Tukubaliane kutokubaliana: Anayesimamishwa kwa utovu wa nidhamu ni shujaa?

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
WAKATI nilipokuwa mpenzi wa mpira, nakumbuka tukio katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 1998 ambalo mchezaji wa timu ya Taifa ya Uingereza, David Beckham, alitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia rafu ya ovyo mchezaji wa Argentina, Diego Simeone.
Baada ya mchezaji huyo wa kutegemewa wakati huo kutolewa, Uingereza ilipoteza mchezo huo kwa magoli ya penati na iliendelea kukumbana na vipigo hadi kutolewa mapema.

Mashabiki wa Uingereza na hata meneja wa timu (kocha), Glenn Hoddle, walimlaumu vikali Beckham bila kujali kwamba alikuwa kipenzi cha wengi kwa kushindwa kuzuia hasira zake dhidi ya Simeone kwa kumfanyia rafu ya kitoto hadi kuigharimu timu.

Lililotokea Uingereza hadi kumfanya Beckham mwenyewe kukiri kwamba lilimnyong’onyesha na kumpa umakini zaidi katika soka, ni tofauti sana na hali ilivyo huku kwetu, hasa katika vilabu vya Yanga na Simba ambavyo wengi wanaamini ndivyo hasa kikwazo cha maendeleo ya soko la Tanzania! Watu wanaamini kwamba mpaka vilabu hivi vitakapokufa, ndipo soka la Tanzania litapata nafasi yake katika angaza dunia!

Hapa Tanzania, mchezaji wa Simba au Yanga anapotolewa uwanjani kwa kadi nyekundi kwa kucheza rafu na hivyo kuifanya timu kucheza ikiwa pungufu, mashabiki na hata kocha wanamuona kama shujaa na kuhamishia lawama au hasira zao kwa refa badala ya ‘kipenzi’ chao aliyeleta utoto!
Hali hii, hakuna ubishi kwamba haiweza kumfanya mchezaji huyo kubadilika kama ilivyokuwa kwa Beckham aliyefikia hata kuomba radhi mashabiki na kujitenga kabisa na vitendo vya ovyo uwanjani, bali humfanya naye adhani ameonewa.

Mbaya zaidi haileti fundisho hata kwa wachezaji wengine waliopo na wanaochipukia (watoto). Kila nikiangalia matukio ya ukosaji wa nidhamu ambayo yamekuwa yakifanywa na wabunge wetu kiasi cha baadhi yao kusimamishwa au kufikishwa kwenye ‘mahakama’ ya Bunge hilo kujibu mashitaka, ni kile kile ninachokiona kwa Simba na Yanga pale mchezaji wao anapotolewa kwa kufanya utoto na upuuzi uwanjani.

Kinachotokea ni kwamba mbunge anayetolewa nje ya Bunge kwa utovu wa nidhamu au anayesimamishwa na hivyo kukosa kuwawakilisha wananchi waliompeleka bungeni, huchukuliwa kama shujaa.

Yaani huwezi kusikia kauli za kumkemea za wakubwa wa chama chake isipokuwa kulalamikia mamlaka zilizomchukulia hatua kwa kufanya vitendo visivyolingana na uheshimiwa wake na wakati mwingine kutafuta huruma ya wananchi wasioona mbali.

Tatizo la nidhamu mbovu bungeni limeendelea kuibuka licha ya kukemewa sana katika kipindi cha Anne Makinda, wakati wa Bunge la 10 kwa tunaokumbuka. Makinda alikuwa akiwaonya wabunge mara kwa mara akisema wanaidhalilisha taasisi hiyo nyeti kiasi cha kupoteza mvuto kwa wananchi akisema wameligeuza Bunge kuwa kama soko la Kariakoo.

Spika huyo mstaafu alikuwa akisema kwamba kitendo cha baadhi yao kuongea bila utaratibu pale mmoja wao anapokuwa anachangia hoja, kukosa uvumilivu na kushindwa kupima kauli za kuongea, kilikuwa kinaharibu taswira nzuri ya Bunge kwa watu wanaofuatilia shughuli zake. Aliwahi kukaririwa akisema: “Napigiwa simu nyingi na kuandikiwa ujumbe.

Image (taswira) yetu mbele ya jamii siyo nzuri. Kuongea bila utaratibu tunatumia muda, ambao wachangiaji wangekuwa wengi.” Makinda aliendelea kusema: “Jamani tuendelee kukua, tusiendelee kuwa kero kwa watu.

Walikuwa wanapenda sana kuangalia kipindi hiki, lakini sasa wengine wanakereka kwa tabia zetu. Kwa hiyo tubadilike, muwe watu waheshimiwa kama tunavyoheshimiwa na watu waliotuchagua.”
Siku nyingine, katika kikao cha jioni kilichokuwa kikiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge wakati huo, George Simbachawene, Makinda alisema katika kikao hicho kwamba wabunge walifanya vituko vya ajabu kiasi cha yeye (Makinda), kushindwa kuendelea kuangalia mwenendo wa kikao huko alikokuwa.

Akasema: “Hii ni aibu kubwa na sijui kwanini mnajidharaulisha kwa wananchi.
Mnajua watu huko nje wanawaheshimu sana, sasa mkifanya mambo ya ovyo wanawadharau na mjue haya yote yanayofanyika humu yanaonekana. Mimi mwenyewe nilikuwa naangalia, lakini nikashindwa kuendelea kwani nilikuwa naona vitu vya ajabu ajabu.

“Hapa bungeni kuna utaratibu wa kuzungumza, mtu akiwa anazungumza wengine mnapaswa kumsikiliza, lakini jana, mtu mmoja anachangia na wengine wanazungumza utadhani mko Kariakoo.”

Katika kikao hicho alicholalamikia Makinda na kilichoongozwa na Simbachawene, wabunge walikuwa wakiwasha vipaza sauti vyao na kutoa maneno ya vijembe kwa wenzao na wengine wakizomea wachangiaji.

Ingawa ni kweli kwamba Bunge la sasa lina mvutano mkubwa, ushindani na damu changa ya vijana, hivyo huwezi kutegemea kuwa kama Bunge la chama kimoja, lakini nidhamu ya ‘kiutu uzima’ na ‘uheshimiwa’ ni kitu ambacho kila mmoja wetu anakitazamia kukiona na siyo kinyume chake.

Niliwahi kuambiwa kwamba neno ‘shehe’ maana yake ya asili ni ‘mzee’ na maana ya pili ni kiongozi wa kidini anayetoa fa-tawa (majibu ya masuala mbalimbali ya kidini) ambaye anatazamiwa pia kuwa mtu wa makamo au mzee. Hivyo, hata kijana anapoitwa shehe kutokana na elimu yake ya dini, msingi wake ni kwamba elimu hiyo inamfanya awe na busara kama unayotazamia kuiona kwa mzee.

Hali kadhalika, ilitazamiwa pia kwamba, hata wabunge vijana, bila kujali wanatoka upande gani wa chama, wawe na busara zile zile za ‘kibunge’. Kwamba mbunge mwenye umri wa miaka 25, kwa mfano, azungumze na kufanya mambo ya kiungwana na busara huku akipima mila na tamaduni zetu Watanzania kama mbunge mwenye umri wa miaka zaidi ya 60. Kwamba aoneshe adabu ya ‘uheshimiwa’ na pia anapojibishana na wale waliomzidi umri au madaraka, pia hilo lionekane kwenye maneno yake.

Kwamba hata kama mbunge fulani anadhani ameonewa au ametukanwa, ataonekana wa maana sana kwa wananchi pale atakapodhibiti hasira zake na kuonesha uungwana na hata kusamehe kuliko kutunisha msuli, kutoa ukali, kutukana, kupiga vijembe au ‘kujibu mapigo’ kwa njia yoyote ile kama tunavyoona bungeni.

Juzi juzi, katika utafiti wa Twaweza, ulionesha kwamba kukubalika kwa chama kikuu cha upinzani nchini (Chadema) kumeshuka kwa kiwango kikubwa miongoni mwa wananchi.
Binafsi naamini kwamba kushuka kwa umashuhuri wa Chadema, kunachangiwa pia na jinsi kisivyokemea nidhamu ya wabunge wake bungeni, huku kikiendelea kupinga kila kitu kinachofanywa na serikali ya awamu ya tano hata kama kina tija kwa wananchi.

Na kwamba upingaji wenyewe unatolewa bila hekima na busara bali kwa kejeli na lugha isiyopendeza Niliwahi kuandika kwamba, Chadema ingeendelea kubaki katika nafasi yake au hata kupanda juu zaidi kama ingeacha kupinga kila kitu, badala yake ikawa inapongeza mazuri yanayofanywa na serikali na ikiwezekana kufikiri mara mbili na kueleza namna ambavyo yenyewe angelifanya jambo lilelile kwa ubora zaidi kama ingelikuwa madarakani.

Lakini kubwa ambalo naliona, pengine si kwa Chadema pekee bali hata kwa vyama vingine ikiwemo CCM ni hili la kutetea hata watovu wa nidhamu na kuwaona kama mashujaa eti kwa kuwa wamewapiga wenzao vijembe au kuwatukana.

Ni lazima ifikie wakati mbunge wa chama fulani anapofanya utoto bungeni, basi wenzake na mashabiki wao wamkemee pale pale kwani anachangia kupunguza uwezo na nafasi ya ‘timu’ katika kuchangia hoja ndani ya ‘uwanja’ wa Bunge.

Kuwaunga mkono watovu wa nidhamu kutawafanya wabunge kutojirekebisha na kudhani kufanya mambo yasiyoendana na uheshimiwa wao ni ushujaa. Lakini mbaya zaidi ni kuwafundisha watoto kasumba na tabia mbaya ambayo ni kinyume cha maadili ya Watanzania
 
"One man's terrorist is another man's freedom fighter" It is a matter of context!!!!!
 
Back
Top Bottom