Tuna uwezo wa kubadili taifa hili tukiamua ( my speech)

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
Mabibi na mabwana taifa letu linapitia katika kipindi chake kigumu na katika kipindi hiki tunahitajika kutafakari kujua nini changamoto zetu na suluhisho la changamoto hizo. Changamoto hizi tunapaswa kukabiliana nazo kwa pamoja kama taifa. Changamoto hizi zinahitaji busara na hekina kuzitatua. Nchi yetu kwa sasa imekosa mwelekeo na dira. Umoja wa nchi umetetereka, nchi imekosa malengo ya pamoja. Ufisadi na wizi wa mali za umma umeongezeka kwa kasi. Wanasiasa wetu wamekuwa wabinafsi kupita kiasi na wenye kujilimbikizia mali na kusahau raia. Siasa zetu zimekuwa za ulaghai, uongo na fitna na jamii zetu zimeanza kujengeka hivyo. Maadili yetu kama taifa yameshuka kwa kasi kubwa. Watu wanatumia ofisi za umma kama mali zao binafsi. Na sasa tumekuwa taifa la wabinafsi na tumekosa dira ya pamoja kama taifa. Katika hali hii tunahitaji kutafakari kwa makini. Elimu yetu imeshuka kwa kiwango kikubwa na imekuwa haina misingi ya utaifa. Tunahitaji kulinyanyua upya taifa letu. Tunahitajika kubadili mitazamo ya watu wetu kutoka kwenye ubinafsi kuja kwenye utaifa.

Swali la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza na kutafakari kila wakati ni Tanzania ya namna gani tunataka kuijenga kwaajili yetu, watoto wetu na kizazi chetu kijacho. Ni muhimu na ni lazima tuwe na taswira ya nchi ambayo tunataka kuijenga ambayo huenda isikamilike sasa lakini matunda yake yakaonekana miaka ijayo lakini ujenzi wake tunawajibika kuuanza sasa na kuendelea nao kizazi hadi kizazi. Ni lazima tuwe na '' idea'' ya aina ya taifa tunalotaka kulijenga na tuwe tayari kizazi hadi kizazi kufanya kazi ili kukamilisha idea hiyo. Kazi hii inawezekana kama tutafanya juhudi za pamoja na kama tunajua ni wapi tunataka kuelekea kama taifa. Ni lazima tujue ni wapi tunataka kufika kama taifa. Ni lazima tufuate njia inayotupeleka sehemu fulani na sio njia ambayo haitotupeleka popote. Kama taifa ni lazima tuwe na uelekeo na hiyo ndio kazi ya kiongozi. Kwahiyo ni lazima tuwe na idea na hiyo idea lazima ifanyiwe kazi kizazi hadi kizazi ili ikamilike. Na watu wetu lazima waamini katika hiyo idea. Kazi ya ujenzi wa taifa sio kazi ya mtu mmoja au wawili au ya serikali ni kazi ya watu wote ni kazi ya raia wote. Na watu hawa lazima waunganishwe na ''idea'' na wafanye kazi kutimize hiyo idea. Kwahiyo ni muhimu kwa taifa letu kuwa na idea au taswira ya wapi taifa letu linapaswa kufika na kuwa tayari kufanya kazi kufika huko. Kama taifa ni lazima tuwe na malengo ya pamoja. Ni muhimu sana. Kwahiyo kiongozi wetu lazima awe na uwezo wa kuunganisha watu na kuwafanya wawe na malengo mamoja kufanya kazi na kuendeleza taifa lao.

Matatizo yote ambayo tunayo kwa sasa kama taifa kama hatutakuwa wamoja itakuwa ngumu sana kwetu kuyatatua. Ili tuyatatue matatizo tuliyonayo ni lazima tuwe wamoja na ni lazima pia tufanye kazi kwa pamoja kukabiliana na changamoto zote ambazo zinatukabili. Ni lazima tujitolee kwa pamoja. Ni wakati sasa kwa watu wetu kufikiria kuhusu utaifa na kama tunataka kuwa taifa kubwa hatuna budi kufikiria utaifa.

Nchi yetu inaumwa ugonjwa unaoitwa ubinafsi na inahitaji tiba ya haraka sana. Ubinafsi umetugawa na kuondoa utaifa wetu na kudhoofisha nguvu yetu kama taifa. Tunahitaji tiba ya haraka. watu wetu lazima wafanye kazi kwaajili ya taifa lao. Watu wetu lazima walipende taifa lao na wawe tayari kulitumikia. Ni wakati sasa wa kuondoa magenge yaliyopo na kufanya taifa hili kuwa moja. Ni wakati sasa wa kujenga jamii zetu upya na kuunda upya siasa zetu. Mambo haya yakiimarika uchumi wetu utaimarika pia. Panapokuwepo uongozi mzuri uchumi wa nchi lazima utaimarika. Uongozi mzuri hudhibiti rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma. huleta watu katika malengo mamoja. Uongozi mzuri uhamamisha watu kupenda taifa lao na kuwa tayari kulijenga. Uongozi mzuri ukiwepo taifa huwa hai na lenye matumaini. Uongozi mzuri hauna siasa zenye kugawa watu. Kama taifa tunapaswa kufikiri sasa ni wapi tunapaswa kuelekea na nafasi yetu ni ipi katika dunia hii. Mioyo yetu na akili zetu ni lazima iwepo katika taifa hili. Ni lazima tuwekeze mioyo yetu kwenye taifa hili na ni lazima tufanye kazi ili taifa hili liendelee. Na watu ambao wenye uwezo wa kubadilisha taifa hili ni nyinyi, hili ni jukumu lenu. Viongozi peke yao hawawezi kubadilisha nchi hii bila ya kuwepo raia wanaojitambua ambao wako tayari kulilinda na kulitumikia taifa lao.

Vijana wa taifa hili lazima wajue sisi sio wamarekani, sisi sio waingereza, sisi sio wakenya, sisi ni watanzania. Ni lazima tujitambue kama watanzania. Tuwe tayari kulitumikia taifa hili na kulinyanyua. Kwasababu bila kujitambua kwetu sisi ni kina nani hili taifa haliwezi kwenda mbali. Huu ni ukweli ambao wote tunapaswa kuuzingatia. Tunahitaji kuwa wamoja kama taifa ili kukabiliana na changamoto zinazotukabili. Kunahitajika kujitolea kwa kila mmoja wetu bila ubinafsi ili taifa letu linyanyuke. Na huu ndio wetu wangu kwa vijana wa taifa hili. Ni wajibu wetu kujenga taifa hili na sio kulibomoa.

Jamii zetu lazima ziwe moja katika malezi na makuzi ya watoto wetu kwakuwa bila malezi bora ya vijana na watoto wetu baadae ya taifa hili itakuwa hatarini. Baadae ya taifa hili inategemea sana malezi na makuzi ya watoto na vijana wetu kwasababu wao ndio watakaokuja kuendesha taifa hili baadae. Kuendelea au kuharibika kwa taifa hili kutategemea sana jinsi gani tunawalea watoto wetu na aina gani ya elimu tunawapa. Kunategemea sana nidhamu zao na uelewa wao. Kunategemea sana ni jinsi gani wanaheshimu taifa lao na jinsi gani wanaheshimiana. Kwahiyo ili tujenge raia bora ni lazima tuangalie elimu na malezi tunayotoa na jamii zetu lazima ziwe na umoja. Ni lazima jamii zetu ziwe na malengo ya pamoja kwenye elimu na malezi ya watoto wetu. Ni lazima tujue taifa hili ndio lilotuunganisha kutoka makabila mengi na dini mbali mbali na kama taifa ni lazima tuwe na malengo. kwakuwa hakuna mtu anayeweza kufanikiwa akiwa peke yake. Mafanikio makubwa tutayapata tukiwa tunaishi ndani ya jamii na ndani ya taifa. Ulinzi wetu na maendeleo yetu inategemea sana uwepo katika taifa na ufanyaji kazi wetu kwa pamoja. Kwahiyo hatuwezi kufanikiwa tusipofanya kazi pamoja.

Kuna wajibu tatu muhimu kwa taifa lolote lile ili liendelee. Wajibu wa mtu kwa taifa lake, wajibu wa mtu kwa familia yake na jamii yake na wajibu wa mtu kwake binafsi. Bila wajibu hizi tatu hatuwezi kuendelea. Tunawajibika kwa taifa, kwa familia na kwa jamii. Na ni muhimu kuulizwa tusipowajibika. Kwahiyo kipindi hiki cha uchaguzi katika taifa letu ni wakati wa kukaa na kutafakari kuhusu utaifa wetu. Siasa sio ushabiki. Siasa inahitaji akili kwasababu inahusiana na maisha ya watu. Kwahiyo tutafakari siasa tulizonazo. Inahitaji busara kuingia kwenye siasa na katika uongozi. Ni dhahiri kwamba mataifa yaliyoendelea hayakuendelea kwa kubahatisha au kwa bahati mbaya ni matokeo ya siasa nzuri na uongozi bora. Walikuwa wanajua walichokuwa wanakifanya na walikuwa wanajua wapi walikuwa wanataka kuelekea. Wakaamua kuanza safari iliyowachukua miaka kufika hapo walipofika ambapo sasa tunawashabikia na kuwaona bora. Ni kazi kubwa walifanya kunyanyua mataifa yao. Hii kazi iko mbele yetu sasa. Inahitaji utayari wetu kuifanya. Inahitaji kujitolea kwetu kwasababu hakuna kitakachobadilika kama hatutafanya kazi. Naamini tunaweza kubadilisha historia kwasababu nguvu ya kubadili taifa hili iko mikononi mwetu wanawake na wanaume wa taifa hili. Tuna uwezo wa kubadili taifa hili kama tukiamua ni suala la kuchagua tu na kuwa tayari kujitolea kufanikisha idea ya kuwa taifa kubwa na linalo jitegemea hakuna alichokiweza binadamu kinachoshindikana. Ni matumaini yangu watu wa taifa hili wataanza kufikiria ni jinsi gani wanaweza kulifanya taifa hili kubwa na linalo heshimika.
 
Back
Top Bottom