Tundu Lissu: Naomba nitofautiane hadharani na Mwigulu Nchemba kuhusu suala la wakurugenzi kusimamia uchaguzi

mwakajingatky

JF-Expert Member
May 30, 2018
555
909
Anaandika Tundu Lissu

Huwa sina tabia ya kujibizana hadharani na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa sababu, tofauti na wengi wengine, ninafahamu na kuheshimu msimamo wake, japo wa mafichoni.

Kwenye hili la wasimamizi wa uchaguzi, hata hivyo, naomba kutofautiana naye hadharani.

Suala la wasimamizi wa uchaguzi kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa sio suala 'mufilisi' kabisa. Suala hili ni amri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Ibara ya 74(14) ya Katiba hiyo inaamrisha kwamba
" *itakuwa ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa...."*

Katiba imewataja watu hao 'wanaohusika na uchaguzi' kuwa ni pamoja na *"wasimamizi wote wa uchaguzi wa miji na Wilaya zote." (Ibara ya 74(15)(e).*

Kwa Sheria ya Uchaguzi, 1985, wakurugenzi wote wa majiji, miji na wilaya ndio wasimamizi wa uchaguzi katika nchi yetu. Katika masuala ya uchaguzi, haki pekee waliyo nayo watu hao, kwa mujibu wa ibara ya 74(14), ni haki ya kupiga kura tu.

Wasimamizi wa uchaguzi hawa ni maafisa wa Tume ya Uchaguzi sio kwa kuteuliwa, bali by operation of the law. Wamelazimishiwa Tume, sio kwa mapenzi ya Tume, bali kwa shuruti ya Sheria ya Uchaguzi.

Hata hivyo, bado wanabanwa na amri ya ibara ya 74(14) na (15) ya Katiba. Ni marufuku kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.

Isingekuwa tuko kwenye Tanzania ya Magufuli ningeona ajabu kwamba mtu ambaye, kama Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, amewahi kushikilia madaraka makubwa kama ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, anaweza kuwa kwenye giza nene kiasi hiki juu ya matakwa ya Katiba ya nchi yetu.

Lakini tuko kwenye Tanzania ya Magufuli ambayo kwayo Katiba na Sheria za nchi ni makaratasi tu. Kwa Tanzania hii, Katiba na Sheria halisi ni kauli na matamko yanayotoka kwenye kinywa cha mtukufu Rais.

Na kwa sababu hii tu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ni mtu wa kusamehewa, kama sio wa kuonewa huruma, kwa sababu na yeye pia ni mhanga wa Tanzania ya Magufuli.

Hoja ndogo ya mwisho kuhusu suala hili. Sio tu kwamba Rais Magufuli amekiuka Katiba na Sheria ya Uchaguzi kujaza makada wa CCM kwenye uongozi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa, bali pia katika kufanya hivyo, Rais amenyakua madaraka yasiyokuwa yake.

Sheria yetu ya Utumishi wa Umma imeweka wazi utaratibu na mamlaka ya kuteua wakurugenzi wa Halmashauri hizo. Mamlaka hayo ni ya Tume Kuu ya Utumishi wa Umma, kwa kupitia Tume ya Utumishi wa Serikali za Mitaa.

Na wanaotakiwa kuteuliwa kuwa wakurugenzi wa Halmashauri hizo ni watu walioko kwenye utumishi wa umma, sio makada wa CCM waliokosa ubunge. Kama hili nalo halieleweki kwa akina Mwigulu Nchemba basi tuna tatizo kubwa kuliko tunavyofikiri.

Wasalaam
TL
 
Kuna watu wapo kwa ajili ya kupotosha hata yaliyoandikwa kwa lugha nyepesi katika Katiba na sheria zetu kama hili. Magufuli alipokuwa anakiuka sheria za Utumishi kwa kuteua maDED ambao hawajawahi kuwa watumishi ilionekana vema kwa CCM kwa sababu angalau ilikuwa inawapunguzia joto la kisiasa wabunge walioshinda wa ccm kwani wapinzani wao waliowashinda kwenye kura za maoni ndani ya chama chao walikuwa wanapata ajira bwelele na hivyo kujipoza kwa cheo kipya. Lakini bila kujua kama Taifa tunatengeneza mgogoro wa Kikatiba kwani hawa Makada kwa nafasi yao ya DED ni wasimamizi wa uchaguzi na katiba inazuia makada wa Chama chochote kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Katazo hili anayelipinga anafanya makusudi kujitoa akili kwani ushahidi usio shaka katika chaguzi mbali mbali maDED wamewahi kuwa chanzo cha vurugu na kupelekea wananchi waliodhulumiwa haki yao ya kuchagua kujichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto majengo au magari (Ref.Shinyanga & Mbozi). Sishabikii vurugu lakini Refa asiyetenda haki anakera na anaamsha hasira isiyoweza kuzuilika. Nahitimisha kwa kuwaasa wanasiasa ndani ya CCM kutopinga maamuzi yanayoiletea heshima nchi hata kama yanasababisha kupunguza mbeleko kwa chama chao.
 
Sitaki kuamini kuwa Mwigulu halijui hili,nadhani manzingira yanamlazimisha awe hivi. Nataka niseme mkifika mahali na kuanza kuiona katiba kama makaratasi tu basi nyinyi wenyewe bila shuruti ya mtu mtakuwa mmechagua njia ya uharibifu.

Sheria na katiba ndo zinaweka ustarabu katika nchi ,kinyume na hapo ni kutafuta mafarakano.
 
Back
Top Bottom