SoC03 Turuhusu uhuru wa habari utuwajibishe

Stories of Change - 2023 Competition

Samahani

JF-Expert Member
Oct 29, 2018
222
335
Utangulizi

Binadamu tumeumbwa na tabia ya “kushangaa”. Tunayoyaona au kuyasikia kwa mara ya kwanza yanatushangaza. Tunaposikia au kuona jambo ambalo hatuna taarifa zinazolihusu, ni kawaida “kushangaa”. Baada ya kuwa na ujuzi juu ya jambo hilo, halitushangazi tena. “Tutakushangaa” utakaposhangazwa na jambo ambalo una ufahamu nalo.

Lakini, tunaendelea “kushangazwa” na mambo yaleyale. Mojawapo kati ya jambo linalotushangaza mara kwa mara ni “uwajibikaji”. Tunapopata mrejesho juu ya uwajibikaji katika taasisi mbalimbali za kidini, kijamii, kiserikali au uwajibikaji wa mtu mmojammoja, “tunashangaa”.

Mathalani, mrejesho kutoka ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kila mwaka umekuwa na mengi “yanayotushangaza”. Wakaguzi wa ufanisi wanapotutembelea maofisini, hutoa mrejesho “unaotushangaza”. Tume mbalimbali zinazoundwa kupima uwajibikaji wa kitaasisi au wa watendaji, zimekuwa na majibu “yanayotushangaza”.

Uhuru wa habari na uwajibikaji

Kushangaa kwetu ni uthibitisho kuwa, bado hatuna “taarifa” juu ya yanayofanyika. Uwajibikaji unapimwa kwa uwazi! Taasisi na hata mtu mmojammoja anayewajibika anapimwa kwa matokeo ya kile anachokifanya. Uwajibikaji, ingawa unaweza kuonekana moja kwa moja, unapewa nguvu zaidi kwa kutolewa taarifa! Kizuri kinajiuza kwa habari za uzuri wake kuwafikia wengine. Hivyo, ili kupata mrejesho juu ya uwajibikaji, ni lazima tupate taarifa kwa wakati

Tunatarajia kupata taarifa kupitia vyombo vya habari vinavyoendeshwa kwa uhuru, vikifuata misingi na maadili, vinavyotusaidia kuhifadhi taarifa zilizopita na kutupa taarifa za sasa. Mlinganyo huu ni muhimu katika kufanya maamuzi kwa uadilifu ili kuepuka uwajibikaji hafifu. Vyombo vya habari vinafichua dosari katika uwajibikaji binafsi na wa kitaasisi. Vinapokuwa huru, vinaifanya jamii kuwa na taarifa muhimu wakati wote.

Taasisi na watendaji wanapaswa kujua wajibu, haki na mipaka katika utendaji wao. Hapo ndipo kilipo kiini cha uwajibikaji wenye tija. Kwa kujua haya, kila mtu na taasisi itajituma kuhakikisha kuwa, uwajibikaji ni “lugha inayoeleweka” kwa pande zote, mtoa huduma na mpokea huduma.

Hali ya uhuru wa habari nchini

Tumeendelea kuzisikia kelele za kuulilia uhuru wa habari licha ya kuwepo maridhiano ya kimikataba, sheria ya vyombo vya habari na maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari ifikapo tarehe 3 Mei. Mwaka huu, maudhui ya siku hii yalikuwa “kuumba mustakabali wa Haki: Uhuru wa kujieleza kama kichocheo cha haki zote za binadamu”. Kumbe, hata baada ya miaka thelathini ya maadhimisho haya, bado tuna kazi ya “kuumba mustakabali wa haki”, hasa ya kujieleza!

Mwaka 2022, waandishi wa habari barani Afrika walikutana jijini Arusha kujadili juu ya “usalama wa waandishi wa habari”. Mwaka mmoja kabla, Mei 2021, katibu Mkuu wa umoja wa mataifa katika siku hii alizihimiza serikali “kufanya kila lililo ndani ya uwezo wao kusaidia uhuru wa vyombo vya habari”.

Hatujafikia bado lengo la kuwa na uhuru wa habari. Hii inadunisha uwajibikaji kwa kuwa, maovu yanayoendelea katika utendaji yameendelea kuwa “siri” inayotushangaza popote inapogundulika, tena mara zote kwa kuchelewa!

Taasisi zetu nyingi zimeendelea kusemwa vibaya kutokana na vitendo vya rushwa, uduni wa huduma, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhilifu mkubwa wa rasilimali na kashfa nyingine zinazofanana na hizi. Lakini, vyombo vya habari bado vinawekewa mipaka katika kupata na kutoa habari katika maeneo haya. Bado majibu yanayoudhi na vitisho vinatolewa tena na wale wanaohusika moja kwa moja!

Usalama wa waandishi wa habari hasa za kiuchunguzi umeendelea kuwa hatarini. Hii inachangia kuwa na waandishi wachache walio tayari kuutafuta ukweli hata katika hatari ya kifo! Gharama za upatikanaji na utoaji wa habari ni mzigo ambao haubebeki kirahisi. Mapinduzi makubwa ya kiteknolojia katika habari, badala ya kurahisisha upashanaji wa habari, yamekuwa mzigo wa gharama kubwa ambazo si rahisi kwa wengi kuzimudu.

Kwa hali hii, tunaamua wenyewe kuuondoa uwazi katika utendaji, na matokeo yake, taarifa za uwajibikaji duni zimeendelea kutushangaza kila siku.

Nini kifanyike?

Mei 2 2019, katika kuelekea siku ya uhuru wa vyombo vya habari, katibu mkuu wa umoja wa mataifa alibainisha kuwa, “vyombo vya habari ni muhimu kwa amani, haki na maendeleo endelevu na haki za binadamu”. Uwajibikaji na haki za binadamu vinachochewa na uwepo wa haki ya kujieleza. Kuupunguza na kuuwekea vikwazo vya aina yoyote uhuru huu, kunaondoa nafasi ya kutoa na kupokea maoni yenye kulenga kuboresha uwajibikaji.

Yafuatayo yawe miongoni mwa vipaumbele ili kuimarisha uwajibikaji.

  • Taaluma ya uandishi wa habari ipewe kipaumbele kwa kuwapa motisha wale wanaojifunza au kujiendeleza katika taaluma hii, tuwaandalie mazingira rafiki na wezeshi ya kujifunza na kufanyia kazi. Tuwe na bodi za ukaguzi wa ufanisi kama ilivyo kwa taaluma nyingine. Hii itachochea zaidi kuwa na waandishi wanaotafuta na kufikisha habari zinazolenga kuchochea uwajibikaji huku wakilinda maadili.
  • Sera ya utoaji wa habari iwe ni ya lazima katika taasisi zote zenye usajili. Wakati wa kusajili au kuhuisha taarifa zetu za kitaasisi, sera ya utoaji na upokeaji wa habari liwe takwa la lazima! Niliwahi kuajiriwa na taasisi ambayo, uongozi wa taasisi uliweka masharti mpaka katika makundi sogozi ya kijamii hasa “whatsapp”! Uongozi ulilazimisha kuwepo katika makundi yote ili “kuthibiti” mijadala inayoendelea! Hii ndio hali halisi kwa taasisi nyingi! Ni wakati wa kuwa na sheria inayolazimisha kila taasisi kuwa na sera ya uhuru wa utoaji wa habari, na pia, kuwa na msemaji mwenye taaluma ya habari. Huyu atawajibika kutoa habari zote muhimu zinazoihusu taasisi.
  • Sheria zinazoweka mipaka kwa wanahabari zisiendekezwe. Kumekuwa na mapitio na maridhiano “kwenye makaratasi” kadhaa yanayolenga kuleta uhuru zaidi kwa vyombo vya habari ingawa hatujaamua kuyabadili kuwa vitendo.
  • Gharama za upatikanaji na ufikishaji wa habari zipunguzwe. Sekta zote zinazopewa bajeti ya kujiendesha ziwe na fungu kubwa katika kutoa habari na mrejesho wa utendaji. Mkulima apewe mrejesho kwa wakati juu ya alichoahidiwa kwenye bajeti ili amuwajibishe bwanashamba ambaye hafiki kumpa elimu juu ya kilimo cha kisasa.
  • Vyombo vya habari vifanywe kuwa rafiki. Waandishi wa habari wamepewa majina yanayolenga kuwadhalilisha na kuwakatisha tamaa. Wamefanywa “maadui” badala ya kuwa sehemu muhimu ya kufikisha habari zinazolenga kuchochea tija katika uwajibikaji. Sheria iwalinde waandishi wa habari. Mambo mengi yanayoibuliwa na “kutushangaza”, yanaibuliwa na waandishi wa habari makini na wanaolenga kuchochea uwajibikaji. Kuwateka, kuwaua au kuwaziba midomo kwa namna yoyote ile ni kuendelea kudunisha uwajibikaji
  • Upatikanaji wa habari uwe sehemu huduma za jamii. Kama vile tunavyowekeza katika afya, maji, miundombinu na elimu, serikali ikubali kuwa sehemu ya upatikanaji na usambazaji wa habari. Katika mataifa yaliyowekeza vema kwenye upatikanaji wa habari, magazeti na majarida vimeendelea kupatikana kwa wingi kwa gharama nafuu. Tuwape ruzuku na motisha waandishi wa habari wakiwepo wale wa binafsi na kuhakikisha kuwa, habari zinafika kwenye jamii kwa wakati.
  • Vitisho kwa wanahabari vitafutiwe adhabu zinazostahili. Mwandishi wa gazeri la Raia Mwema, Manga Msalaba aliwahi kutoa ushuhuda wa kutishiwa alipokuwa akifuatilia kupungua mapato ya mkoa wa Mwanza na kujibiwa kuwa, (nanukuu) “kijana jiangalie usijekuwa umeanza kwa mguu mbaya kuja kwangu” (Chanzo Initiative, 18/05/2023). Niliwahi kutembelea ofisi za idara ya kazi ili kufikisha malalamiko ya kuwepo kwa ofisi isiyokuwa tayari kutoa mikataba ya kazi huku ikiwafukuza waajiriwa bila kufuata sheria za kazi. Afisa mmoja baada ya kueleza nia yangu akanionya kuwa, “najua tu unataka ukaanze kututangaza. Kinachowaponza wengi wenu ni kutokujua kuwa kuna maelekezo huwa yanatoka msikokujua”. Vitisho vya aina hii ni kilio cha kila mpenda uhuru wa habari. Ni wakati wa kuvitambua kama vitisho juu ya uhai wa habari na hata uhai wa waandishi na vyombo vyao
Hitimisho

Falsafa ya kuwa hakuna uhuru usio na mipaka hauondoi ukweli kuwa, mipaka hii haipaswi kuwa yenye kunufaisha upande mmoja. Wanaoitumia falsafa hii huitumia wanapoguswa katika nyakati ambazo kuna habari mbaya zinazohusu uwajibikaji wao. Wanapokuwa katika mazingira ya kupongezwa, uhuru huu huwa hauwekewi mipaka! Tukubali uhuru wa habari uingilie uwajibikaji wetu. Palipo na makandokando, turuhusu yawekwe wazi ili iwe ni kumbukumbu nzuri kwetu ya kuboresha utendaji kwa siku zijazo. Tuondoe mipaka yote yenye ukakasi juu ya upashanaji wa habari. Tuwajibike kwa kuwapa uhuru wa kutosha raia, wadau na taasisi kutoa na kupokea habari kwa uhuru.
 
Tatizi hii dunia ni mpya hadi kwa wanaoitengeneza (mapapa), cha msingi ishi wewe dagaa
Lakini naamini inawezekana kujenga uwazi katika upashanaji wa habari. Hao ambao, labda, tumewapachika au wamejipachika"UPAPA" watambue kuwa, uhuru wa habari hata wao wanauhitaji sawasawa na hao walio "dagaa", na pengine, wao zaidi
 
Back
Top Bottom