Tulioumizwa tutafakari kwa sauti hapa

Kalamu Yangu

JF-Expert Member
Dec 21, 2016
1,099
1,042
IMG_7197.JPG
MOYO MPWEKE
Moyo wangu ni mpweke,kupendwa ninatamani,
Ila nimepigwa teke,hauna tena thamani,
Upo wapi njo udeke,usinombe samahani,
Nani nimweke moyoni,awe radhi myaka yote.

Asiwe kiruka njia, leo wangu kesho sina,
Aiweke yake nia,nami nimpende sana,
Akiona ninalia,anitake kupambana,
Nani nimweke moyoni, awe radhi myaka yote.

Tangu siku ninaachwa, na muhibu tunda langu,
Kutwa kucha ninaachwa, silijui kosa langu,
Nilienda kichwakichwa,nitulize moyo wangu,
Nani nimweke moyoni,awe radhi myaka yote.

Si utani kweli tupu, moyo wangu u mpweke,
Siipendi tena supu,wala mahidi mateke,
Siyajui magrupu,nimeshakuwa mpweke,
Nani nimweke moyoni,awe radhi myaka yote.

Kila moja nina wangu, hakuna aliye singo,
Nikienda wanguwangu,naweza vunjwa mgongo,
Njia yangu sasa chungu,nusu niivunje shingo,
Nani nimweke moyoni,awe nami myaka yote.

Nalala mi macho wazi, nausubiri ujumbe,
Mlango naacha wazi,mawazo we ‘siombe,
Nikipigia wazazi,naiwaza hata pombe,
Nani nimweke moyoni,awe radhi myaka yote.

Hayupo kapata bwana, nabaki nayumbayumba,
Atamba bonge la bwana,tena aitwa mchumba,
Huyu naye ana bwana,wala siyo ombaomba,
Nani nimweke moyoni,awe radhi myaka yote.

Simu sasa nakatiwa, dakika zinabakia,
Eti we wasumbuwa,mume ananipigia,
Pia kaa ukijuwa,mjanja katangulia,
Nani nimweke moyoni,awe radhi myaka yote.

Machozi yanizuia, kuandika ninalia,
Kama upo wasikia,njoo nitakupokea,
Cha msingi zingatia,napenda upende pia,
Niandikie nikujuwe,’kiona waweza penda.
 
Ninapiga Bismillah, kwa jina lake Mwenyezi
Aliyetukuka Mola, Wa pekee aso mwenzi
Nitajaribu inshallah,kuelezea mapenzi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Naliona swali gumu, Lilokosa jibu wazi
Lataka mtaalamu, Alojaliwa ujuzi
Pia mie ninahamu, Kuyaelewa mapenzi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Ninamkumbuka babu, Wa zamani marehemu
Aliyetoa jawabu, Kusema kila sehemu
Mapenzi kitu ajabu,Na hasa kwa binadamu
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Mpende akupendaye, Ndio raha ya mapenzi
Yule akuchukiaye, Takufanyia ushenzi
Ni msemo wake yeye,Alonena toka enzi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Nimejaribu uliza, Kwa waliofunga ndoa
Waweze kuniongoza,Nami nipate kuoa
Nikaambiwa tongoza,Mambo yatakuwa poa
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Wanaume tuna tabu, Tutafutao ni sisi
Waeza pata aibu, Kwa tamaa kama fisi
kwanza piga mahesabu, Usitake vya upesi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Mapenzi yakuridhisha, Kuyapata si rahisi
Kwa kweli inatutisha, Na kutupa wasiwasi
Maana ndio maisha, Ya kila mtu binafsi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Unaeza kudhania, kwamba umeshampata
Mzuri kupindukia,Na wala aso matata
Mara ukashitukia,Mwengine kamfuata
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Duniani kuna mambo, Siku hizi mpaka pesa
Wanazipenda warembo,Ni mtindo wa kisasa
Usije jitoa chambo, Mwishowe ukamkosa
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Tabia zao mabinti,Huwa wana lao lengo
Ukifanya utafiti, Utakuta ni waongo
Kwanza atakudhibiti, Baadaye ni maringo
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Sio hapa tu mjini, Mapenzi yatuadhibu
Mpaka na vijijini, Utaona maajabu
Madawa wanaamini, Waganga na matabibu
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Hujasikia walimu, Waitumiao dini?
Mapenzi kuyafahamu,Kuelewa kwa undani
Wakamvuta Saumu, KWa kufukiza ubani
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Nimetatizwa na swali,Lako we kaka Omari
Isitoshe usijali, Nazidi kutafakari
Jibu lake si kamili, Wasemavyo ni kadari
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako

Japo moyo waumia, Usichoke kusubiri
Ni kweli umekawia,Vumilia kijasiri
Ipo siku nakwambia,Utampata mzuri
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom