Uchunguzi wa miili ya maiti wanne waliopigwa risasi na askari polisi katika Mgodi wa African Barrick North Mara uliofanywa na daktari bingwa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Makatta imebaini kuwa marehemu wote walipigwa risasi maeneo ambayo hayakulenga kujeruhi, bali kuua.
Uchunguzi huo uliochukua saa 4:27 ulianza saa 5.20 asubuhi hadi saa 9.47 alasiri. Upande wa familia za wafiwa ulisimamiwa na Dk Greyson Nyakarungu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Tarime na askari wawili. Taarifa hiyo itakabidhiwa kwa hospitali
Source Mwananchi
Dk Nyakarungu alisema Emmanuel Magige mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari namba za PM1/5/2011 (TGH), alipigwa risasi katika nyonga ya kushoto ambako kulikuwa na tundu la duara llilokuwa na upana wa sentimita 0.5 ilipoingilia na sentimita 2.5 ilipotokea.
Mishipa ya damu iliharibiwa, kibofu cha mkojo, mishipa ya fahamu, mfupa wa nyonga ulisagika, damu ikavia ndani ya tumbo, lakini chini ya mgongo karibu na risasi ilipotokea kulikuwa na tundu linaloonyesha kuwa alichomwa na kitu chenye ncha kali kama singa ya bunduki, alisema na kuongeza:
Tumebishana sana kwa hilo wenzangu wakidai huenda aliangukia kitu kikamchoma, ikumbukwe kuwa alipigwa kwa nyuma akikimbia hivyo asingeweza kuanguka chali zaidi ya kifudifudi, alisema.
Kuhusu Chacha Ngoka mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari PM 2/5/11 (TGH), uchunguzi ulibaini kuwa alipigwa risasi mgongoni karibu na kiuno na kutokea katikati ya mbavu chini ya titi, tundu la kuingilia likiwa ni sentimita za duara 0.3 na ukubwa wa tundu pa kutokea ikiwa ni sentimita tano.
Mishipa mikubwa ya damu iliharibiwa, ini likasagwasagwa, damu iligandia kwenye mfumo wa upumuaji hali ambayo inadhihirisha kuwa alipumua kwa nguvu, damu ilikwisha mwilini na kuwa alipigiwa risasi kwa mbali.
Alisema marehemu Bhoke mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari PM/3/5/11(TGH) alipigwa risasi ya kichwani karibu na sikio na kidonda chake pakuingilia ni sentimita za duara 0.2 ,pa kutokea sentimita tano za duara kwenye paji la uso hivyo kuharibu ubongo, fuvu na mifupa yote kubomolewa.
Kuhusu uchunguzi wa Mwikwabe Marwa Mwita mwenye jalada la uchunguzi wa kidaktari PM/4/11 (TGH) alisema alipigwa risasi karibu na nyonga na kuacha tundu la sentimita za duara 3,5 na risasi haikutoka nje na kuharibu mifupa yote ya nyonga, misuli ikawa imeharibiwa na kipande cha risasi kilikutwa katikati ya misuli (PSOAS), damu ikiwa imevia tumboni.
Kilichoonekana hapo ni kuwa walipigwa risasi kwa mbali tena kwa nyuma maana wote zimeingilia kwa nyuma na maeneo waliyopigwa risasi ni yale ya kuua si kuwapunguza nguvu kama walikuwa wamegoma kusalimu amri, alisema daktari huyo.