Na Mphamvu Daniel
Real Madrid wanakaribia kuja nchini, sio Madrid ambayo ilipata ushindi wa goli2-0 dhidi ya Sevilla kwenye Michuano ya Kombe la Super wiki hii. Hawa ni Madrid maveterani ambao wengi wao walicheza soka miaka ya 1990 na 2000.
Wiki moja kabla ya mechi yao na timu ya Tanzania 11 tayari kila mpenda michezo ana taarifa kamili za hili tukio. Pitapita zangu katika mitandao niliona tangazo likinihamasisha kwenda kutazama mchezo huu kwa gharama nafuu ya shilingi elfu tano.
Rekodi zangu kichwani zinanionesha kuwa hii ni mara ya tatu tuna jaribu kuwaleta 'Real Madrid' nchini, jaribio la kwanza likiwa ni lile la mwaka 2006 wakati wa duru ya kwanza ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete na la pili lilikuwa kama msisitizo tu kuhusu nia ya Serikali ambao Rais aliutoa mwaka 2012.
Taarifa iliyotolewana kampuni ya TSN kuhusu safari hii ya maveterani hao ilibainisha kuwa Real Madrid wanakuja Afrika kwa mara ya kwanza na wao ndio wamefanikiwa kuwaleta.
Mazungumzo yangu nawashabiki kadha wa soka yaligundua kuwa nao wanafurahia ujio wa mastaa hawa, licha ya kuwa ni kitambo kidogo tangu wastaafu soka la ushindani bado wana mvuto na ushawishi miongoni mwa jamii ya wapendasoka.
Nikiwa mdau wa soka,naona tatizo katika ujio huu wa Real Madrid. Washabiki na wadau wengine wanaweza wasione tatizo kwa kuwa ni suala la burudani kwao kuwaona watu ambao walikuwa wakiwaona kwenye runinga na kuwasoma magazetini tu.
Tatizo linakuja pale ambapo tunatumia fedha, muda na nguvu nyingi kwenya jambo ambalo halina manufaa wakati bado hatujamaliza kwanza mambo ya msingi.
Mechi ambayo Stars watacheza na vikongwe hawa wa zamani wa Madrid si mechi ya ushindani na kwa namna yoyote haitawajenga wachezaji wetu kiufundi, na wala kiufundi haina maana kwa akina Figo kwani tayari wameshamaliza soka lao la ushindani.
Mechi hii itakayochezwa Agosti 23 inakuja waakti ambao timu za ligi Kuuzinajiandaa na msimu mpya wa ligi. Maana hapa ni kuwa wachezaji watalazimika kuachiwa na timu zao kuja kucheza mechi ya ridhaa ambayo haiwakuzi kisoka kwa namna yoyote na wala haina malengo ya kijamii zaidi ya biashara kwa watu fulani.
Awali mpango huu ulioasisiwa na Rais Kikwete ulidhamiria kuwaleta Rea Madrid halisi, wakiwa katika ubora wao na sio hawa wanaokuja kwa jina la timu. Mpango huo ulikwama kutokana na kukosa wadhamini,au wafadhili.
Mwandishi maarufu wa makala, Israel Saria akizungumzia jaribio lile lililofeli mwaka 2006 alisema, "Fedha ambayo itatafutwa kuidhamini Real Madrid, kama hoja ni kuleta vilabu, kwanini zisiweze kutumika kuleta vilabu vingine vitatu au vinne kujakucheza Tanzania"
Hoja ya Saria ilikuwa tunatumia gharama kubwa kufanya jambo ambalo halina faida saana kwetu, makosa ambayo miaka nane baada ya kushindwa,tunayafanya tena.
Waweza kusema kuwa hili sio tatizo sana kwa kuwa fedha hizi za kuileta Madrid ya zamani zinatoka kwa mashirika binafsi. Tunasahau ukweli kwamba tunayahitaji sana mashirika haya linapokuja suala la udhamini wa vilabu namashindano.
Takribani mwezi kabla ya ujio huu, tayari shughuli hii imeshajihakikishia udhamini wa uhakika kutoka kwa makampuni makubwa zaidi ya matano wakiwemo FastJet, Tropical na Lake Gas.
Waandaaji wa safari hii wameidhamini wakati ambapo timu za ligi kuu nyingi hazina udhamini wa uhakika kutoka kwa makampuni. Wadau wa soka wamekuwa wakiweka wazi mapungufu haya siku zote, kuwa Soka letu pamoja na mambo mengine linakwamishwa na kukosekana kwa wadhamini ambao kwa kaiasi kikubwa ni mashirika binafsi, hayahaya ambayo leo yanatuletea Madrid.
Sijawahi kuwaona Fastjet au Lake Gas wakijihusisha na michezo katinga ngazi ya taifa,lakini ghafla wameiukia katika ziara ya Madrid Veterani. Haijulikani ni kiasi gani wametupa huko, lakini kwa vilabu na mashirikisho yetu ambayo huwa yanalalama njaa, kingetosha kuwa kiasi cha kuwasukuma angalau kwa mwaka mmoja.
Siku zote mcheza kwao hutunzwa, lakini sisi kwa sababu tunazozijua tumeamua (kwa kujua au kwa kutojua) kuacha makampuni makubwa yadhamini shughuli ambazo hazina faida kwetu.
Moja ya sababu ambazo waandaaji wa ziara kama hizi huwa wanatumia ni kuwa safari yamastaa wa dunia huwa inakuza utalii katika nchi yetu. Danganya toto hii wanaambiwa watanzania wakati iko wazi kuwa mnufaikaji mkubwa wa utalii ni hoteli za kitalii na makampuni ya usafirishaji watalii(anga na ardhi) ambayo mengi yanamilikiwa na wageni.
Dola kadhaa ambazo huwa watalii wanalipa katika vivutio hazilingani na maelfu ambayo wanaacha katika mahoteli na usafiri.
Kamati ya maandalizi ya safari hii ni wafanyabiashara na kwa vyovyote wamelenga faida.Tija katika michezo yetu inayodumaa haipo kabisa katika safari hii.
Ziara kama hizi za maveterani tumeiga kutoka kwa wenzetu wa majuu ambao walishamaliza mambo ya msingi. Waakti ambako hakuna shule za uhakika za michezo zinazomilikiwa na Serikali kuu, wadau wanashadadia matumizi ya kufuru kama haya.
Twende tukawatazame hao Madrid, lakini tukijua wazi kuwa tunacheza kamari. Kutupa muda,fedha na nguvu ambazo zingetufaa mahala kwingine.
+255 713 049 852