwa ni Sh. bilioni 300 lakini hadi sasa fedha zilizokusanywa ni Sh. bilioni 9 tu (sawa na asilimia 3).
Kwa mujibu wa chanzo hicho, licha ya utaratibu wa sasa wa serikali wa kutaka ajira zote zitangazwe kwenye vyombo vya habari ili kutoa fursa kwa Watanzania kushindania, lakini kigogo mmoja ametoa ajira za kudumu kwa watumishi kumi (majina tunayo) bila kutangaza wala wahusika kufanyiwa usaili.
Chanzo hicho kimesema kuwa, miezi michache iliyopita bodi hiyo ilitangaza ajira za watumishi 21 wakati kibali cha ajira kilikuwa ni nafasi 24.
“Cha kushangaza nafasi 11 zimejazwa na ndugu wa mmoja wa vigogo hao akiwemo mtoto wake (jina tunalo) ambaye alipewa nafasi ya mwanamke (jina tunalo) aliyekuwa amefaulu nafasi hiyo, nafasi nyingine tatu (majina tunayo) wamepewa wajomba zake,” kimesema chanzo hicho.
Chanzo hicho kimedai watumishi wamekuwa wakipandishwa vyeo kiholela bila kufuata sifa na sheria zilizopo.
“Kwa mfano zipo nafasi kadhaa (majina tunayo) ambazo wale waliopewa hawana sifa, moja inamtaka mtu aliye na sifa na uzoefu wa usiopungua miaka mitatu na nyingine ilikuwa inahitaji mtu mwenye Uzamili (masters), yupo aliyepandishwa cheo bila ya kuwa na CPA (T) kama miongozo inavyosema,” kimebainisha.
Aidha, chanzo kimeendelea kufichua kuwa nusu ya wakurugenzi walioajiriwa hawana sifa wala vyeti stahiki na wanaajiriwa kiudugu.
Baadhi ya vigogo walioajiriwa wanadaiwa kupewa ajira, wakiwa hawana kiwango cha elimu kilichokuwa imetangazwa na kwamba wengine walikuwa bado wanafunzi na wengine hawakuwa na taaluma ya kazi aliyoajiriwa.
Pia chanzo hicho kimedai kigogo wa ngazi ya juu amekuwa na matumizi mabaya ya madaraka ambapo mwaka 2010 alitumia zaidi ya Sh. milioni 50 kwa ajili ya safari nchini Zambia akiambatana na vigogo wengine wawili.
Chanzo hicho kimesema ubadhilifu mwingine ni posho za vikao vya bodi na safari.
Kimebainisha kuwa, malipo ya fedha za wanafunzi vyuoni hutolewa kwa mfumo wa bajeti na kwamba katika mwaka mmoja wa masomo idadi ya vikao vya bajeti HESLB huwa ni 30 au 32.
Chanzo hicho kimesema kwa mwaka posho za vikao hivyo kutengwa kiasi cha Sh. milioni 600 na wanaopitisha bajeti hizo huwa ni wajumbe wa bodi wa kamati ya utoaji wa urejeshwaji mikopo (LARC) na menejimenti ya bodi.
“Kamati hii ina wajumbe wasiopungua watano na wakurugenzi kumi wa bodi yaani menejimenti, kwa kila kikao mjumbe wa bodi hulipwa posho Sh. 500,000 huku wakurugenzi kumi kila mmoja hulipwa Sh. 400,000,” kimesema chanzo na kuongeza:
“Ukijumuisha gharama zilizosalia za posho za kujikimu kwa wajumbe wanaotoka nje ya Dar es Salaam, chai na gharama nyingine kikao kimoja hugharimu Sh. milioni 20, hivyo kwa vikao 30 ni Sh. milioni 600,” kimebainisha.
Aidha, chanzo hicho kimesema kuwa, kiwango hicho kinachotumika kwa mwaka kwa ajili ya vikao hivyo ikizidishwa mara miaka saba ya bodi hiyo kukaa madarakani ni sawa na Sh. bilioni 4.2 kwa kamati moja ya bodi.
“Hii ni sawa na kusomesha wanafunzi wa Shahada za Sayansi ya Jamii 1,400, ila kwa makusudi menejimenti imekuwa ikiagizwa iweke vikao vingi vya LARC wakati akijua kuwa wanafunzi wanateseka vyuoni na njaa kwa urasimu huu usio na tija,” kimefafanua chanzo hicho na kuongeza:
“Bajeti ya mwaka kwa vikao vya bodi na menejimenti ni Sh. bilioni 3 ambapo fedha hizi kama utawakopesha wanafunzi kwa mwaka jumla yao ni 1000,” kimesema.
Aidha, chanzo hicho kimesema kuwa, katika mwaka wa masomo 2011/12 Baraza la Mawaziri kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, chini ya Waziri Shukuru Kawambwa, lilitangaza kwenye vyombo vya habari vigezo vya utoaji mikopo.
Chanzo hicho kimesema licha ya vigezo vya utoaji mikopo kutangazwa lakini ilikiuka kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 600 wasiostahili.
Kimefafanua nafasi hizo zilizotolewa ni wanafunzi 45 wa mwaka wa kwanza wanaosoma shahada ya ‘Law Enforcement’ Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao ni waajiriwa wa Jeshi la Polisi nchini.
“Tangazo lilitoa kipaumbele kwa kozi zote za afya ya binadamu na mifugo, ualimu wa Sayansi na Hesabu. Pia uhandisi, ualimu wa Art, na kozi za Sayansi ambazo zitazingatia uwezo wa muombaji kiuchumi na asiye na sifa linganishi yaani cheti na diploma,” kimesema na kuongeza:
“Kozi ya sayansi ya jamii, hizi si kozi za kipaumbele kwa taifa hivyo watapata fedha itakayokuwa imesalia kwa uhitaji kwa kupima mtu hali yake ya kifedha na shule ya sekondari aliyosoma na kuchukua ile gharama ya juu zaidi , ufaulu haukuwa na kigezo, mikopo isitolewe kwa mtu mwenye sifa linganishi yaani cheti/diploma au aliyeajiriwa,” sehemu ya tangazo hilo imesema.
Chanzo hicho kimesema, wanafunzi hao ambao wengi wao wakiwa na sifa linganishi za cheti/ diploma kinyume cha mwongozo kwa mwaka huo wa masomo awali walikosa wote mikopo.
Aidha, kimesema kuwa baadaye wanafunzi hao kupitia uongozi waliwapatia mikopo kwa njia zisizoeleweka na suala hilo lilifikishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ambaye hakuchukua hatua zozote.
“Wapo wanafunzi zaidi ya 100 watoto wa vigogo wenye sifa linganishi cheti/diploma wanaosoma kozi zisizo za kipaumbele vyuo mbalimbali ambao mwanzoni walinyimwa mikopo na sasa wamepata kinyume cha taratibu,” kimebainisha chanzo hicho.
Chanzo hicho kimesema kuwa, wanafunzi hao wa vigogo walisoma shule za sekondari zenye ada kubwa kati ya Shilingi milioni tatu hadi saba na kwamba huko vyuoni hawasomi kozi za vipaumbele kama tangazo lilivyoainisha.
“Waliosoma shule za Sekondari Fedha Boys na Girls ni wanafunzi 29, Marian Girls Bagamoyo wanafunzi 41, St. Marys wanafunzi 200, Laurentine International wanafunzi 20, Baobao Sekondari wanafunzi 40, St. Francis Mbeya wanafunzi 28, Loyola high school wanafunzi 60 na waliosoma nje ya nchi wanafunzi 10,” kimebainisha chanzo hicho.
Chanzo hicho kimetoa ubadhilifu mwingine uliofanywa na vigogo hao kuwa ni matumizi ya Sh. milioni 300 kwa ajili ya kuhonga ili kuzima zoezi la kuiwajibisha Bodi hiyo baada ya kuundwa Tume ya Rais kuichunguza.
Katika hatua nyingine, chanzo hicho kimesema kuwa katika mwaka wa masomo 2010/11, bodi ilitangaza tenda ya 'scan' fomu za wanafunzi na kampuni iliyokuwa imeshinda ni Digital Scap na kupewa barua ya kufanya tenda hiyo lakini uongozi ulitengua maamuzi hayo na kuipa kampuni ya Koseke.
“Hili linafahamika mpaka PPRA lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa,” kimesema.
Pia chanzo hicho kimesema ubadhilifu mwingine ni bodi hiyo kujilipa mishahara na mikopo mikubwa ya aina mbili yenye riba ya asilimia mbili tu isiyo na uwiano na watumishi wengine.
Jumla ya mikopo iliyotolewa kwa watu hawa 16 ni Sh. 2,560,000,000, kiukweli fedha hizi ni sawa na kutoa mikopo kwa Watanzania 853,” kimebainisha.
Pia chanzo hicho kimesema unyanyasaji wa wafanyakazi HESLB umesababisha wafanyakazi watatu waliofukuzwa na kushinda kesi hiyo iliyokuwa mahakamani Bodi kulazimika kuwalipa fidia ya Sh milioni 300.
Katika hali isiyo ya kawaida, chanzo hicho kimesema, toka mwaka 2005 Bodi hiyo ianzishwe mikopo iliyotolewa na inapaswa kurudishwa ni Sh. Bilioni 300 lakini hadi sasa fedha zilizokusanywa ni Sh. Bilioni 9 tu sawa na asilimia 3.
NIPASHE ilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo ili kupata ufafanuzi wa madai hayo lakini ilijibiwa na mtu wa mapokezi kuwa yuko nje ya mkoa kikazi.
Licha ya kupigiwa simu yake ya mkononi na kutumiwa ujumbe mfupi, hakupokea wala kujibu ujumbe.



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Tutakoma cc watoto wa wakulima!vzuri kama unge post kwenye jukwaa la elimu mkuu!!!!!!!!
 
Back
Top Bottom