SoC03 Tutoke gizani tupunguze maambukizi mapya ya VVU

Stories of Change - 2023 Competition

Mrs Samambo

New Member
Jul 25, 2023
2
3
Ugonjwa wa UKIMWI sambamba na maambukizi ya VVU kwa dunia ya sasa siyo tishio kubwa sana kama ilivyokuwa miaka ya themanini kipindi ugonjwa huo ulivyoingia. Hii imekuja baada ya ujio wa ARV ambazo kwa kiasi kikubwa zimeweza kusaidia kufubaza VVU na kutoa tumaini jipya la maisha kwa watu walioathirika.

Elimu ya UKIMWI inayoendelea kutolewa na serikali ikishirikiana na taasisi nyingine zisizo za kiserikali imesaidia pia kuendelea kupunguza ongezeko la maambukizi mapya ya VVU ila itoshe kusema kuwa uelewa mkubwa juu ya ugonjwa huu bado ni changamoto kwa wanajamii wengi.

Mafunzo mengi yanayoendelea kutolewa ni jinsi ya kujikinga na maambukizi kwa kutumia kondomu, kupima afya, matumizi ya ARV Pamoja na kuachana na unyanyapaa kwa wanaoishi na VVU lakini kuna mambo mengine bado hayajawekewa msisitizo.

Katika jamii yetu kwa sasa, watu hawaogopi UKIMWI Kama ilivyokuwa hapo awali kiasi cha wengi kutokuchukua tahadhari katika kujiepusha na maambukizi lakini changamoto bado ipo kwa wale wanaokuja kujigundua kuwa wamepata maambukizi, wapo ambao hupatwa na hofu kiasi cha kuanza kudhoofika ghafla, kukata tamaa na hata wengine kujiua au kuua wenzi wao ambao huhisi kuwa wamewaletea maambukizi.

Tatizo la unyanyapaa pia bado lipo ingawa siyo kwa kiwango kikubwa Kama ilivyokuwa hapo awali. Mimi nimebahatika kupata elimu juu ya masuala ya UKIMWI na natamani karibu kila mwanajamii angeipata na kuielewa nina uhakika tungepiga hatua kubwa sana kwenye kupunguza maambukizi mapya.

Wimbo wangu mkubwa utabaki kuwa ELIMU, ELIMU, ELIMU juu ya masuala ya UKIMWI na VVU katika kila ngazi ya jamii. Ninaishi na jamii ya wasomi (ninafanya kazi kwenye taasisi ya Elimu ya juu) lakini kuna masuala ya UKIMWI ukizungumza hata na hao wasomi wanaishia kuguna na kuona kuwa haiwezekani.

Hili lisitukatishe tamaa kwani ninaamini suala la uelewa wa mambo ni utashi wa mtu binafsi, Kuna watu hawajabahatika kusoma lakini ni wazuri mno kwenye kudadavua masuala mbalimbali ya kijamii. Je ni elimu gani hii ambayo natamani jamii iwafikie?

1. Natamani kila mwanajamii angetambua kuwa unaweza kuishi na mtu mwenye VVU, mkakutana kimwili na asiweze kukuambukiza. Hapa kuna mambo kadhaa ya kufanikisha Jambo hili, kwanza kabisa ni mtu mwenye VVU kutumia ARV kwa usahihi kiasi cha kufikia hatua ya kutokuweza kuambukiza mtu mwingine. ARV hufubaza virusi hivyo zikitumiwa kwa usahihi huwa inafika hatua mtu mwenye virusi anakuwa hawezi kuambukiza mtu mwingine hata wakikutana bila kutumia kinga. Jambo lingine ni wenza kuhakikisha hawapati michubuko wakati wa kujamiiana, Pamoja na matumizi ya PREP.

Nimewahi kushuhudia watu wakivunja mahusiano baada ya kukuta mwenzi mmoja akiwa na maambukizi kwa hofu kuwa nikiishi nae ataniambukiza. Laiti elimu hii ikipatikana kwa usahihi watu wasingekimbiana na maisha yangeendelea Kama kawaida. Nimewahi pia kushuhudia wanandoa wenye hali tofauti za afya (mwenye maambukizi na asiye na maambukizi) wakiishi Pamoja na wamejaliwa kupata watoto wenye afya njema kabisa wasiokuwa na maambukizi.

Binafsi niliwahi kwenda kupima afya na mwenzi wangu, na kabla hatujaenda nikamwambia hata nikimkuta na maambukizi sitaachana na yeye (niliongea nikimaanisha haswa), ila yeye aliniambia ikitokea mimi nina maambukuzi ataniacha (hahahahaha). Nacheka siyo kwa uzuri ila ELIMU bado sana kwenye jamii yetu.

2. Watu wenye maambukizi wanaweza kuzaa watoto wasiokuwa na maambukizi. Kwa kufuata kanuni za afya, watu wenye maambukizi ya VVU wanaweza kupata watoto wenye afya njema kabisa wasiokuwa na maambukizi ya Afya kikubwa ni kuhakikisha wanatumia dawa zao kwa usahihi na mama anaanza kliniki mapema pindi tu anapojigundua kuwa ni mjamzito ili aweze kupewa dawa za kuzuia maambukizi yasitoke kwake yakaenda kwa mtoto aliyepo tumboni. Kwa maeneo ya mjini tatizo hili kwa sasa ni dogo kwani muamko wa wanawake kuhudhuria kliniki ni mkubwa tofauti na maeneo ya vijijini. Elimu ya masuala ya uzazi iendelee kutolewa kwa mkazo zaidi maeneo ya vijijini Pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinafikishwa kwa ukaribu zaidi

3. Elimu juu ya matumizi ya PREP na PEP ifike kwa wanajamii wengi zaidi na zipatikane kwa urahisi. Hizi ni dawa ambazo zinatumiwa na watu ambao hawana maambukizi ili kujikinga dhidi ya maambukizi. PREP hutumiwa kabla ya kushiriki tendo na mtu mwenye maambukizi na ni dawa ambazo zinatakiwa kutumiwa kila siku. Zinafanya kazi vizuri zaidi zikitumiwa siku Saba kabla ya kuanza kukutana na mwenzi ili mwili uweze kutengeneza Kinga vizuri zaidi.

PEP hutumiwa ndani ya masaa 72 baada ya kukutana na mtu mwenye maambukizi au kwa mtu ambaye anahudumia watu wenye maambukizi na yupo kwenye hatari ya kupata maambukizi mfano wahudumu wa afya, na zinaendelea kutumiwa kwa muda wa mwezi mzima. Kuna vitendo vinatokea katika jamii zetu ambavyo ni vya kikatili na huwaweka waliotendewa katika hatari ya kupata maambukizi mfano ulawiti na ubakaji. Jamii ikiwa na uelewa mzuri juu ya matumizi ya dawa hizi itasaidia hata kwa wale waliobakwa kupatiwa dawa na kuepushwa na maambukizi

4. Sheria ya UKIMWI ifahamike kwenye ngazi zote za jamii. Adhabu ziainishwe wazi kwa makosa yote yaliyoongelewa kwenye Sheria ya UKIMWI ya mwaka 2008. Sheria imeelezea wajibu wa serikali, watu binafsi na Taasisi mbalimbali juu ya masuala ya UKIMWI. Kwa mfano, sheria imeweka wazi wajibu wa mtu mwenye maambukizi kuwa anatakiwa kulinda wengine wasipate maambukizi. Katika jamii yetu ya Leo Kuna watu wakishajigundua kuwa wamepata maambukizi hudiriki kuanza kuambukiza wengine kwa makusudi.

Wapo wenye maambukizi wanashirikiana na watoa huduma za afya kuficha hali halisi ya maambukizi kwa wenzi wao Jambo ambalo Sheria inatakiwa kusimama kulikomesha kwa kutoa adhabu kali na hata kuwafutia leseni zao za Biashara/kazi watoa huduma za afya wote watakaojihusisha na udanganyifu huu.

HITIMISHO
Suala la mapambano juu ya ugonjwa wa UKIMWI ni la jamii nzima. Kwa sasa kuwa na VVU au UKIMWI siyo kifo ila inabidi kujikinga na maambukizi kwani Pamoja na uwepo wa ARV lakini tukumbuke zoezi la kunywa dawa kila siku mpaka mwisho wa maisha yako siyo zoezi dogo. Ni zoezi linalotaka kujikubali na kuwa na moyo haswa.

Serikali pia inatumia rasilimali fedha nyingi kwa ajili ya kuagiza dawa na vifaa tiba kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI hivyo jamii nzima ikijitahidi kupunguza maambukizi itaisaidia serikali kupunguza matumizi kwenye eneo hili na fedha hizo kuelekezwa kwenye maeneo mengine ya maendeleo.

Viongozi wa dini wawe pia mstari wa mbele kwenye kutoa elimu hii kwenye maeneo yao ili kuifikia jamii kwa ukubwa zaidi
 
Back
Top Bottom