Tumbo joto

Ahmad Mussa

Member
Oct 21, 2011
46
19
(Haki zote zimehifadhiwa, hairuhusiwi kuiga kunakili au kutumia sehemu ya simulizi hii
kwa namna yoyote ile bila ya Ruhususa ya Mwandishi) Nawatakia usomaji mwema.

SURA YA KWANZA

USIKU


Saa 3.36 gari ndogo aina ya Toyota Allion lilisimama eneo lisilo maalum kwa maegesho ya magari karibu kabisa na eneo la mapokezi la hospitali ya Amana. Kijana mwenye umbo la wastani akateremka kwenye gari na kuelekea kule alikodhani kuwa ni mapokezi. Watu wengine wawili wakateremka kwenye gari na kusimama nje. Mmoja alikuwa mwanamke mnene ambaye umri ulishaanza kumpungia mkono, mtu wa pili alikuwa ni dereva ambaye alielekea kwenye boneti na kuiegemea huku akitikisatikisa funguo.
Mara wauguzi watatu mmoja wa kiume wawili wa kike wakiwa wameongozana na Yule kijana aliyeteremka mwanzo walikuja kasi huku wakisukuma machela kwa mikono yao.



"Zunguka kule!" aliamrisha Yule aliyerudi na wauguzi akimuelekeza mwenzake aende upande wa pili. Akaenda upande wa pili akafungua mlango. Wauguzi wakaja upande ule na kumsaidia Yule jamaa kuutoa mwili wa mtu ambaye haikufahamika wazi kama alikuwa hai. Kwa kusaidiana na wale wauguzi wakanyanyua kiwiliwili kile ambacho hakuna aliyekuwa na uhakika kama kilikuwa hai au vinginevyo!
Shuka nyeupe ambayo kiwiliwili kile kilifunikwa kwayo ilikuwa imelowa damu. Kikiwa na shuka yake walikichukua na kukilaza juu ya ile machela kisha wakaanza kuikimbiza kuelekea chumba maalum. Kazi hiyo ilifanywa na wale wauguzi watatu.



"Vipi dokta wa zamu amefahamishwa?" Aliuliza muuguzi mmoja wa kike. "Dokta Maulidi yupo Ofisini kwake hajaondoka na ameshadokezwa!"
"Wewe nenda chumba hicho cha daktari ukatoe maelezo" aliamrisha yule muuguzi wa kiume huku akitoa ishara kwa mmoja kati ya wanaume wale wawili walioleta kile kiwiliwili. Yule mwanaume akakimbia kuelekea chumba cha daktari huku akiwa na uso wenye taharuki. Baada ya dakika chache akatoka akiwa ameongozana na daktari. Walipofika pale kwenye korido daktari akaendelea na safari yake kuelekea chumba ambacho mwili wa Yule mtu umepelekwa.


Daktari akatembea kwa kasi hadi kwenye mlango ule wa vioo wenye pazia la kijani ambalo lipo kwa ndani. Baada ya dakika chache muuguzi mwingine akatoka mle chumbani kwa kasi, akaingia kwenye chumba kingine ambacho kilikuwa mbele kidogo ya korido ile. Baada ya takribani dakika tano yule muuguzi akatoka ndani ya kile chumba. Akatembea kwa kasi kuelekea chumba kile ambacho kiwiliwili kilikuwa kimepelekwa.

Pale kwenye viti wale wanaume wawili na yule mama mtu mzima walikuwa wametulia huku kila mmoja akionyesha hofu ya wazi. Kila mlango wa chumba kile maalum ulipofunguliwa wote walielekeza macho yao huko kana kwamba kuna kitu wanatarajia kusikia.


Baada ya dakika chache askari wanne wawili wakiwa na silaha wakafika pale walipokaa wale watu watatu. Kabla hawajaongea lolote madaktari wengine watatu wakakatisha pale kwenye korido kuelekea chumba kile maalum. Wale polisi hawakuonekana kuwa wageni wa tukio lile hivyo walisimama bila kuuliza chochote.



Huku wakiwa na hofu ambayo iliwaondolea machungu ya kung'atwa na mbu waliendelea kukaa pale kwenye korido huku wakiwa kimya. Hakuna aliyekuwa na hamu ya kuongea chochote. Daktari akasimama mlangoni na kumwita mmoja kati ya wale wanaume wawili kwa ishara ya mkono.


Akasimama yule aliyekuwa anaendesha gari akatembea haraka kuelekea kule aliko daktari. Daktari akaongea kwa sauti ya kunong'ona huku jamaa akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na maelezo ya daktari. Wote waliosalia pale kwenye korido walikuwa wametega masikio kwa matarajio ya kusikia alichokuwa anaongea daktari, hakuna aliyesikia.
"Lulu mwananguuu!" Alianza kulia yule mama mtu mzima kwa sauti ya chinichini huku akiwa na hofu ya wazi juu ya taarifa atakayoletewa na yule anayemsikiliza daktari.



Daktari akarudi tena kwenye chumba kile maalum. Wakati jamaa anarudi wote wakasimama na kumzunguka.
"Anasemaje?" aliuliza askari mmoja huku akionyesha wazi kuwa na hofu kubwa ya jibu atakalolipata. Yule mtu akainua uso wake na kuwatazama wale waliomzunguka kwa sura iliyokata tamaa.
"Muhimbili!" Lilikuwa jibu fupi lililoeleweka.
Wakashusha pumzi baada ya kugundua kuwa kile walicho hofu moyoni mwao hakikuwa.



SEHEMU YA PILI
Sura ya kwanza

Ndani ya uzio wa majengo ya taasisi ya mifupa ya muhimbili. Wale watu waliendelea kung'atwa na mbu wakisubiri kujua hatma ya mgonjwa wao. Askari wawili walikuwa wameondoka na kubaki wawili wenye silaha. Muda wa kusubiri ulikuwa mrefu hakuna aliyeongea.
Hatimaye kulikuwa kumepambazuka. Watu wakaanza kuingia na kusubiri ruhusa ya kuingia wodini kutoka kwa wauguzi na madaktari. Wengi walikuwa wamesimama kando ya milango ya Wodi za SEWA HAJI na KIBASILA.


Pale waliposimama wale waliomleta mgonjwa usiku aliongezeka mtu mwingine ambaye alisimama kando na kujifanya kama hana habari nao. Macho na masikio yake yalikuwa kwao katika namna ambayo hakuna ambaye angeweza kugundua.



Dakika chache baadaye akaja mmoja wa madaktari. "Nani wahusika wa Lulu!" "Sisi hapa!" Walijikuta wakijibu kwa pamoja.
"Hapana sihitaji askari nahitaji ndugu kwanza!" "Lulu ni afande mwenzetu mkuu!" Alijitetea askari mmoja ili kuonyesha kuwa hayuko kikazi tu. "Anhaa! Sasa nawaomba mje huku ofisini!" Huku nyoyo zao zikienda kasi wakamfuata daktari. Wakaingia kwenye chumba no. 26 A ambacho kilikuwa na ubao wenye maandishi mlangoni Dr. Msokile. Wote kwa pamoja wakaingia ndani ya chumba kile kidogo.


Ni chumba ambacho kilionekana wazi kuwa kimeandaliwa kwa ajili ya faragha ya mgonjwa na daktari. Ndani ya chumba hiki kulikuwa na vifaa vingi vya kidaktari na kitanda kidogo ambacho bila shaka kilitumika kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa awali wa matatizo ya mgonjwa.
"Enhe ndugu wa karibu zaidi wa mgonjwa!" Alihoji daktari. "Huyu ni mama yake mzazi, huyu ni mumewe, hawa ni wafanyakazi wenzake na mimi ni jirani yao!" Alifafanua mmoja kati ya wanaume waliomleta mgonjwa hospitali. "mi nafikiri hakuna haja ya mzunguko mrefu, ninasikitika kuwafahamisha kuwa pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na madaktari lakini imeshindikana kuokoa maisha ya mgonjwa. Nasikitika kuwafahamisha kuwa mgonjwa wenu amefariki dunia!"



Baada ya hapo kikafuata kilio kutoka kwa mama mzazi wa Afande Lulu. Kilio hicho kiliandamana na maneno ya kuomboleza. "Wamemuua mwanangu wameemuua, nimewaona jamani wamemuua……" Aliendelea kulia yule mama.

Yule mtu ambaye mwanzo alikuja na kusimama kando yao bado alikuwa anawafuata kwa siri huku akisikiliza kilio cha yule mama. Ni kilio ambacho kwa kiasi fulani kilimshtua yule mtu na kumtisha. Alikuwa na sababu ya kutishwa na kilio hicho kwani kiliambatana na maneno ambayo hakutaka kuyasikia. "Nimewaona jamani wamemuuaa…….."


Nimewaona? Swali lisilo na majibu lilipita kichwani mwake. Akaachana na ule msafara ambao ni wazi ulikuwa kwenye huzuni na kilio. Pia watu wanaomfahamu marehemu wakazidi kuongezeka. Uongezekaji huo ulimtisha mfuataji kwani makachero na maafande wa kawaida walikuwa wanazidi kumiminika.



Haraka haraka akajitenga na kundi lile la watu akaingiza mkono katika mfuko wa kulia wa suruali yake, akachomoa simu yake ya mkononi akaangalia huku na huko akahakikisha kuwa yuko peke yake. Akapiga namba alizozihitaji. Huku akionekana mwenye wasiwasi mkubwa.
"…..Eeeh! analia halafu anasema anajua kila kitu!" "….Ndiyo!" "Makachero ni wengi sana sijui tufanye nini? " "Ok ni njia nzuri ngoja niwapange wamalize kazi!" Alikuwa anaongea na mtu kwenye simu huku akipoteza kabisa utulivu kwa kuangalia huku na huko kwa wasiwasi.

ITAENDELEA..........


 
Back
Top Bottom