SoC01 Matatizo makubwa yanazaliwa kwa utatuzi mbaya wa tatizo dogo

Stories of Change - 2021 Competition

Allynho 12

New Member
Apr 10, 2021
3
2
Kilichonifanya niandike ujumbe huu ni baada ya kukutana na kisa kimoja kilichonitoa machozi. Ilikuwa kama mida ya saa saba mchana rafiki yangu (jina nalihifadhi) alinifata nyumbani kwangu napoishi, nilimkaribisha ndani bahati nzuri alifika mda ambao nilikuwa napata chakula cha mchana na familia yangu, aliketi na sisi tukapata chakula kisha tukaenda chini ya miti kupunga upepo maana nyumbani kulikuwa kijijini kidogo haukua mji ambao tayari umeshajengeka. Basi stori mbili tatu zikiiendelea ndipo rafiki yangu aliponipa kisa ambacho leo hii kimenifanya niandike makala hii kwa Watanzania wote wasome huenda wakapata funzo ambalo mimi nililipata. Mwanzo liniona ni jambo dogo sana lakini kadri mda ulivyozidi kwenda nilielewa nini kipo ndani ya kisa hiki cha kuhuzunisha.

Rafiki yangu aliingia mfukoni akatoa karatasi zisizopungua tatu ambazo mwandishi wa karatasi hizo alionekana ni mtoto mdogo asiyezidi umri wa miaka kumi na nane. Zilikuwa ni mfano wa barua au hotuba kisha akanambia soma hizi karatasi ndugu yangu huenda ukajifunza kitu siku ya leo. Kama unavyojua Watanzania ni wavivu wa kusoma sikuwa na shauku ya kusoma yaliyoandikwa kwenye karatasi zile nikamwambia nitazisoma nikitulia, alijibu haya kisha akaniaga anakwenda zake ila alinihusia sana nizisome zile karatasi huenda nikajifunza kitu.

Kutokana na uchovu sikumsindikiza umbali mrefu tuliagana kisha akaenda zake na mimi nikarudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu zingine. Mida ya saa mbili mbili hivi usiku nilikuwa mpweke sana familia yote ililala kutokana na mazingira tunayoishi hayakuwa na umeme hivyo hakukua na runinga yakupoteza poteza mda, mbu wengi kutokana na nyasi nyingi zinazozunguka eneo letu ilikuwa ni lazima ulale mapema tu ukijifanya mgumu hakika mbu watakuadhibu ipasavyo.

Nilikuwa sina cha kufanya kutokana na upweke na usingizi pia ulikuwa mbali na macho yangu, nikakumbuka rafiki yangu aliniachia makaratasi mchana nikasema ndo wakati wa kuyasoma sasa japo mwanga wa sola ukikuwa hafifu wenye lakini sikuwa na jinsi maana hakukuwa na cha kufanya na usingizi umegoma kuja. Karatasi ziliandikwa namba kwa juu,kwa haraka haraka nikahisi sio mwandishi aliezipa namba karatasi zile bali ni rafiki yangu kufanya wepesi kwa mtu mwingine kuzisoma. Nikaanza kusoma karatasi namba moja nikagundua kuwa ni hadithi imeandika moyo wangu ukawa unasita kusoma maana hadithi nyingi ni zakufikirika na za uongo nikahisi hakuna funzo naweza kulipata zaidi ya kuumiza macho yangu tu na mwanga hafifu wa taa ya sola.

"Bwanaweee acha nisome nipoteze muda maana hata nisiposoma hakuna kitu cha kufanya mda huu" sauti ya ndani ilinilazimisha kusoma nahisi ilijua ujumbe mzito uliopo kwenye makala ile.Zoezi la kuanza kusoma makala ile likaanza na hivi ndivyo ilivyoandikwa:

"Jina langu naitwa Yilla ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa mzee kiwia. Pia ni mtoto wa pekee wakike wa familia yangu,maisha ya nyumbani hayakuwa mabaya sana wala magumu sana. Baba yangu alikuwa mfanyabiashara na mama yangu alikuwa mwalimu wa shule ya msingi mapololo shule ambayo nilikuwa nasoma kabla sijamaliza darasa la saba na kujiunga na shule ya sekondari mapololo.Maisha yangu kiujumla yalikuwa magumu sana kutokana na tatizo langu ambalo lilikuwa linanisumbua toka nazaliwa.

"Nilikuwa na tatizo la kujikojolea kitandani lilinifanya nitengwe na familia na hata kukosa marafiki.Nilipoteza marafiki wengi sana kwa mda mfupi kutokana na tatizo hili, mwanzo haikuwa ngumu sana kwasababu nilijitahidi kujiweka safi ili marafiki zangu na watu wangu wakaribu wasigundue, nilifanikiwa kwa kiasi flani ila baadae nilishindwa kulificha tena tatizo hili. Mama yangu alianza kutoa nje asubuhi na kisha kunizungusha mtaa mzima watoto kwa wakubwa wanicheke na kunizomea, kiukweli haikuwa rahisi kwangu nakumbuka nilikuwa na umri wa miaka kumi na tatu kidato cha kwanza mama alipoanza kunifanyia hivi alinambia sasa nimekuchoka unaniharibia magodoro kila kukicha huenda hii itasaidia kuacha tabia hii ikakoma kabisa.

Kwangu haikuwa adhabu ulikuwa ni zaidi ya udhalilishaji sikuwa na raha tena wala amani napotoka mtaani kila mtu vidole vilikuwa kwangu watoto kwa wakubwa. Lakini yote haya hayakusaidia mimi kuacha kukojoa kitandani kiukweli sikuwa najielewa wala sikuwa nafanya makusudi nilijikuta tu naamka katika hali ile hivyo sikuwa nadhani kama anachofanya mama kinaweza kunisaidia.

"Sasa mama alipoona bado naendelea na tabia ile ikabidi aongeze mipaka ya kunidhalilisha.Akawa ananipeleka shule anayofundisha asubuhi bila kuoga vile vile kama nilivyolala,ili lilivuka mipaka kutokana na umri wangu kuzomewa na watoto wadogo ambao mimi ni kama dada yao kabisa iliniumiza sana. Aliwakusanya wanafunzi wake wote wanizomee mbele ya walimu wote na mama yangu,walinizomea haswa aibu ilinijaa hili lilizidi kuniathiri kisaikologia sikuwa na amani tena wala furaha tena na maisha yangu.

Hakaona haitoshi mama akaanza kuwaambia marafiki zangu wote kuhusu matatizo yangu,nikaanza kupoteza marafiki wangu wa karibu ghafla aibu zikaanza kunitawala nilikuwa kituko sas mbele ya kila mwanafunzi. Ndoto yangu ilikuwa siku moja niwe mwanasheria ila sasa nikaona kabisa ndoto zangu zinaenda kupotea sizani kama ningeweza kukamilisha ndoto zangu tena. Baba yangu sasa nae akalivalia njuga nilikuwa napokea vipigo kila siku asubuhi kabla sijaenda shule na mama akawa ananipeleka kila siku shule anayofundisha.

"Nilikuwa mpweke sana mda mwingi nilikuwa peke yangu chumbani hakuna marafiki wala mtu yoyote wa karibu aliyekuwa na mimi kila mtu sasa alinicheka nilipokea zarau kila kukicha hii ilinifanya nichukie kuishi. Nilimchukia kila mtu sasa mawazo yaliniandama sio kwamba tabia iliisha kutokana na adhabu nilizopata hapana,niliendelea kukojoa kupokea vipigo kutoka kwa baba na kuzomewa na wanafunzi pamoja na marafiki zangu kila kukicha.Kichwani mwangu lilikuja wazo moja tu kwanini na ishi wakati sifurahii tena maisha? Kuna faida gani ya kuishi dunia ambayo kila siku dharau na kudhalilishwa ndo sehemu ya maisha yangu? Kwanini mimi ndo wa kwanza kukojoa kitandani? Wenzangu wote wanaishi hivi navyoishi mimi?.

"Upweke,vipigo,udhalilishaji vilinifanya nifikirie mambo mengi sana kwenye kichwa changu ndoto zangu zimeharibika sina ndoto tena maisha yamekuwa magumu sana kwangu upweke unaniandama sina tena mtu yoyote wa karibu kila nakopita nanyooshewa vidole.

Nimeamua kufanya uamuzi ambao huenda ukawa waajabu mbele ya watu ila ni bora kwangu kuliko aibu nazopitia kila kukicha nimeamua kujitoa uhai wangu huenda nakoenda kuna amani zaidi ya huku nilipo huenda mungu na malaika wake wakanipa heshima kuliko wanadamu naoishi nao ila kabla ya kuchukua maisha yangu nimeona niache historia hii uenda ikawa funzo kwa wote ambao wanafanya kama haya ambayo nimefanyiwa mimi.

Jamii inapaswa ielewe zipo njia sahihi za kutatua matatizo ya watoto mbali na kupigwa na kudhalilishwa,udhalilishaji na vipigo unatengeneza uoga na upweke ndani yetu ambao unaweza kupelekea matokeo mabaya mbeleni na pia unatengeneza chuki baina ya wazazi na mtoto kama mimi ambavyo nawachukia wazazi wangu sasa hivi na ntamwambia mungu kila kitu mlichonitendea," mwisho wa kunukuu.

Nilijikuta chozi linanitoka sikuamini kama ntakutana na stori ngumu kiasi hiki,niliwaza ndoto za mtoto huyu na hatima yake,niliwaza vipi watoto wengine wanaokutana na kadhia ya namna hii vipi nini kipo kwenye vichwa vyao? Sikuwa na majibu sahihi zaidi ya kujawa na majonzi na simanzi moyoni mwangu.Sikutaka hili liishie hapa nilitamani kulifikisha kwa kila mtanzania kwa sababu hii ndo desturi yetu iliyotutawala tokeapo, Watanzania hatujui kutatua matatizo tunachofanya ni kuzidi kutengeneza matatizo. Lengo langu halikuwa kukupa stori ya msichana yilla, lengo ni kukupa mafunzo yanayotokana na hadithi hii.

FUNZO LA KWANZA
Utatuzi wa matatizo yanayotokea katika jamii yetu yanaweza kupelekea matatizo makubwa zaidi ya ambayo tunahangaikia kuyatatua.wazazi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kujaribu kurekebisha watoto wao kuliko maarifa jambo ambalo linapelekea watoto wengi wa kitanzania kuathirika kisaikologia kutokana na vipigo na hata kufokewa.Watoto wengi wa kitanzania tumepoteza kujiamini tunapokuwa mbele ya familia zetu na hata jamii kutokana na njia mbovu wanazotumia wazazi wetu katika kutatua changamoto zinazotukabiri,tunashindwa kufanya jambo tukihofia kupigwa au kufokewa kama tukakosea.Utawala wa kimabavu unaotumiwa na wazazi juu ya watoto unafanya watoto wengi wa kitanzania kukosa kujiamini na kuamini mawazo yao kwa kuhofia kama watakosea basi vipigo vitahusika.

FUNZO LA PILI
Udhalilishaji wa watoto sio njia sahihi ya kutatua tatizo bali ni njia sahihi ya kumuongezea uoga na upweke ambao unaweza kupelekea maamuzi mabaya mbeleni.kumdhalilisha mtoto ni njia sahihi sana ya kumfanya mtoto awe muoga pindi anapokuwa na wenzake na familia yake,pia ni njia sahihi sana kama unahitaji mtoto wako awe mpweke kama ambavyo yilla alikuwa mpweke kutokana na kila mtu kujua aibu yake,angeongea na nani kila mtu angemdharau kutokana na tatizo lake hivyo ikampelekea achukue maamuzi magumu ambayo yaliuondoa uhai wake.Naweza pia nikachukulia mfano wa tukio ambalo lilizagaa kila pande ya afrika, msichana aliyefahamika kwa jina la lufuno mavhunga alijiua baada ya ubaguzi wa rangi aliokuwa anaupata toka kwa watu aliokuwa anasoma nao,upweke na udhalilishaji ndio ulimfanya achukue maamuzi hayo magumu.tukirudi kwenye lengo letu kumdhalilisha mtotot hakutafanya yeye aache kitu ambacho wewe unataka aache bali kutamtengenezea uoga na upweke ambao huenda ukapelekea matatizo zaidi mbeleni.

NINI KIFANYIKE SASA KUEPUSHA MATATIZO ZAIDI

Niliwahi kusoma kitabu cha mwandishi mmoja hivi mashuhuri kinaitwa "how to win friends and influence people" kilichoandikwa na dale carnegie.Katika kitabu chake bwana dale aliandika hivi "Remember that tomorrow when you are trying to get somebody to do something.If, for example, you don’t want your children to smoke,don’t preach at them,and don’t talk about what you want;but show them that cigarettes may keep them from making the basketball team or winning the hundred-yard dash." Akimaanisha: Kumbuka kwamba kesho unapojaribu kumfanya mtu afanye kitu.kwa mfano, hutaki watoto wako wavute sigara, usiwahubirie, na usizungumze juu ya kile unachotaka; lakini waonyeshe kwamba sigara zinaweza kuwazuia kutengeneza timu ya mpira wa magongo au kushinda mbio za yadi mia moja.

Jaribu kakaa na mtoto wako ujue nini anapenda alafu mwambie ukiacha kitu fulani basi ntakupatia kitu flani.mfano unaweza kuta mtoto wako anapenda kucheza mpira au kuimba mwambie kama utaacha kukojoa au kufanya ilo jambo lnalokukataza basi ntakupeleka kiwanjani ukaanze mazoezi au nitakupeleka studio ukaimbe nakadhalika hii itamsaidia kujitahidi kuacha kufanya lile jambo ambalo wewe kama mzazi hupendezewi nalo

Njia ya pili ni ya mazungumzo pia inaweza sana kutatua tatizo la mtoto wako jaribu kukaa chini na mtoto wako mzungumze nini kinamsumbua hasa nini tatizo na ni ipi shida kwake hii inaweza kumsaidia mzazi kutatua changamoto zinazomkabiri mtoto wake kwa haraka na urahisi kuliko kutumia mabavu ambapo hakutamsaidia mtoto zaidi ya kumuathiri kisaikologia tu.

Pia ni vizuri mzazi akaonana na mshauri wa afya au watoto kutokana na tatizo alilonalo mtoto wake hii itasaidia kujua ni njia gani ya kitaalamu mzazi anaweza kutumia kutatua tatizo alilo nalo mtoto wake.

"WATOTO NDIO TAIFA LA KESHO,TULINDE NDOTO ZAO,TUWE NAO KARIBU,TUSIWADHALILISHE,TUTAFUTE NJIA SAHIHI YA KUTATUA MATATIZO NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKUMBA"

ZINGATIO: Majina yote yaliyotumika kwenye makala hii ni ya kubuni hayana uhalisia wowote na makala hii.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom