Tuna kazi kubwa kujenga maadili ya Taifa

nivoj.sued

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
221
190
Tuna kazi kubwa kujenga maadili ya Taifa
Padre Privatus Karugendo
Mwananchi
Toleo la 6 Agosti 2016

Tumempongeza Rais, wetu kwa kutumbua majipu, na tunaomba aendelee kufanya hivyo.

Sambamba na hilo la kutumbua majipu, tunapenda kwa nia njema kujikumbusha sisi wenyewe, kumbukumbusha Rais wetu na Watanzania wote, kwamba kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kujenga upya maadili ya Taifa letu.

Hatuwezi kupuuza ugumu na hatari iliyopo katika kuyatumbua majipu; tunajua wazi kwamba hii ni kazi ya kujitoa mhanga, tunachokifanya ni kujaribu kwenda mbali zaidi ya utumbuaji. Majipu ni ugonjwa na kawaida hakuna ugonjwa unaokuja bila chanzo.

Majipu, yanajitokeza, kwa vile maadili mema ya Taifa letu yamepotea.Ni muhimu kutambua kwamba kazi hii ya kujenga maadili ni ya Watanzania wote.

Kujenga maadili ya kitaifa si kazi ya makanisa wala misikiti, si kazi ya Serikali au vyama vya siasa, ni kazi ya Watanzania wote, maana hiki ni kitu kinachotugusa sote, tutake tusitake.

Panya road wanaposhambulia, hawaangalii sura ya mtu, dini ya mtu, chama cha siasa cha mtu. Wanatafuta fedha, chakula na mali nyingine.

Mafisadi, ‘wanapopiga’ fedha za umma, hawangalii sura ya mtu au kujiuliza fedha hizo zingesomesha watoto wangapi, zingetibu wagonjwa wangapi na wala hawajiulizi kwa kufanya hivyo wanawaumiza wanachama wenzao kwenye vyama vya siasa, au kuwaumiza waumini wenzao makanisani na misikitini.

Maadili mema yakipotea, utakuwa muuaji, utabugia madawa ya kulevya, utakuwa fisadi, utasema uongo, utakuwa mlevi na kutumbukia kwenye vitendo vya ngono, utaingia kwenye umoja wa kujenga nyumba ndogo, utafanya mambo mabaya ambayo hayawezi kuleta maendeleo ya kudumu kwako na kwa watu wanaokuzunguka.

Ni lazima tutambue kwamba kinga madhubuti ya haki za raia, uhuru wa raia, na mambo yote wanayoyathamini, hatimaye yatahifadhiwa na maadili ya kitaifa.Taifa linapokosa maadili yanayoiwezesha Serikali kusema hatuwezi kufanya hivi, huu si Utanzania.

Iwapo watu hawana maadili ya aina hiyo, haisaidii sana hata kama tungeyatumbua majipu yote na kuwa na Katiba iliyoandikwa vizuri sana.Bado raia wanaweza kukandamizwa na majipu kuota upya.

Tunachopaswa kukifanya ni kujenga maadili ya Taifa hili, kila mara kuimarisha maadili ya taifa hili, maadili yatakayomfanya Rais yeyote yule kusema ninayo madaraka ya kufanya jambo hili chini ya Katiba, lakini sitalifanya, maana huu si Utanzania.

Tujiulize, Utanzania, unanyesha kama mvua? Unaweza kujenga Utanzania kwa kuhutubia tu majukwaani? Inatosha kuzaliwa Tanzania,mtu akatenda na kuishi Kiutanzania?Mtanzania wa kweli mwenye maadili bora ya Kitanzania, hawezi kuisaliti nchi yake, hawezi kuipora nchi yake.

Mtanzania wa kweli ni mzalendo. Mtanzania wa kweli analitanguliza taifa bila kuangalia kwanza maslahi yake binafsi, analitanguliza taifa bila kutanguliza tumbo lake.Huyu yuko tayari kuyapoteza maisha yake kwa kutetea uhai wa taifa lake.

Ili kuujenga Utanzania, mwalimu Julius Nyerere na waasisi wengine, walibuni mbinu na mifumo mbalimbali kama lugha moja, siasa ya ujamaa na kujitegemea, vijiji vya ujamaa,kuwasambaza watoto kwenye shule za mikoa mbalimbali, Jeshi la Kujenga Taifa, Mwenge wa Uhuru na mengineyo.

Hali ikoje?Leo hii lugha yetu tunaipiga vita. Tunataka kutumia lugha za kigeni! Ujamaa tumeuweka kaburini. Vijiji vya ujamaa havisikiki tena. Mwenge wa huru umetaifishwa na CCM, badala ya kujenga umoja wa kitaifa unatumika kukipigia debe Chama cha Mapinduzi.

Tuna mbinu gani za kujenga Utanzania?Ni nani mwenye sera ya wazi ya kuujenga Utanzania? Tusijidanganye na kuamini kwamba jambo hili linaweza kunyesha kama mvua.Ni jambo la kufanyia kazi.

Na mwenye nafasi ya kufanya jambo hili, hawezi kupata nafasi ya kujilimbikizia mali, nafasi ya kuwa na viwanja na kujenga nyumba kila mkoa, Mwalimu Nyerere, alikuwa na nyumba ngapi? Kwa nini hatupendi kujifunza?Mwalimu, alikuwa rais wa kwanza wa Taifa letu, watu wengi walikuwa hawajawa macho kama ivyo sasa hivi, angeweza kujenga nyumba zake kila wilaya na kila mkoa.

Kwa vile alikuwa na maadili mema, hakufanya hivyo. Kwa nini tusijifunze kutoka kwake? Je, nyuma yake ameacha vitabu vingapi vyenye sera, dira, falsafa na mambo mengine mengi ya kuujenga Utanzania na ubinadamu?Kujenga Utanzania, kunahitaji umakini.

Huwezi kushinda na kulala kwenye pombe, kufukuzia dogodogo, kujenga nyumba ndogo, kugombania viwanja, kufukuzia asilimia 10 kwa kila mradi upitao, ukapata muda na uwezo wa kujenga dira ya Kitanzania.

Hoja hapa ni kwamba sambamba na utumbuaji wa majipu, tuwe na mfumo wa kujenga fikra. Tuwe na mfumo wa watu kupenda kusoma vitabu na maandishi mengine ya kutupanua kifikra na kutuingiza kwenye uwanja wa uchambuzi na tafakuri.Binadamu ni kiumbe wa kuchambua mambo na kuyatafakari.

Binadamu akiacha kufanya hivyo, ni lazima awe kama wanyama wengine. Ni lazima atajiangalie yeye mwenyewe na kuyajali maisha yake, bila kutimiza wito wetu wa hapa duniani wa kuishi pamoja, kupendana na kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Majumba yamejengwa, viongozi wetu wanavaa suti za Ulaya, wanaendesha magari ya bei mbaya, ofisi zinapendeza – lakini uko wapi urithi wa vitabu? Ni nani anaandika, ni kiongozi gani anakaa chini kusoma,kufikiri na kutunga sera.

Viko wapi vitabu hivi tuvisome. Viongozi wetu wa sasa wanaongozwa na falsafa ipi? Ni nani mwenye kuitetea falsafa hiyo.

Tunahitaji mabadilikoTunahitaji mabadiliko. Na hapa haina maana ya kuingia Ikulu, ndipo tulete mabadiliko. Kazi ya kuleta mabadiliko ni yetu sote, viongozi wa Serikali, viongozi wa upinzani na watu wote wa Tanzania.

Bila kubadilika, hatuwezi kujenga kwa pamoja maadili ya Taifa letu, na bila kujenga maadili ya Taifa letu, ni ndoto kuleta maendeleo tunayoyatamani.

Ni vigumu kuijenga Tanzania, tuitakayo, bila kujenga kwanza maadili mema. Kwa jambo hili hatuna uchaguzi zaidi ya kukubaliana juu ya mradi huu wa pamoja wa kujenga maadili ya taifa letu.Siasa, zitatofautiana, dini zitatofautiana, lakini maadili ya Taifa letu, UTanzania, wetu ni lazima ufanane.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii anapatikana kupitia:
Email: pkarugendo@yahoo.com
Simu: 0754 633122.
 
Back
Top Bottom