Turudishe mijadala ya Richimond, EPA, Dowans kwa vile tunayo tume ya kuanzia na wahusika wako

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482



Deogratius Temba

MKUTANO wa saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliomalizika wiki iliyopita umeacha historia nyingine baada ya kuhitimishwa bila kuhitimisha hoja za msingi zilizokuwa na masilahi kwa taifa.
Jukumu kubwa la Bunge ni kutetea, kulinda rasilimali za Taifa na kudai uwajibikaji kwa waliopewa dhamana na wananchi.
Mawaziri wanapotuhumiwa kuwa wameshindwa kazi, wameshirikiana na wezi kuiba rasilimali za wanaanchi na kuwasababishia wananchi umasikini na matatizo makubwa wanapaswa kuwajibishwa na Bunge ambalo ni chombo cha wananchi.
Mkutano wa Bunge uliopita ulikuwa na nafasi kubwa ya kuhakikisha Mawaziri wanajiuzulu wakiwa Dodoma na si Dar es Salaam, lakini kutokana na mfumo mbovu wa Bunge, kiti cha Spika na mamlaka za uteuzi huu umekuwa ni mchezo wa kuigiza. Bunge likageuzwa kuwa ‘ze comedi’.
Baadhi ya Watanzania hawakuona ni busara kumaliza mkutano huo uligharamiwa na fedha za kodi zao bila kujadili juu ya wizi unaofanywa na watendaji wakuu wa serikali, au kuwachukulia hatua wahusika. Kusema kuwa mamlaka zinazohusika zifanya kazi ya kuwaadhibu haina maana.
Watanzania walitegemea kuwa Bunge lingesimamia kikamilifu kushinikiza uwajibikaji na kuchukuliwa sheria kwa mawaziri walioliibia taifa au waliosababisha taifa hili kufikia hapa lilipo.
Tunaona jinsi ambavyo hali ya uchumi imezidi kuwa mbaya, mfumko wa bei imekuwa mara dufu, thamani ya shilingi imeshuka, ugumu wa maisha umeongezeka, najiuliza hivi kama wenye kazi tunalalamika kiasi hiki je wasio hata na kibarua cha kufyeka nyasi hali ikoje?
Kuna watu wasio na uhakika na mlo mmoja kwa siku, viongozi wetu wao, rasilimali zipo lakini haziwanufaishi walio wengi kwasababu wenye dhamana ya kuzigawa na kuweka mipango mizuri wameamua kuweka masilahi binafsi mbele.
Viongozi wetu wamezipa kisogo shida za wananchi, wanashirikiana kuzihujumu rasilimali za taifa kwa masilahi ya wachache ambao wanaishi kama wapo peponi.
Watanzania walitarajia wawakilishi wao (wabunge) wawe wakali kwa wabadhirifu hasa mawaziri waliopewa dhamana ya kuongoza wizara husika, mbunge anayeshindwa kukidhi kiu ya yule anayemuwakilisha hafai kuwepo bungeni.
Hatutegemei wabunge waliopewa mamlaka kisheria ya kumwondoa Rais au Waziri Mkuu madarakani washindwe kufanya hivyo baada ya kujiridhisha utendaji wa viongozi hao si wa kulikomboa taifa kwenye lindi la umaskini.
Wananchi tulitegemea bunge lingeahirishwa baada ya hoja za msingi kufikia mwisho, lakini limeahirishwa kwa namna isiyotarajiwa. Mfano: Hoja ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Richmod na nyinginezo hazikufikia hitimisho lenye masilahi kwa taifa.
Hii ni nchi gani tunaijenga? Je, kwa jinsi hii tutafika? Mamlaka ya Rais ambayo ni ya uteuzi imeshindwa hata kuwawajibisha mawaziri husika, je, kiti cha rais au ofisi yake ikifanya makosa inaweza kuwajibika? Hapa tunaona jinsi ambavyo baba akiwa si mwajibikaji anashindwa kusimamia uwajibikaji kwenye familia.
Wanaotuhumiwa kuwa ni wabadhirifu hivi sasa wanaendelea kukuza sauti za kuwataka wawajibike, wanakejeli na kudhubutu kusema ni “upepo” unapita. Hii ni dharau kwa wananchi. Hatuhitaji serikali ya kuwadharau wanachi wake vile.
Matatizo tuliyonayo ya kukosekana kwa uwajibikaji ni ya kimfumo, hata hivyo tuna tatizo zaidi la viongozi wakuu wanaosimamia mifumo hiyo mibovu. Waziri Mkuu wa nchi yetu hana mamlaka ya uteuzi kama aliyonayo rais.
Kwa muktadha huo Waziri Mkuu hawezi kuwafukuza kazi mawaziri bali atamshauri ‘bosi’ wake ambaye rais atakayekuwa na hiyari ya kukubali au kukataa ushauri aliopewa kulingana na mazingira.
Inapofikia hatua ya mawaziri kuguswa na kashfa mbalimbali na wao wakagoma kung’atuka na aliyewateua haonekani kuwachukulia hatua basi rais ndiye wenye matatizo na kuna haja wabunge kuangalia namna ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais.
Katika makala zangu huko nyuma, nimesema kuwa Tanzania tuna ombwe la uongozi kwa sababu ya taasisi ya urais yenye madaraka makubwa lakini yanatumika kulea baadhi ya watendaji wazembe, wabadhirifu na wafitini.
Rais hawezi kukwepa lawama za watendaji wabovu walio chini yake, kwasababu yeye ndiye aliyewateua na ndiye mwenye mamlaka ya kuwawajibisha pindi anapoona mambo hayaendi vizuri.
Mara kadhaa watu mbalimbali wamemshauri Rais avunje Baraza la Mawaziri na afanye mabadiliko makubwa katika utendaji serikali ili kuleta tija lakini ushauri huo hakuupa uzitounaostahili mpaka hivi sasa mambo yamekuwa magumu ndiyo anaamua kulifanyia mabadiliko.
Mwaka 2007 rais alipuuza kelele za wananchi kupitia vyama vya upinzani, mawaziri, makatibu wakuu waliokuwa mafisadi walitajwa waziwazi kwenye orodha ya mafisadi Septemba 15 pale Mwembeyanga, hakuwachukulia hatua, mawaziri, wakapuuza wakasema ‘kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala.’
Kinachonisikitisha ambacho nimekieleza ni kuacha mambo katikati, baada ya Mwembe Yanga na hatimaye maazimio ya Bunge ya Richmond 2008, taarifa ya kamati ya 'Bomani', Timu ya Rais ya 'EPA' na nyingine operesheni uwajibikaji iliendelezwa lakini mijadala ikafungwa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010; na sasa imeanza mijadala mipya.
Tunapaswa kufungua mijadala ile iliyofungwa kinyemela na kuichanganya na mijadala hii ya sasa ikiwa tunataka kusimamia uwajibikaji mpana na mabadiliko makubwa ya kimfumo katika taifa letu.


 
Back
Top Bottom