Tuwe wakweli, kwa pesa hii kuna mzawa kweli ataweza kuwekeza?

Maboso

JF-Expert Member
Feb 18, 2013
5,164
5,761
TAARIFA KWA UMMA

ZABUNI YA 4 YA KUNADI VITALU VYA UTAFITI WA GESI ASILIA

Utangulizi.



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), tarehe 25/10/2013 ilizindua rasmi zabuni ya nne ya vitalu vya utafiti wa mafuta na gesi asilia vilivyoko bahari kuu na ziwa Tanganyika kaskazini. Uzinduzi wa zabuni hii ulihusisha vitalu 7 vilivyoko bahari kuu (deep offshore blocks) pamoja na kitalu cha ziwa Tanganyika kaskazini (Lake Tanganyika North). Vitalu vya bahari kuu vipo katika kina cha maji kati ya mita 2000 na 3000 wakati kitalu cha ziwa Tanganyika kinafikia kina cha mita 1500. Mchakato wa zabuni utafungwa rasmi baada ya miezi sita na Zabuni zitakazowasilishwa kabla ya saa nne asubuhi ya Alhamisi ya tarehe 15 mwezi Mei mwaka 2014. Zabuni zitafunguliwa kwa uwazi mbele ya washiriki wa mnada watakaopenda kuwepo ama kuwakilishwa siku ya ufunguzi.






Majina ya vitalu vinavyonadiwa ni kama inavyooneka katika jedwali hapa chini.

NambariJina la kitaluEneo (mita za Mraba)
1Block 4/2A3630
2Block 4/3A2620.3
3Block 4/3B3045.0
4Block 4/4A2963.3
5Block 4/4B3048.9
6Block 4/5A2545.3
7Block 4/5B3052.6
8Lake Tanganyika North9670.2



Faida za Ugawaji wa Vitalu vya utafiti kwa njia ya Zabuni



Utaratibu huu wa kutoa maeneo kwa kutumia zabuni hutumika sehemu nyingi duniani zikiwemo nchi nyingi za Bara la Afrika, Asia, Ulaya, Marekani (kusini na kaskazini). Umuhimu wa kugawa vitalu kwa njia ya zabuni ni pamoja na:


  • kuhakikisha kuwa mchakato mzima unafanyika kwa njia ya uwazi;

  • kutoa vitalu kwa utaratibu mzuri ili kuweza kuendeleza rasilimali kwa gharama nafuu endapo ugunduzi utafanyika;

  • kupata wawekezaji bora wenye mitaji, utaalamu na uzoefu wa kufanya utafutaji;

  • kutoa nafasi kwa wawekezaji wazalendo kushiriki katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi; na

  • kutoa fursa kwa makampuni mengi na wataalamu mbalimbali kuona takwimu (data) zilizopo na hivyo kupata kwa wingi maoni mbali mbali ya kitaalamu kuhusiana na uwezekano wa kuwepo mafuta na/au gesi.

Gharama za kushiriki kwenye Zabuni
Gharama za kushiriki kwenye zabuni zinajumuisha ada isiyorejeshwa ya ushiriki kwenye zabuni, gharama za kununulia kifurushi cha zabuni yenyewe, gharama za kununulia vifurushi vya data za mitetemo cha lazima kwa waomba zabuni wa vitalu zilivyopo bahari kuu na ziwa Tanganyika kaskazini na gharama za kununulia ‘data’ za nyongeza za hiari kadri mshiriki atakavyoona inafaa.

Ada ya ushiriki kwenye zabuni isiyorejeshwa ambayo ni Dola za Marekani 50,000. Gharama halisi ni kama zilivyonyambuliwa hapa chini:
Gharama kwa muombaji wa vitalu vya baharini

  1. Gharama za kununulia kifurushi cha lazima cha zabuni za vitalu vya bahari kuu (Bidding Round Data Package (BRDP) for deep offshore blocks) ni Dola za Marekani 750,000 kwa kila kifurushi.

  1. Gharama za kununulia kifurushi cha lazima cha taarifa za mitetemo ya ‘Mandatory 2D SPAN’ ni Dola za Marekani milioni

  1. Gharama za kununulia taarifa za hiari za mitetemo ya ‘Optional 2D SPAN data’ ni Dola za Marekani 750 kwa kila kilomita moja ya urefu.
Gharama kwa muombaji wa kitalu cha kaskazini ya ziwa Tanganyika

  1. Gharama za kununulia kifurushi cha lazima cha zabuni ya kitalu cha ziwa Tanganyika kaskazini (BRDP for Lake Tanganyika North) ni Dola za Marekani 350,000 kwa kila kifurushi
  2. Gharama za kununulia taarifa za hiari za mitetemo ya ‘Optional Phase I and Phase II data’ ni Dola za Marekani 220 kwa kila kilomita moja ya urefu.
Waomba zabuni ni lazima waoneshe ushahidi wa kununua taarifa (data) kwa kuambatisha risiti ya manunuzi pamoja na mkataba wa kutunza siri waliosaini katika zabuni watakazo rejesha.

Kabla ya kushiriki katika uombaji zabuni, makampuni yote ni lazima yaweze kutimiza masharti ya zabuni yaliyowekwa. Makampuni inabidi yanunue kifurushi cha zabuni husika (Bid Round Data Package – BRDP).

Kifurushi cha zabuni (Bid Round Data Package – BRDP)
Katika kifurushi hiki kuna vitabu vya zabuni pamoja na maelekezo ya taratibu za kushiriki na kuwasilisha zabuni [Bidding Instructions]; maelezo ya jinsi ya kutathini zabuni [Evaluation Criteria]; vipengele vya tathmini ya uwezo kifedha [Fiscal Terms]; mfano wa mkataba wa kugawana mapato wa 2013 [Model Production Sharing Agreement]; Sheria inayosimamia utafiti na uzalishaji ya mwaka 1980 [Petroleum (Exploration and Production) Act 1980]; Sheria ya Hifadhi ya Mazingira [Environmental Management Act 2004]; Sera ya Nishati ya 2003 [Energy Policy of 2003]; na Sera ya Gesi Asilia ya 2013 [Natural Gas Policy].

Sababu za kuuza data
Data za utafutaji mafuta na gesi huuzwa kwa sababu gharama za kukusanya data ni kubwa sana, hivyo mauzo hufidia gharama za ukusanyaji data hizo za awali na kufanya miradi ya ukusanyaji data kuwa endelevu.

Kwa upande wa baharini inabidi kukodi meli maalumu zenye mitambo ya kukusanyia data. Meli hizi zinabeba mitambo na kompyuta maalumu zinazotumia teknolojia ya hali ya juu kurekodi tabia za miamba za kuakisi mawimbi ya sauti chini ya ardhi (reflection seismic methods). Meli hizi huweza kukaa baharini kwa hadi miezi mitatu au zaidi zikifanya shughuli za ukusanyaji data na zinahudumiwa kimahitaji kwa kutumia helikopta na meli ndogo za kutoa huduma. Ulinzi pia kujikinga na maharamia huhitajika. TPDC na wabia wake hugharamia zoezi la ukusanyaji data. Ni wazi kwamba gharama hizi huwa ni kubwa sana, hivyo inabidi data zinazopatikana ziuzwe ili mwekezaji na TPDC waweze kurejesha gharama zao.

Kwa upande wa nchi kavu napo pia gharama ni kubwa. Gharama huanza kwa kutengeneza mikuza, kulipa fidia, kulipa makandarasi wa kipima mikuza, kusafisha mikuza na kurekodi tabia za miamba za kuakisi mawimbi data za mitetemo.

Tunahitaji makampuni yatumie data hizi kutathmini sehemu ambazo zinaweza kuwa na hifadhi za mafuta na gesi asilia. Tathmini hizo zitatumika kusaidia wataalamu kupima uwezo wa makampuni na kuchagua kampuni stahili kupewa vitalu.

Utazamaji wa Takwimu/ Taarifa - Data Viewing
Utazamaji wa taarifa za kijiofizikia na kijiolojia (data viewing) unaweza kufanywa kwenye ofisi za Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC). Mtazamaji anapaswa kuweka miadi ‘appointment’ ya kutembelea chumba chenye hizo taarifa kupitia:

Shirika la Mendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
Tower A, Benjamin William Mkapa, Pension Towers Building, Plot 23/90-23/92 Azikiwe/Jamhuri Streets,
Dar Es Salaam,

Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
Simu ya mezani : +25522 2200103/4
Barua pepe :tpdc4thround@tpdc-tz.com

Tovuti :www.tpdc-tz.com/tpdc/


Mtazamaji atapata nafasi ya kuona taarifa zilizomo kwenye kifurushi cha zabuni cha vitalu vya bahari kuu (BRDP), kifurushi cha zabuni cha ziwa Tanganyika, ‘data’ za lazima za mitetemo zenye jumla ya kilometa 4500 za urefu, na taarifa nyinginezo za mitetemo kama zitahitajika na pamoja na seti ya ‘data’ za zamani zilizoboreshwa.

SEHEMU A: USHIRIKI WA WAZAWA
Maelezo kuhusu fursa sawa katika kushiriki kwenye mnada wa vitalu vya utafiti wa mafuta na gesi ni kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 (Public Procurement Act, 2002).
Ingawa Zabuni iko wazi kwa makampuni ya ndani na ya nje kushiriki, Utaratibu umewekwa utakaotoa upendeleo kwa makampuni ya ndani yaliyosajiliwa kwa sheria za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kumilikiwa na wazawa kwa asilimia zisizopungua 50 ikiwa yatatimiza vigezo vilivyowekwa kuviwezesha kupata huo upendeleo. Vilevile ushirikiano wa ubia kwa makampuni yanayomilikiwa na wazawa na yale ya nje utapewa upendeleo ikiwa utatimiza vigezo vilivyowekwa ambavyo vinataka pamoja na mambo mengine; kuthibitisha kuwa atafanya kazi zenye thamani isiyopungua asilimia 10 ya gharama ya kazi na kuwa atapata mgawo usiopungua asilimia 20 ya faida itakayopatikana.

Mambo ya kufanya ili kushiriki kwenye Zabuni
Kampuni inayotaka kununua data na kushiriki kwenye zabuni inaweza kuwasiliana na:
Mkurugenzi Mtendaji,

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania,

Tower A, Benjamin William Mkapa Pension Towers Building, Plot 23/90- 23/92 Azikiwe/Jamhuri Streets,

  1. 2774,

Tel: +25522 2200103/4

Dar Es Salaam, TANZANIA

Barua pepe: tpdc4thround@tpdc-tz.com

Wazabuni watarajiwa wanaweza kutuma maswali ya ufafanuzi kuhusiana na zoezi la zabuni.

Muombaji anapaswa kurejesha kwa mkono nakala 2 pamoja na nakala halisi vikiwa vimefungwa na kuviweka katika sanduku la zabuni lililopo katika ofisi kuu za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, (Tower “A”) chumba numbari 401 kilichopo gorofa ya nne, jengo la Benjamin William Mkapa Pension Towers, Kitalu nambari 23/90-23/92, Azikiwe/Jamhuri



Streets, Dar es Salaam, au itumwe kwa huduma ya kutuma vifurushi vilivyoandikishwa (registered post/mail) kwenda kwa:

Katibu wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania S.L.P. 2774, Dar-es-Salaam.

Mshiriki katika zabuni pia anaweza kushiriki katika zabuni kwa kuwasilisha zabuni yake siku ya ufunguzi kabla ya saa nne asubuhi kwa masaa ya Tanzania siku ya Alhamisi tarehe 15 mwezi Mei mwaka 2014 kama ilivyoelekezwa kwenye muongozo wa zabuni uliokwishatolewa na unaweza kuuona kwenye tovuti maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya zabuni ya ugawaji wa vitalu: http://www.tz-licensing-round.com


Tathimini za Zabuni za vitalu zilizopokelewa
Zabuni za vitalu ni zabuni za kimataifa na za wazi kwa makampuni yenye nia ya kufanya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Zabuni hizo hazibagui asili ya makampuni, kampuni yaweza kuwa ya kitaifa au ya kimataifa. Utoaji wa zabuni huzingatia mambo makuu matatu;


  • uwezo wa kampuni kifedha;

  • uwezo wa kampuni kitaalamu; na

  • mgawo wa rasilimali kwa Taifa endapo gesi na mafuta vitagunduliwa.

Zabuni zitakazopokelewa zitafanyiwa tathimini kufuatana na vigezo vilivyowekwa kulingana na kazi za kitaalamu ambazo muomba zabuni atakuwa ameahidi kuzitekeleza kwa vipindi vyenye jumla ya miaka 11 (4/4/3) ya utafiti kama vilivyo kwenye sheria inayosimamia shughuli za utafiti na uzalishaji wa mafuta na gesi Tanzania. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika ataunda Kamati ya kufanya tathimini kwa mujibu wa sheria inayosimamia manunuzi ya umma.

Mapendekezo ya Kamati ya tathimini hupitiwa na Bodi ya Manunuzi ya Shirika ambapo mapendekezo ya Bodi ya Manunuzi huwasilishwa kwa Mkurugenzi Mtendaji ambaye naye huyawasilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika ili kuandaa mapendekezo yatakayopelekwa kwa Waziri kwani ndiye mwenye dhamana ya kutoa leseni za utafiti. Kama Waziri atakubaliana na mapendekezo aliyoletewa ataiagiza kampuni iliyoshinda itaarifiwe na kujiandaa kwa mazungumzo na timu ya washauri wa serikali kuanza kwa nia ya kusaini mkataba wa kugawana mapato. Mkataba huu pindi unaposainiwa pamoja na majukumu hutoa haki za kipekee kwa kampuni iliyoshinda zabuni kufanya shughuli za kutafuta mafuta na gesi asilia kwa kipindi kilichowekwa katika eneo husika.

Kampuni iliyoshinda hupewa kuendesha leseni ya utafutaji na Waziri wa Nishati na Madini kwa niaba ya TPDC kama mkandarasi. Kampuni hiyo itapaswa kufanya kiasi cha kazi za kitaalamu za kitafiti zitakazo husisha shughuli za kijiofizikia, kijiolojia na kijiochemia kama ilivyo kwenye mkataba.

Kazi hizo huhusisha uchukuajia wa data za mitetemo za 2D na 3D, uchimbaji wa visima vya utafiti, uchimbaji wa visima vya kuthibitisha kiasi ya hazina ya gesi au mafuta iliyopatikana na pia uchimbaji wa visima vya uendelezaji wa maeneo hazina ilipogunduliwa.

Makadirio ya gharama za mfano kwa kiwango cha chini kufanikisha shughuli za utafiti mpaka uendelezaji zinaweza kuwa kama zilivyoainishwa hapa chini:

Dola za Marekani
Tathimini za kijiofizikia na kijiolojia10 milioni
Ukusanyaji wa takwimu za 2D na 3D5 - 25 milioni
Jumla kwa Tathmini zote za kimazingira (EIAs)12 milioni
Uchimbaji wa visima 3 vya utafiti (@ 170 mill)510 milioni
Uchimbaji wa visima 6 vya tathmini (@ 150 mill)900 milioni
Uchimbaji wa visima 10 vya uendelezaji (@ 100 mill)1000 milioni

Jumla ya gharama isiyohusisha miundombinu Dola za Marekani milioni 2437 (2.4 Bn)
Makadirio haya hayahusishi gharama za kuweka miundombinu ya kuwezesha uzalishaji, usafishaji, uchakataji, uuzaji na gharama zinginezo. Gharama hizi zinaonesha makadirio ya gharama za awali za shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Gharama za uendelezaji kuweka miundombinu hadi kufikisha gesi kwa mtumiaji huweza kufikia hadi Dola za Marekani bilioni 15 (US$ 15Bn).

Baada ya kusainiwa kwa mkataba, mshindi wa zabuni atatakiwa kutekeleza mambo aliyoahidi wakati wa vipindi vya utafiti.

Akichimba kisima na kugundua mafuta au gesi, atapaswa kufanya utafiti zaidi ili kujiridhisha kuwa kiasi kilichogunduliwa kinaweza kuzalishwa kwa faida. Katika utafiti huo, mwenye leseni analazimika kuchimba visima zaidi pamoja na kufanya thathmini za kijiofizikia na kijiolojia zaidi.

Akijiridhisha, kuwa hazina iliyogunduliwa inaweza kuzalishwa kwa faida, anapaswa kuomba leseni ya uzalishaji ambao hutakiwa kuambatanisha maombi yake na mpango kabambe wa kuendeleza hazina iliyopo (mafuta au gesi). Waziri akiridhika na mpango uliowasilishwa na kampuni, huipa hiyo kampuni leseni ya uendelezaji inayompa haki mwenye leseni kuendeleza na kuizalisha hazina aliyoipata kwa kipindi cha miaka 25 na inaweza kuongezwa kwa kipindi kingine cha miaka 20.

Mauzo ya kinachozalishwa hutumika kurudishia gharama zilizowekezwa kwenye shughuli zote za mradi na faida hugawanywa kwa namna iliyokubalika katika mkataba wa kugawana mapato.
Taarifa hii inatolewa ili kuelimisha umma kuhusiana na zabuni za ugawaji wa vitalu iliyozinduliwa tarehe 25/10/2013 na haipaswi kuchukuliwa kama maelekezo kwa wanaotaka kushiriki kwenye zabuni (Invitation to Bid). Maelekezo ya namna ya kushiriki kwenye zabuni yanapatikana kwenye mtandao ufuatao:

(http://www.tz-licensing- round.com/pdf/Invitation%20for%20Bids%2031%20Oct%202013.pdf).

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linayaalika makampuni ya wazawa yenye uwezo wa kifedha na kitaalamu kushiriki katika zabuni iliyotangazwa ya kutafuta wawekezaji wa vitalu vya utafiti sambamba na makampuni ya nje.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na:
Idara ya Utafutaji, Uzalishaji na Huduma za Kiufundi, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania

Tower A, 9th Floor; BWM Pension Tower Azikiwe/Jamhuri Street
P.O. Box 2774

Dar es Salaam, Tanzania
simu: +255 22 2200103/4, 2200112
fax: +255 22 2200113
Barua pepe: tpdc4thround@tpdc-tz.com
 
Back
Top Bottom