Uandikishwaji kupiga kura ubadilishwe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uandikishwaji kupiga kura ubadilishwe

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by Tankthinker, May 19, 2011.

 1. Tankthinker

  Tankthinker Member

  #1
  May 19, 2011
  Joined: May 1, 2011
  Messages: 58
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Uandikishwaji kupiga kura ubadilishwe.

  MOJAWAPO ya matatizo makubwa ya demokrasia yetu jinsi ilivyoundwa na CCM ni kuwa inazuia kundi la wananchi kushiriki kupiga kura kama wanataka kupiga kura. Mbinu hii ya kuzuia upigaji kura hutumiwa vizuri sana pale ambapo kuna uwezekano wa chama tawala kuondolewa madarakani kama wale “wote” wanaotaka kupiga kura watapiga kura.
  Mfumo wetu tulionao sasa hivi ambao unaonesha upungufu mkubwa wa ubunifu wa watawala wetu umetengenezwa kiasi kwamba ni wale tu ambao chama tawala kinataka waje kupiga kura ndio wanaweza kupiga kura. Bila ya shaka unaweza kubisha au kunikatalia. Fuatana nami.
  Mfumo uliopo sasa hivi ni chombo kimoja tu kinachosimamia uandikishwaji kupiga kura na ndicho hicho ambacho hatimaye huamua nani atapiga kura au nani hatopiga kura. Ninazungumzia Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Tume ya Uchaguzi ndiyo iliyopewa jukumu la kuandikisha, kutengeneza orodha ya wapiga kura na kuandaa hata vitambulisho vya wapigaji kura na hatimaye kusimamia uchaguzi mzima.
  Mabadiliko ya Katiba yetu yaliyofanyika mwaka 2000 yaliweka kile ambacho tunakitambua kama Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo liliwekwa chini ya Tume ya Uchaguzi. Hivyo ukawekwa utaratibu wa watu kujiandikisha ukiwa ni miongoni mwa ukiritimba usioingia akilini na ulibuniwa na watu wenye akili timamu.
  Ukitaka kujiandikisha kupiga kura ni lazima usubiri tume ipange muda na siku timu yake itakuwa kwenye mji wako katika kile walichokipa jina la “uboreshaji wa daftari la wapiga kura”.
  Huwezi kujiandikisha kupiga kura hadi tume iamue lini ujiandikishe kupiga kura. Kama ulikuwa tayari umeandikishwa kwenye hilo “daftari la kudumu” basi usiwe na shaka ni kutunza tu namba yako na kusubiri wakati wa uchaguzi uone kama jina lako lipo au la au kama umehama kutoa taarifa kuwa umehama. Hivyo, daftari la wapiga kura linasimamiwa kabisa na Tume ya Uchaguzi bila chombo kingine chochote kuwa na sauti.
  Mfumo huu ni mbaya kwa sababu nyingi tu mojawapo ni hiyo niliyoidokeza hapo juu kuwa hakuna chombo kingine chenye kusimamia au kushiriki mchakato huo na hivyo utaratibu wa kusimamiana haupo (checks and balances).
  Hivyo, Tume ikisema waliojiandikisha kupiga kura ni watu milioni 20 hakuna wa kuhoji; ikisema walijitokeza watu milioni 8 hakuna wa kuhoji na ikitafutwa sababu kwanini watu milioni 12 hawakujitokeza kupiga kura wote tunabakia kuiangalia Tume ya Uchaguzi kutafuta majibu. Hakuna njia yoyote nje ya Tume ya kuweza kuthibitisha nafasi na ushiriki wa wapiga kura.
  Hilo lina maana nyingi sana katika upigaji kura, utangazaji wa matokeo na hata ushiriki wa wananchi kupiga kura. Mfumo huu haupaswi kuendelea na kama ningekuwa na uwezo wa kushauri ubadilishwe naamini unapaswa kubadilishwa mapema hata bila ya kusubiri Katiba Mpya.
  Binafsi, ningependa kutoa mapendekezo yafuatayo kama kuna mtu anaweza kuyasikiliza na nina uhakika vikiunganishwa vichwa vingine humu basi tunaweza kuwa na mapendekezo bora zaidi.
  Daftari la kudumu liwe chini ya Tume ya Uchaguzi, liandikishwe chini ya Halmashauri
  Halmashauri za Miji na Manispaa mbalimbali ndiyo mamlaka zilizoko karibu na wananchi na ambazo zina uwezo mkubwa sana wa kutumiwa kuandisha wapiga kura. Mamilioni ya Watanzania huenda kutafuta huduma mbalimbali karibu kila siku kutoka kwenye halmshauri zao na karibu wote wanajua wapi ofisi zao za Halmashauri zilipo.
  Kwa nini tusitumie Halmashauri kuweka ofisi ya kudumu au hudumu ya kudumu ya uandikishwaji wapiga kura? Fikiria mtu anaenda kwenye halmashauri na amekumbuka kuwa baada ya mkutano mkubwa wa chama chake hatimaye anaamua kwenda kuwa mpiga kura, kwanini mtu huyu asubiri hadi Tume ya Uchaguzi ipange siku ya kwenda “kuboresha” daftari hilo wakati angeweza tu kuamua kesho yake kwenda kwenye ofisi za Halmashauri na kujiandikisha.
  Halmashauri ikishapata majina na vitambulisho vyote vinavyotakiwa ikiwemo picha za mpiga kura zinatumwa taarifa hizo (kwa njia ya mtandao) kwenye Tume ya Uchaguzi ambapo kitambulisho cha kudumu cha mpiga kura kinatengenezwa na kutumwa kwenye Halmashauri ambapo mpiga kura ataenda kukichukua. Kutakuwa na faida nyingi tu za kufanya hivi kwanza hakutakuwa na gharama za kupeleka watu mara kwa mara na kuhamisha vifaa kwenda kuboresha madaftari na kuondoa ulazima wa misururu ya watu kusubiri kujiandikisha.
  Uzuri mwingine ni kuwa taarifa za vifo haziitaji kusubiri tume ije kuboresha ili waweze kuwaondoa watu kwenye daftari la kudumu. Wafiwa wanajua kati ya mambo ambayo watatakiwa kuyafanya ni kwenda kwenye Halmashauri na vyeti vya vifo na cha kupiga kura na kusema huyu mpiga kura amefariki na Halmashauri inafuata utaratibu wa kujulisha Ofisi za Daftari la kudumu ambapo jina la huyu mtu linaondolewa na hivyo uboreshaji wa daftari la wapiga kura unafanyika karibu mwaka mzima.
  Iandikwe sheria ambayo mtu anapotimiza miaka kumi na nane ni lazima ajiandikishe kupiga kura
  Mojawapo ya mambo ya ajabu sana ni kuwa tumeiga mtindo wa kuwaondolewa watu haki ya kupiga kura pasipo sababu yoyote. Binafsi ninaamini kuna sababu tatu tu ambazo zinapaswa kuondoa haki ya mtu kupiga kura; hajatimiza umri wa utu uzima (miaka 18), hana akili timamu kwa sababu ya ugonjwa wa kudumu wa akili, si raia wa Tanzania. Leo hii kwa mfano tumeweka kwenye sheria kuwa mtu akihukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita basi hawezi kuandikishwa, kwamba akishtakiwa kwa makosa fulani hawezi kuandikishwa, kwamba akiwa katika hukumu ya kifo hawezi kuandikishwa. Hii haiingii akilini.
  Kimsingi, tumejipa madaraka ya kuwanyima watu wetu haki ya kumchagua kiongozi wao wakati kiongozi huyo ataamua maisha yao yaweje. Hivi kama kuna wafungwa ambao wanaamini sheria ambazo zimewasababisha wawe kifungoni si za haki na yupo mgombea ambaye wanaamini atasimamia sheria bora zaidi ili wengine wasijikuta huko lupango kwanini wasiwe na haki ya kumchagua kiongozi huyo wakati wanatimiza hayo masharti matatu ya msingi?
  Uzuri wa kuwa na utaratibu wa nje ya Tume ya Uchaguzi kujiandikisha kupiga kura basi hata kwenye maeneo ya magereza wafungwa wanaotaka kujiandikisha kupiga kura wanaweza kufanya hivyo na hata wakihama gereza au kutoka gerezani wanakuwa na haki yao ya kikatiba ya kupiga kura. Sijui ni watu gani waliojipa uwezo wa kufuta haki ya mwananchi kupiga kura kiholela hivi. Sioni uhusiano wa moja kwa moja wa mtu kufungwa na kuondolewa haki ya kuchagua viongozi wako.
  Kimsingi, tukiweka utaratibu kuwa mtoto anapofikisha miaka kumi na nane (mtu mzima) basi ajue ni lazima na ni haki yake kujiandikisha kuwa mpiga kura. Hivyo, kijana akijua wajibu huo hana sababu ya kusubiri tume ya Uchaguzi bali anaenda kwenye halmashauri yake na kujiandikisha kuwa mpiga kura.
  Uandikishaji kupiga kura utaendana na kupata pasi ya kusafiria au kitambulisho cha uraia
  Kwa vile kuna vitambulisho vingine viwili muhimu basi vinaweza vyote kuweza kufanyika kwenye ofisi hizi za Halmashauri. Kwa mfano, kule Marekani pasi ya kusafiria ya Marekani huweza kuombwa na baadaye kuja kuchukuliwa kwenye tawi la posta la nchi hiyo. Matawi ya posta yapo mengi karibu kila kona na hivyo mtu kupata pasi ya kusafiria haitaji kwenye kwenye ofisi ya Uhamiaji kama ilivyo Tanzania.
  Sasa tukiweka utaratibu huu kwenye Halmashauri tunaweza pia kutumia ofisi hizo hizo kwa ajili ya kuombea pasi ya kusafiria na hata kitambulisho cha uraia. Fikiria kwa mfano mtu unaenda kuomba kitambulisho cha kupiga kura unaulizwa “unataka pasi ya kusafiria” unasema “ndiyo” basi unajaza na fomu zao na kulipa ada yao; unaulizwa una kitambulisho cha “uraia” unasema “sina”. Sasa umeenda pale na vitambulisho vyote vinavyoweza kutumika kupiga kura ambacho kimsingi ndivyo vinavyokuonesha kuwa ni raia na ambavyo vinaweza kutumika kuombea pasi.
  Vitambulisho vyako vyote vikishaangaliwa na picha na alama za kimwili (biometrics) ambazo zinahitaji kuchukuliwa zikichukuliwa wewe mpiga kura unaondoka na labda kitambulisho chako cha muda cha uraia na cha kupiga kura wakati unasubiri vitambulisho vya kudumu. Baada ya sema siku 21 na si zaidi ya siku thelathini unaenda kwenye halmashauri yako unachukua vitambulisho, pasi yako. Tutajikuta tunaondoa ukiritimba mwingine mkubwa sana wa kupata pasi za kusafiria na tutakuwa tumesogeza huduma hizi muhimu kwa watu wetu katika maeneo yao.
  Kujiandikisha kutawezekana hata muda mfupi kabla ya uchaguzi
  Kwa vile tutakuwa na orodha ya wapiga kura ambayo inaendana na wakati sana wakati wowote wa uchaguzi uwe mdogo au uchaguzi mkuu au hata kura za maoni watu watakachohitaji kufanya ni kwenda huko huko kwenye Halmashauri kuthibitisha kuwa watashiriki uchaguzi huo ili kusaidia katika masuala ya bajeti ya uchaguzi na miundombinu yako.
  Sasa uzuri wake mmoja ni kuwa kwa kuwa na taarifa ambazo ziko na wakati ni rahisi hata kufanya makisio ya vitu mbalimbali na vile vile inaweka uwezekano wa mtu kuweza kujithibitisha kushiriki uchaguzi hadi kama wiki mbili kabla ya uchaguzi wenyewe.
  Hii ina maana ya kuwa mpiga kura anaweza akafuatilia kampeni mbalimbali na hatimaye kukata shauri kushiriki uchaguzi bila kuwa na wasiwasi wa jina lake kutokuwepo kwenye uchaguzi.
  Majina ya Wapiga kura wa uchaguzi yataweza kuwepo kwenye Halmashauri
  Mojawapo ya mambo ambayo yanashangaza sana na kusababisha usumbufu ni kujua kama jina lako “lipo” kwenye eneo fulani la uchaguzi au kituo fulani. Kama mtu ameandikishwa kupiga kura na amethibitisha kupiga kura basi utaratibu huu ninaopendekeza utamuwezesha kupiga kura kwenye kituo chochote kilichoko kwenye halmashauri yake.
  Hii ina maana badala ya mtu kuhangaika kutoka eneo moja la Halmashauri (labda anakofanya kazi) na kwenda eneo jingine (karibu na nyumbani) basi mpiga kura anaweza kabisa kupiga kura kwenye kituo kilicho karibu yake ilimradi tu jina lake liko kwenye orodha ya wapiga kura wa Halmashauri ile.
  Hii itaondoa mojawapo ya mambo mabaya tuliyoyaona kwenye uchaguzi uliopita ambapo mtu aliamini jina lake lipo na ana kitambulisho lakini anaenda kwenye eneo la kupigia kura na kuambiwa hawezi kupiga kura wakati ana kitambulisho na wasimamizi wa kituo wasiwe na la kufanya. Katika mtindo huu, kwa kadiri mtu anakitambulisho cha kupigia kura (na hata kama akipoteza lakini anacho cha uraia au pasi yake ya kusafiria) ambavyo vimeonanishwa na vile vya kupigia kura basi ataweza kupiga kura yake.
  Ndugu zangu, mapendekezo haya na kama nilivyosema hapo juu na ya wengine yanaweza kutusaidia kuja na mfumo mzuri wa kujiandikisha na kupiga kura ambao utahakikisha kanuni muhimu sana ya demokrasia inazingitiwa: anayetaka kupiga kura kwenye uendeshaji wa nchi yake anafanya hivyo. Kati ya haki za kiraia za msingi sana ni haki ya raia kushiriki katika maamuzi ambayo yatamgusa yeye. Haki hii kwangu ni haki kubwa sana ambayo Tanzania bado hatujaipa nafasi yake kwani watu wanaona kama hisani ya serikali kwa wananchi. Hili siyo ombi au wazo la kukata hivi hivi. Lazima utengenezwe mfumo utakaohakikisha ushiriki wa hali ya juu kabisa wa wananchi katika kupiga kura bila kuwa na vizuizi visivyo na sababu.
  Unasemaje?

  Source. Raia mwema.

  Ushabiki ni mzuri kwa timu uipendayo, lakini ushabiki mzuri hukosoa makosa ya timu uipendayo. KSDK
  [​IMG]
   
Loading...