Tutapuuzwa kwa upuuzi wetu itaifa

Ben Saanane

JF-Expert Member
Jan 18, 2007
14,581
18,124
Tutapuuzwa kwa upuuzi wetu kitaifa

Na Ben Saanane


16 Dec 2015

WIKI iliyopita niliandika makala yenye kichwa cha habari "Rais Magufuli na Slack Management Style; Ni utekelezaji mbaya wa ilani ya Ukawa". Ndani ya makala ile nilikosoa mwenendo wa utawala mpya chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa siku 30 alizokaa madarakani.

Nilikosoa vikali utamaduni wa kujirundukia mamlaka na pia kutoa uamuzi na amri zinazoambatana na mtindo wa kuvizia/kushtukiza. Mtindo huo ulioigwa na baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya kiasi cha kufikia hatua ya kuvunja sheria kwa amri zisizo halali, kama za kuweka ndani baadhi ya watendaji kwa makosa ya kuchelewa kufika eneo la kazi unashangaza na kutia aibu utawala unaopaswa kujiendesha kwa kanuni, taratibu na sheria.

Utaratibu huu ni mbovu kwani hauwezi kutoa suluhisho la kudumu bila kutengeneza mfumo au mnyororo imara wa kiuwajibikaji (Chain of Accountability). Kwa mfano, nilisema huwezi kupambana na rushwa kwa kukamata watu wachache na kusamehe wakwepa kodi kwa kuwapa siku saba wawe wamelipa wakati ni wahujumu uchumi.

Ufisadi umekuwa wa kitaasisi. Bila kuimarisha taasisi za kiuwajibikaji kama Takukuru na kuipa mamlaka ya kupambana na rushwa bila kuingiliwa ikiwa ni sambamba na kubadili sheria ili waweze kuwafikisha watuhumiwa mahakamani bila kupitia kwa DPP, hatutafanikiwa.

Niligusia umuhimu wa kuzingatia Ripoti ya Jaji Warioba kuhusu Rushwa ya mwaka 1996. Niligusia kuwa ili kuimarisha utawala bora na kulijenga upya taifa letu ni vyema sasa Rais Magufuli akaonyesha ujasiri kwa kuirejesha Rasimu ya Katiba ya Wananchi kwa kuwa ilikuwa na maudhui na maono ya kuufumua mfumo (system overhaul) na kuijenga Tanzania mpya yenye neema kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kuhusu suala nililogusia juu ya mwenendo wa wakuu wa wilaya na mikoa ambao wanamuwakilisha Rais katika wilaya na mikoa, tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRGG) imelaani hatua zilizoripotiwa kuchukuliwa na baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwaweka selo watumishi ambao wameshindwa kutimiza majukumu yao ya kikazi.

Kwa mujibu wa tamko lililotolewa na Mwenyekiti wa CHRGG, Bahame Nyanduga, kamisheni hiyo ilipokea ripoti ya vitendo vya baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kutoa amri za kuwakamatwa na kuwekwa selo kwa muda fulani watumishi wa umma.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa makosa ya kiutendaji yanapaswa kuchukuliwa hatua za kiutendaji kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma na sio kuwaweka jela kama watu waliofanya makosa ya jinai.

Taarifa hiyo ilitaja baadhi ya matukio ambayo imepokea ripoti zake kuwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuamuru maafisa ardhi waliochelewa kufika kazini wakamatwe na kuwekwa selo kwa saa sita.

Alilitaja tukio lingine kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma kuamuru afisa afya wa kata kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa kosa la kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa maelekezo ya Rais John Magufuli, kufanya usafi katika siku ya kumbukumbu ya Uhuru, Disemba 9.

Kuwapa adhabu za kinidhamu ingekuwa njia bora zaidi kuliko kuwafunga jela kama vile wamefanya jinai.

Nilipokosoa hatua hii ya viongozi hao nilipata mrejesho hasi na chanya kutoka kwa wasomaji wengi wa makala ile. Lakini pia kuna waliomwaga matusi na vijembe vyenye ushabiki wa vyama (partisan). Kwao hawaamini kukosoana kwa hoja bali matusi na vijembe vya mitaani tu.

Hii ni tabia mbaya kabisa ambayo mara kadhaa tumekuwa tukiikemea. Kukosa uvumilivu wa kisiasa (political tolerance) ndiko kunakosababisha mambo ya ajabu kabisa. Unaweza kushuhudia watu wakipigana kwenye vituo vya kuuzia magazeti, watu kukatana mapanga na hata kuuana kwa sababu ya kukosa uvumilivu wa kisiasa tu.

Hali hii inatokea katika dini na hata kikabila. Tabia hii imeshamiri kwa nchi nyingi Afrika. Hatujawahi kuzichukulia itikadi kwa kiwango cha kawaida bali kwa kiwango cha juu kabisa cha uumini hadi kujenga chuki kwa walioko katika mrengo kinzani. Ndipo hapo unapoona kuwa watu wanaweza kuuana katika kugombea haki ya kuchinja ng?ombe au mbuzi.
Ni katika mazingira haya na fikra hizi za hatari tunaendelea kuzalisha chembechembe za ubaguzi ambazo zina uhusiano na uwezo mdogo wa kufikiri.

Uchaguzi Mkuu mwaka huu umetuvua nguo na kutuacha utupu kabisa kama taifa. Kura zilipopigwa utakuta kanda fulani mgombea wake kapata kura nyingi kwa sababu mgombea urais katoka ukanda huo. Sifa za mgombea na sera zinatupwa kando. Ushabiki na ubaguzi umetamalaki. Wagombea na hata watawala kwa kusoma fikra za jamii husika hata mikakati ya propaganda inaelekezwa katika mkondo huo huo.

Viongozi tulionao wanaakisi taswira (reflects) ya sisi wananchi. Ni kioo cha jamii tuliyonayo. Maana viongozi hao wanatokana na sisi wananchi, kwa hiyo ni sura ya jinsi jamii yetu ilivyo.

Ikiwa jamii inaamini kuwa wizi ni sifa, uzinzi, ushirikina na tabia nyingine kama hizo si ajabu kwa jamii hiyo ikawachagua watu wenye tabia hizo kuwa viongozi wake, vile vile jamii inayojadili uadilifu, ucha Mungu, uchapakazi na utawala bora wa sheria itawachagua viongozi wenye sifa hizo hizo.

Wapo hata baadhi ya wasomi, wao wameacha kufikiri kabisa. Wanaamini kuukosoa utawala ni jambo la uhaini (treason). Mtawala anapoonekana akifanya mambo ya ajabu anaweza kupongezwa kabisa na wasomi waoga, wanafiki na walioacha kabisa kufikiri.

Sisi wengine tunaamini katika kusimamia kile tunachoamini. Mfalme akiwa utupu tutamwambia. Kamwe sitamwambia amevaa suti mpya. Nitamwambia hata kama nimezungukwa na maelfu ya watu wanaomshabikia na kumsifia kinafiki kuwa amevaa suti mpya.

Woga na unafiki ndio uliolifikisha taifa hapa. Ni uwoga huu na unafiki uliopitiliza uliowawezesha watawala kujivika mamlaka ya U-Mungu Mtu. Wanaamini wapo juu ya sheria, hawakosolewi wala hawastahili kushauriwa. Wanaamini ni wao pekee wenye uwezo wa kufikiri. Wamejipa mamlaka yanayokaribiana na U-Mungu mtu. Wamepoka haki na mamlaka ya umma hata kama Katiba yetu inasema msingi wa mamlaka yote ni umma.

Rais, wakuu wa mikoa na wilaya wamejiona kwamba wao ndio msingi wa mamlaka yoyote, wao ni mabwana na sio watumishi wa umma.

Nilipoandika kuwa Rais awe mstari wa mbele kutaja mali na madeni yake na pia itungwe sheria ya kuwalazimisha watokapo madarakani au kuachia ofisi vilevile wataje mali na madeni yao, baadhi ya watu walinitumia ujumbe wakisema "kwani unahisi Rais kaiba nini? Maana anachukia mno ufisadi".

Niligundua kuwa watawala wetu kwa kujua fikra (mentality) ya jamii wanayoiongoza waliamua kwenda nayo jinsi ilivyo. Jamii inayopenda matukio, hasa matukio mapya. Jamii inayoamini katika miujiza katika kupata mafanikio au matokeo chanya. Jamii isiyoamini katika uchapakazi, kufikiri kwa kina na kuweka mikakati thabiti ya kisayansi kwa muda mfupi, wa kati na muda mrefu.

Utafiti uliofanywa mwaka 2010 na asasi ya Marekani inayoitwa PEW Research Centre, ulionyesha kuwa asilimia 93 ya Watanzania wanaamini katika ushirikina.

Yaani kati ya nchi 19 za Afrika ambako utafiti huo ulifanyika, Tanzania ilikuwa kinara kwa kuyaburuza mataifa mengine kwa mbali kabisa kwa kuwa na kiwango kikubwa (asilimia 93) cha watu wanaoamini katika uchawi na ushirikina ikifuatiwa na Cameroun yenye asilimia 78.

Hii ni aibu kabisa. Nakumbuka Babu wa Loliondo, Ambilikile Mwasapile alipoibuka na kudai kuwa alioteshwa dawa ya kutibu ukimwi, kansa, kisukari na mengineyo waliibuka wasomi, wanahabari na hata viongozi wakubwa kabisa wa serikali na wa upinzani wakawa mstari wa mbele kushabikia na kufakamia kikombe.

Hata watu waliowahi kuwa walimu wa masomo ya sayansi ya kemikali (chemistry) walikuwa mstari wa mbele kubugia bila kuhoji utafiti wa kisayansi juu ya dawa husika.

Serikali ikawa mstari wa mbele kuweka miundombinu ili kuwezesha misafara ya watu waliofunga safari kunywa dawa ambayo haijathibitishwa. Tena serikali yenye idara inayosimamamia masuala ya dawa na vyakula (TFDA), serikali yenye ofisi ya Mkemia Mkuu ikashindwa kutumia taasisi zake na kuweka msimamo thabiti wa serikali ya nchi inayoendana na karne ya 21 ya sayansi na teknolojia. Ehh, viongozi tulionao ni taswira yetu wenyewe.

Haishangazi sasa kila kona tunakopita vimejaa vibao barabarani vya waganga wa kienyeji. Matangazo yao utaona yanasomeka ?Dk. Bingwa kutoka Kilosanja. Anatoa huduma zifuatazo: Kumrudisha mpenzi wa zamani, kuongeza nguvu za kiume, akili za darasani, kumsahaulisha mdai wako, kuongeza mvuto, kujiunga na freemason, kupandishwa cheo kazini n.k?. Na pengine safari hii huduma inaweza kuongezeka ukasikia ?Kuzuia kutumbuliwa majipu, kuteuliwa ukuu wa wilaya na nyinginezo.

Wateja wa huduma hizi ni jamii ile ile inayoamini katika miujiza,inayoshabikia matukio bila kuyafanyia kazi na kujiridhisha kiutafiti.

Watu hawa wanaamini kwamba taifa imara au hata maisha yao na familia zao yanaendeshwa kwa matukio ya siku husika. Hawaamini kwamba ubora wa maisha yao ya kesho unategemea na mikakati katika kuchapa kazi na kujiwekea malengo. Wanaamini kabisa Rais akifanya tukio la kumfukuza kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali, basi ametekeleza sera ya afya na hivyo tatizo la msongamano wa wagonjwa hospitalini limekwisha au tayari huduma ya kinga ili kuzuia gharama za matibabu imetolewa.

Ukimkosoa Rais kwa uamuzi wake, ukaweka hoja mbadala kwamba Rais anapaswa aimarishe taasisi za utafiti katika sayansi ya afya n.k wataona kama vile unamkosea adabu kupingana na uamuzi wa Rais.

Ni jamii hiyo hiyo inayoamini kwamba hata katika michezo, timu ya taifa itafanya vizuri kwa kumleta kocha kutoka Brazili au Ujerumani kwa vile ni mabingwa wa dunia. Hawaamini katika kuweka programu ya muda mrefu kukuza na kulea vipaji. Wao wanaamini ukimteua kocha ukamlipa mshahara wa shilingi milioni 20 kwa mwezi atafanya miujiza. Ukikosoa uamuzi huo kwa sababu ni jamii hiyo hiyo tuliyoiona ikiamini katika ushirikina na miujiza kwenye nyumba za ibada bila kufikiri, utaonekana mchawi tu. Lakini wakifungwa bao 7-0 na Algeria, kimyaa! Kama vile hawapo!

Tanzania inaweza kufufua ndoto zake ikiwa tutakubali kuwa watafiti, kupunguza unafiki, mihemko, ushabiki na pia ikiwa tutauvaa ujasiri wa kumwambia mfalme upo utupu.

Viongozi wetu wasitumie tatizo hili kwa manufaa yao kisiasa na badala yake wawe chachu ya kubadili fikra za jamii wanayoiongoza. Ndio maana tunasisitiza sana umuhimu wa elimu bora ili tuweze kujenga taifa linalojitambua na ubora wa taifa uonekane katika maisha ya kila siku ya Watanzania katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Nitaendelea kuikosoa, kuishauri na kuifanyia tathmini serikali mpya. Mchango wangu kwa taifa hili nimechagua kukosoa na kushauri, nitapongeza pale panapostahili kwa kuwa uungwana ni vitendo.

Nahitimisha kwa leo!

Mwandishi wa Makala hii Ben-Rabiu Wa Saanane ni Mkuu wa idara ya sera na utafiti CHADEMA, Anapatikana kwa Namba 0768078523

Chanzo: Raia Mwema
 
Sasa hivi tunashuhudia ONE MAN BAND ikitumbuiza! Hakika tunakoelekea ni kubaya sana, eti Rais anaweza kuteuwa Naibu Waziri akakosa Waziri? Hii haijawahi kutokea po pote duniani isipokuwa Tanzania!
 
Asante sana Ben Saanane hofu yangu kubwa sana sana ni siku haya mambo ya Ukanda yanayopaliliwa na CCM yatakaposhamiri na kushika kasi, je wataweza kuiunganisha nchi tena? Maneno yetu yanabeba mustakabali wa nchi yetu.
 
Last edited by a moderator:
Tafuta gazeti lingine la kuweka makala zako, hiyo raia mwema ni sawa na uhuru siku hizi
Kwangu hili ni miongoni mwa magazeti bora machache tuliyonayo. Kabla Sijaamua nichapishe chombo gani huwa natafakari aina ya wanasafu wenzangu. Gazeti lina wanasafu ambao wanafanya uchambuzi wa kina na wa kisomi hata kama chambuzi zao nyingine zinanikera. Sitaki kuandika kwenye magazeti ya kishabiki yenye waandishi wa majungu badala ya kufanya uchambuzi wa kina.

Kuna magazeti ambayo baadhi ya waandishi au wahahriri wanajifanya waandishi wa habari za uchunguzi (Investigative journalism) akini kumbe wanaandika majungu na hakuna qualities zozote za kiuchunguzi.

Kuandikia huko ni kujiweka katika mtego wa kujenga himaya za kimajungu-majungu na kuwalisha wasomaji takataka.
 
Mkuu wa idara ya sera na utafiti chadema pamoja na kujisifu kote umeangukia kwenye kazi isiyo na kichwa wala miguu, ilimradi tu wameongeza mchaga kwenye uongozi wa chama.
 
Nilitegemea kuona analysis ya kitaalam, kuja kugundua kua ulikua ni uchambuzi wenye kuelemea upande wa mleta mada, hizi ni ngonjera na si uchambuzi.
 
Haujui hata unachokitetea utaweza kuandika makala yenye TBS?

Unatupotezea muda.
 
Sasa hivi tunashuhudia ONE MAN BAND ikitumbuiza!!! Hakika tunakoelekea ni kubaya sana, eti Rais anaweza kuteuwa Naibu Waziri akakosa Waziri?! Hii haijawahi kutokea po pote duniani isipokuwa Tanzania!
sio kila kitu tuige kwa wazungu vingine wanaweza iga kwetu, maana mmekariri sisi ni lazima tuige, wenyewe wanamsifu we unaponda. Hata huyo uliyekuwa unamtaka asingeweza fanya yanayofanyika leo
 
Mtoa mada hongera, umeeleza kwa lugha na mifano rahisi tu hata mtoto wa darasa la saba atakuelewa.
 
Hili la Babu wa Loliondo unanikumbusha mbali-Leo hii Raisi JP anaweza kweli kusema neno kuhusiana na Babu wa Loliondo?
Ilishangaza kuona mtu aliyebobea katika masuala ya Kemia akibugia kikombe bila kujiuliza mara mbili mbili.
 
Sijui kwanini huwa sisomi siredi zako, nimeingia kujaribu najikuta nasepa tena nikaamua kukusalimu kidogo.
 
unapokosoa pia kubali kukosolewa.

hebu jiulize katika mazingira corrupt, kila unayempatia fedha kutekelezajambo Fulani corruption inaigia kwa wtu watu kuweka maslahi yao mbele. kila utakayeuagiza kuunda taasisi Fulani corruption inaingia na kunaundwa taasisi feki zisizo timiza malengo hayo unaoyasema yanaweza kufanyika vipi?.

kwa maoni yangu nadhani raisi yuko sahihi kwa kuakikisha watendaji anaowatuma utekeleza hayo unayoyasema wanakuwa serious na majukumu yao then kila kitu kianyooka.

lakini kwa approach yako mimi nadhani nothing can be done kwa maana corrupt government haiwezi kufanya unayoyasema, serikali iliyoundwa na wazembe haiwezi kufanya unayoasema.

utafiti unatakiwa kujikita katika kuangalia mtatizo yaliyopo na njia za kutatua kwa kuangalia changamoto zilizopo kwenye utatuzi. hivyo kukimbila kuunda taasisi zisizoweza kufanya kazi kutokana na watumishi walioko kenye sytem, haina maana badala yake kurekebisha watumishi hawa ili maagizo watakayokuwa wakipewa au ili waweze kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa ndio first priority.

kwa utagulizi umesema raisi anatekeleza sera za ukawa lakini hukubaliani na anachokifaya, ukitaka akifanye kivingine hiyo ni kuonyesha hatekelezi sera zako bali kwa kuwa nyote mmejikita katika kutatua changamoto za jamii moja mtashughulikia matatizo yaleyale ila kila mmoja kwa approach tofauti na hizo ndizo sera.

mwisho nadhani kukaa kichwani kwa raisi huyu ambaye anayoyafanya mpaka sasa yamewaridhisha wengi ili ionekane anakuiga au unaweza zaidi yake inahitaji uwe smart sana tofauti na hapo unaweza kuonekana kituko. ni vizuri kusoma game vizuri na kujua staili ya kuingia nayo awanjani kwa makini.
 
Ben nilisoma makala yako ya wiki iliyopita na pia ya wiki hii kwenye gazeti la Raia mwema.

Kwangu mimi makala zimejitosheleza na kwa hakika nakupongeza kwa maandishi yako.

Bahati mbaya ni watu wachache sana watakaosoma maandishi hayo kwa fikra huru bila kuongozwa na uvyama,ukanda n.k.

Lakini haidhuru ili mradi umetimiza wajibu wako kwa nchi yako bro.

Salute!
 
Thanks Ben. Sababu kuu za ushirikina wa kupindukia (maana hata huko kulikoendelea uko kwa kiasi) ni uhaba wa elimu, kukata tamaa, ukosefu wa miundo afya ya kisasa au kutomudu gharamaze.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom