Tumshukuru Mungu kwa maisha tuliyojaaliwa kuwa nayo.

Amani Dimile

JF-Expert Member
Jul 27, 2022
243
395
Baada ya kushika kalenda na kuzihesabu siku hatimae nimegundua tajiri na maskini wanaishi siku sawa ndani ya mwaka mmoja. Yaani siku 365.

Lakini furaha na amani zinatofautiana miongoni mwao, majukumu ya kuyatimiza huenda ni yale yale, ila nguvu wanazotumia kutimiza majukumu hayo ni tofauti.

Nashindwa kulizuia chozi langu kutiririka katika shavu langu, mikono yangu inapata kigugumizi kufuta shavu langu linaloloa kwa machozi ya moto yenye huzuni, majonzi na hisia kupita kifani.

Tunaishi katika dunia moja ila yenye maisha tofauti kwa kila mmoja. "Eeh! Mwenyezi Mungu kisikie kilio chetu sisi watoto wa kimaskini"

Na tena naomba mkionana na yule aliyesema "mchumia juani hulia kivulini" basi mwambieni kauli yake haina maana tena kwenye karne hii. Sababu watu wanatafuta kwa shida na bado wanakula kwa shida.

Wengine wanatafuta kwa shida na bado wanakufa wakiwa kwenye shida, "Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema" Amina.

Furaha ya maskini ni kulala, si sababu ya uvivu wala si sababu ya uchovu bali sababu ya ndoto. Maskini anapolala huota ndoto tamu na njema ila akiamka anakutana na maisha halisia yenye shida na tabu. "Ndoto ni tamu kuliko uhalisia wa maisha yetu"

Nani anasema duniani kuna usawa, yupo wapi, nawauliza ninyi yupo wapi huyo mtu anaesema duniani kuna usawa ??
Hakuna hakuna, narudia tena hakuna usawa duniani sababu kipindi ambacho wewe unasema "utakula nini" yupo yule mtoto wa kigogo aliyezoea kula na kusaza anawaza "atakula na nini".

Lakini ndugu zangu, kama tumechagua kuwa waungwana basi ni lazima tukubali kuwa mipango ya Mungu ni sahihi sana kuliko mategemeo yetu. Acha tuishi kama anavyopenda yeye.

Tusitafute mafanikio kwa njia za haraka zisizo za halali, sababu tunaweza ona sisi ni wajanja sana ila Mungu na Muda ni wajanja kuliko vyote. "Mheshimu na Umuogope sana aliyekuumba, sababu pesa zinatabia ya kuisha"

Finally, Tumshukuru Mungu kwa maisha tuliyojaaliwa kuwa nayo hata kama si yale ambayo tulitegemea tutakuwa nayo.

Katika kalamu ni yule yule kijana wenu Amani Dimile

#amanidimile #tungomaridadi
1699359234952.jpg
 
Back
Top Bottom